WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amekutana na wakuu wa taasisi za kimataifa za WFP, IFAD na FAO na kufanya nao mazungumzo kuhusu namna ya kuendeleza kilimo nchini Tanzania.
Waziri Mkuu amekutana na viongozi hao Alhamisi (Machi 21, 2013) alipowatembelea kwenye ofisi zao jijini Roma, Italia kila mmoja kwa nyakati tofauti.
Mkurugenzi Mtendajiwa Shirika la Umoja wa Mtaifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Bi. Ertharin Cousin, alimweleza Waziri Mkuu kwamba shirika lake litaendelea kutumia bandari ya Dar es Salaam kusafirishia vyakula kwenda nchi zenye uhitaji wa chakula ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa bidhaa kwa maendeleo (Purchase for Progress Programme).
“Tumekubaliana na wadau tunaoshirikiana nao, tuendelee kutumia bandari ya Dar es Salaam kupeleka mizigo Sudan ya Kusini na Uganda kwa sababu ya amani iliyopo nchini Tanzania. Kwa hiyo muamini kwamba sisi ni wadau wenu wa karibu na wa kuaminika,” alisema Bi. Cousin.
Akitoa mfano, Bi. Cousin alisema: “Kuna wakati kulikuwa na njaa kubwa kule Somalia na Zambia wakawa na hifadhi kubwa ya mahindi, lakini tulishindwa kusafirisha mahindi kutoka huko na kuyapeleka yanakohitajika kwa sababu ya hali mbaya ya usalama kwenye ukanda wa magharibi,” alisema.
Akizungumzia kuhusu ukuaji wa miji na kasi ya watu kuhamia mijini, Bi. Cousin alionya kwamba kuna haja ya kuwianisha uendelezaji wa miundombinu kwenye maeneo ya mijini na yale ya vijijini ili kuepuka tatizo la msongamano mkubwa wa watu mijini linalozikabili nchi nyingi zinazoendelea.
Alisema shirika lake limefanya utafiti nchini India na kubaini kuwa kadri kiwango cha ukuaji wa miji kinavyoendelea ndivyo kasi ya wakazi kuongezeka inavyozidi. “Tumeziainisha nchi za Kenya, Tanzania na Ethiopia na kuziweka kwenye mpango maalum ili zijipime jinsi zitakavyokuwa katika miaka 20 ijayo ili zisije kuwa na hali kama ya India hivi sasa,” aliongeza.
Naye, Rais wa Shirika la Kimataifa Kuendeleza Kilimo na Chakula (IFAD), Dk. Kanayo Nwanze alimweleza Waziri Mkuu kwamba shirika lake limeandaa mpando wa miaka mitatu ambao utazihusisha nchi 30 ikiwemo Tanzania ambazo zitafanyiwa impact evaluation kulingana na misaada ambayo zimekuwa zikipatiwa na shirika hilo.
“Tunataka tuangalie hali halisi kule Vijijini, je maisha ya wananchi yamebadilika kulingana na misaada ambayo tumekuwa tukiitoa? Je, wakulima wameongeza uzalishaji? Je wakulima wameunganishwa na masoko? Je, taasisi za kifedha zinawajali wakulima wadogo?” alifafanua Rais huyo wa IFAD.
Alisema hivi sasa wameanza kukusanya takwimu za awali (baseline data) katika nchi husika kabla ya kuanza kufanya tathmini itakayoanza mwaka huu hadi mwaka 2016.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Bw. Jose Graziano da Silva alimweleza Waziri Mkuu kwamba shirika lake limetiliana saini makubaliano na benki ya Rabo (Rabobank) ili iweze kuwasaidia wakulima waliojiunga kwenye vyama vya ushirika.
“RaboBank imekubali kufanya kazi hiyo na imeichagua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zitakazokuwa waanzilishi wa mpango huo (pilot project)… watawasiliana nanyi muda si mrefu kuhusiana na suala hili,” alisema.Aliomba wakati mpango huo utakapoanza, wakulima wa Tanzania wawe tayari kushiriki kwenye mpango huo.
Waziri Mkuu Pinda kwa upande wake, katika nyakati tofauti aliwaarifu wakuu wa taasisi hizo za kimataifa juu ya hali ya uchumi wa Tanzania, Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP), Ukanda wa Kilimo wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT) na mchakato wa kuandaa Katiba mpya.
Alisema ili kuendeleza kilimo, ipo haja ya kushirikiana na wadau kutoka sekta binafsi kama njia ya kuleta maendeleo ya haraka nchini Tanzania. Bado tunayo changamoto ya kukabiliana na umaskini, lakini tunaamini kuwa kilimo ndiyo jawabu la tatizo hili,” alisema.
Waziri Mkuu alikwenda Roma, Italia kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye ibada maalum ya kumsimika Papa Francis iliyofanyika Jumanne, (Machi 19, 2013) kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Mt. Petro mjini Vatican, kisha akaamua kukutana na viongozi wa taasisi hizo.
Waziri Mkuu alirejea nchini Ijumaa, Machi 22, 2013).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
JUMAMOSI, MACHI 23, 2013.