Na Lilian Lundo – MAELEZO
Pombe kali zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki maarufu kama ‘viroba’ zenye thamani ya shilingi Bilioni 10.8 zimekamatwa Jijini Dar es Salaam katika msako wa pombe hizo uliofanyika kuanzia Machi 01 mpaka 03, mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba leo Jijini, Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu operesheni ya utekelezaji wa maelezo ya Serikali ya kusitisha pombe hizo za viroba hapa nchini kuanzia Machi 01, mwaka huu.
“Jumla ya katoni 99,171 za pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (Viroba) zimekamatwa ambapo katoni 69,045 ni zenye ujazo wa na mililita 50, katoni 29,344 zenye ujazo wa mililita 100, katoni 782 zenye ujazo wa mililita 90 pamoja na katoni 10,625 za chupa zenye ujazo wa mililita 100. Thamani yake ni Shilingi Bilioni 10.83,” alifafanua Makamba.
Aliendelea kwa kusema kuwa, jumla ya viwanda 16 vya kuzalisha pombe kali, maduka ya jumla 18, maghala 4, baa 3 na kiwanda kimoja cha kuzalisha bidhaa za plastiki ikiwemo vifungashio vya plastiki vya kufungashia viroba vilikaguliwa katika opesheni hiyo.