Na Bashir Yakub.
Matunzo ya mke kutoka kwa mme ni jambo la lazima. Kwa maana kuwa ni lazima mme kutoa mahitaji kwa mke wake .Hakuna uhiari katika hili. Ni lazima na neno lazima maana yake inajulikana. Ifahamike kuwa matunzo anayotoa mme kwa mke wake si msaada, si hisani, si upendeleo, si zawadi bali ni wajibu.
Matunzo yenyewe ni kama chakula , sehemu ya kulala na kuishi, mavazi, matibabu na kila kitu ambacho ni muhimu kwa mahitaji ya mke husika. Kifungu cha 63(a) cha Sheria ya ndoa kinasema kuwa ni wajibu na lazima kwa mume kumtolea matunzo mke wake.
1.VIPI MUME AKISHINDWA KUTOA MATUMIZI.
Yapo mambo ambayo mke anaweza kuyafanya ikiwa mme wake atashindwa kumtolea matumizi . Mojawapo ni hili la kuruhusiwa kuuza mali ya mme wake bila ridhaa ya mme huyo.
Tutaona likoje hili baadae. Mengine ambayo anaweza kufanya mke ikiwa amenyimwa matumizi ni pamoja na kufungua shauri mahakamani kudai matumizi, na hata kudai talaka ikiwa hali hiyo imekuwa sugu.
2. KUUZWA KWA MALI YA MME.
Kwa ujumla kifungu cha 64( 1 ) cha Sheria ya ndoa kinasema kuwa mke ataruhusiwa kuuza mali ambayo kimsingi inamilikiwa na mme wake kwa ajili ya kujipatia matunzo au mahitaji muhimu ya kwake na/au ya watoto/mtoto wake.
Kuhusu ni kipi kinaweza kuuzwa, wakati gani kiuzwe, kwa masharti yapi tutaona hapa chini.
3. MASHARTI KABLA MKE HAJAUZA.
( a ) Kwanza ambaye anaruhusiwa kuuza ni lazima awe mke halali wa mme huyo. Kimada( concubine) hawezi kuuza mali ya mwenzake. Ni mke wa ndoa tu ndiye anayeruhusiwa. Yaweza kuwa ndoa ya kidini, ya kimila, ya serikali au ile inayotokana na kuishi wote miaka miwili.
( b ) Ni lazima iwe mke amenyimwa matumizi muhimu. Ikiwa hajanyimwa matumizi hawezi kuwa na mamlaka ya kuuza mali ya mme wake.
( c ) Pia ikiwa ana watoto/mtoto na hawana matumizi basi napo anaweza kuuza mali ya mme wake.
( d ) Huwezi kuuza mali ya mme wako kwa ajili ya kujipatia matumizi ya anasa. Matumizi yatakayokupelekea kuuza mali ya mme ni yale ya lazima.