Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
WAKULIMA wa matunda wametakiwa kulima kwa kutumia mbegu bora na kilimo cha kisasa ili kupata soko kwenye viwanda vinavyosindika zao hilo, ndani na nje ya nchi. Aidha wananchi wameshauriwa kulima kilimo kinachostahimili ukame ikiwemo mahindi, mihogo, viazi vitamu na mikunde ili kujihadhali na baa la njaa baadae
Hata hivyo wametakiwa kuhifadhi chakula wakati wa mavuno utakapofika kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kuwa na akiba ya kutosha. Rai hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, alipotembelea kiwanda cha Elven Agri company ltd kilichopo Mapinga na kiwanda cha Sayona kinachomilikiwa na kampuni MAMA ya MMI steel, kilichopo kata ya Mboga wilayani Bagamoyo.
Alieleza, wakulima wengi wanahitaji kulima kwa tija badala ya kupata hasara kwa kukosa masoko. Mhandisi Ndikilo alisema, kwa kutambua hilo, kuna kila sababu ya kubadilika kwa kuona umuhimu wa kulima matunda yaliyo na rutuba bora na yanayojiuza.
"Wataalamu wa kilimo, watendaji wa halmashauri katika idara hii, mtoke maofisini muende kuwapa elimu wakulima hawa ili waweze kujifunza kulima kwa kutumia mbegu za msimu mfupi, kuweka pembejeo na kupalilia, Kwa kutoa elimu za mara kwa mara kwa kufuata teknolojia za kisasa, lazima waende na wakati ili waweze kunufaika kwa jasho lao "alisema mhandisi Ndikilo.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, aliyeshika ndizi, akionyeshwa hatua za uzalishaji katika usindikaji wa matunda kwenye kiwanda cha kusindika matunda cha Elven Agri co. Ltd kilichopo Mapinga, Bagamoyo.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto) akionyeshwa namna bidhaa mbalimbali kama pilipili zinavyofungashwa katika kiwanda cha kusindika matunda cha Elven Agri co. Ltd kilichopo Mapinga Bagamoyo.