Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, imetuma timu ya Makachero kuja Zanzibar kuungana na wenzao wengine wa Polisi Zanzibar katika Upelelezi wa tukio la kushambuliwa kwa Paroko wa Parokia ya Mpendae Amrose Nkenda (pichani).
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai Zanzibar ACP Yusuf Ilembo, amesema kuwa timu hiyo ambayo inaongozwa na Afisa mmoja wa ngazi ya juu (hakumtaja jina) ina jumla ya Makachero watano waliobobea katika masuala ya upelelezi hapa nchini.
Amesema kuwa nia ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, kuituma timu hiyo kuja hapa Zanzibar, ni kutaka kuengeza nguvu katika tukio hili ambalo linatazamwa kwa aina tofauti hasa ikizingatiwa kuwa aliyeshambuliwa ni Kiongozi mkubwa wa dini na limetokea katika kipindi cha siku kuu ya Krismas.
Amesema Jeshi la Polisi limeamua tukio hili kupelelezwa kwa pamoja kati ya wenzao wa makao makuu ya Polisi Dar es salaam na wa hapa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika katika kumshambulia Paroko huyo wanakamatwa.
Hata hivyo kamanda Ilembo amesema kuwabado Polisi wanaendelea na Upelelezi wa kubaini sababu za kushambuliwa kwa Paroko huyo bila ya kuibwa kwa kitu chochote kutoka kwa mshambuliwa.
Amesema kuna uwezekana kuwa watuhumiwa wameshindwa kuchukua kitu chochote baada ya kubaini kuwa eneo la tukio lisingekuwa salama kwao kwa vile kulikuwa na walinzi na ni eneo ambalo ni karibu kabisa na makazi ya viongozi wengine wa dhehebu hilo.
Akizungumzia siku kuu ya mwisho wa mwaka 2012 na mwanzoni mwa mwaka 2013, Kamanda Ilembo amewahimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa wahalifu ili wachukuliwe hatua.
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amewatahadharisha wazazi na walezi kutowaruhusu watoto wadogo kuranda barabarani ama kwenda katika fukwe za bahari kuogelea pasipo uangalizi wa watu wazima.
Kamanda Aziz amesema kuwa uzoefu unaonyesha kuwa watoto wengi wamekuwa wakigongwa na magari ama kuzama na kufa maji katika siku hizi za siku kuu za mwisho wa mwaka kwa kukosa uwangalizi wa watu wazima.
Aidha amewataka wananchi kutoziacha nyumba zao wazi ama bila ya kuwa na uwangalizi wa kutosha ili kutowapa nafasi kwa wahalifu kupata fursa ya kuwaiba.