Wakati uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ukiwa umepangwa kufanyika Septemba 29, Majaji na wanasheria wametangazwa kuongoza kamati mbali mbali za shirikisho hilo.
Kikao cha kamati ya utendaji kilichoketi jana kilifanya mabadiliko kwenye kamati zake mbali mbali ikiwa ni pamoja na kutekeleza agizo la FIFA lilitolewa Aprili mwaka huu baada ya kusimamisha mchakato wa uchaguzi wa TFF, na kuagiza kwanza yafanyike marekebisho ya Katiba ili kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya Maadili ambavyo ndivyo watashughulikia matatizo ya kimaadili kwa familia ya mpira wa miguu nchini.
Mbali ya kamati hizo, mabadiliko hayo pia yametengeneza ngazi mbili za kushughulikia masuala ya kinidhamu ambazo ni; Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Rufani ya Nidhamu.Jana Rais wa TFF, Leodegar Tenga alitangaza kamati Maadili itaongozwa na Wakili Jesse Mguto akisaidiwa na Francis Kambwe (Msajili Mahakama Kuu), Kamanda Mohamed Mpinga, Profesa Madundo Mtambo, na wakili Evod Mmanda.
Kamati ya Maadili ya rufaa itaongozwa na Jaji mstaafu Steven Hema akisaidiwa na Mwanasheria Victoria Makani huku wajumbe ni Mohamed Misanga (Mbunge), Murtaza Mangungu (Mbunge) na Henry Tandau (mshauri wa Fifa).
Pia Kamati ya uchaguzi ambayo ilikuwa inaongozwa na Deo Lyato sasa itaongozwa na Mwanasheria mzoefu Hamidu Mbwezeleni kwa vile kwa mujibu wa katiba ya sasa ya TFF mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi lazima awe mwanasheria hivyo Hamidu Mbwezeleni ataongoza kamati hiyo akisaidiwa na Moses Kalua (mwanasheria) na wajumbe ni Mustapha Siami (Mwanasheria),Chabanga Ndyamwale (Mwanasheria) na Kitwana Manara.
Kamati ya rufaa iliyokuwa chini ya Idd Mtiginjola sasa itaongozwa na Jaji Benard Rwanda akisaidiwa na Francis Kiwanga (Wakili), Annesteve Msemo (Mwanasheria), Yohane Masala (Mwanasheria) na Allen Kasamala (Mwanasheria).
Akifafanua kuhusu kufanya mabadiliko kwenye kamati ya rufaa ya uchaguzi Tenga alisema "Tuliitaji kuwa na jaji mzoefu kwenye kamati ya rufaa, mkutano ndio ulivyoamua hivyo, na pia mwenyekiti aliyekuwepo (Mtiginjola), alishaandika barua ya kujiuzulu na kutaka asifikiriwe kwenye hili.
Hata hivyo alisema kamati ya nidhamu itabaki kuongozwa na Kamanda Mstaafu Alfred Tibaigana, akisaidiwa na Kambona, Musa Hazan 'Zungu', Yusuf Nzowa (Usalama wa Taifa) na Mohamed Msomali na pia Kamati ya Mgongo Fimbo itabaki kama ilivyo ambapo atasaidiwa na Idd Kipingu, Kibuta, Mshindo Msola na Kamanda Mstaafu Jamali Rwambo.
Pia Tenga alisema Kamati ya marefa wamefanya mabadiliko kwa kuingiza mwenyekiti na Katibu wa Chama cha Marefa ambapo kwa sasa kamati hiyo itaundwa na Kapteni Lugenge, Said Nassoro, Mohamed Mnyaa na Charles Ndagala, wakati ile ya madaktari itaongozwa na Paul Marealle baaada ya dokta Faya kuomba kupumzika wakati wajumbe ni Mwanandi Mwankemwa, Antony Ngome, Helen Msemo, Joachimu Mshanga na Frank Muhonda.