Na Is-haka Omar, Zanzibar
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” amesema atalinda na kusimamia kikamilifu mali na miradi mbali mbali inayomilikiwa na chama hicho ili iwanufaishe wananchi wote badala ya watu wachache wanaojimilikisha baadhi ya rasilimali hizo kinyume cha sheria.
Msimamo huo ameutoa wakati akikagua shamba la CCM lenye zaidi ya hekta 200 huko katika Kijiji cha Kilombero Wilaya Kaskazini “B” Unguja, alisema CCM haiwezi kufikia dhamira yake ya kuimarika kiuchumi endapo kama kuna baadhi ya watu wanaotumia rasilimali hizo kwa maslahi binafsi.
Alisema lengo la CCM kupitia mabadiliko ya muundo wa taasisi hiyo yaliyofanyika hivi karibu ni kuhakikisha rasilimali zinatumika vizuri na kwa maslahi ya wengi kwa lengo la kufikia dhamira chama hicho kujitegemea kiuchumi.
Dkt. Mabodi alisema CCM itasimamia Utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kama ilivyowahidi wananchi kwa kuhakikisha inaondosha mianya yote ya ubadhirifu wa mali za chama hicho.
Kulia ni Ni Afisa milki wa CCM Zanzibar Nd. Mwenemzi Omar Said aliyevaa fulana ya njano akionyesha ramani na mipaka ya Shamba hilo kabla ya kuanza ziara hiyo (katikati) ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” na kushoto aliyevaa kanzu na kofia ni Kaimu Mkuu wa Utawala Afisi Kuu CCM Zanzibar Nd. Mohamed Sijaamini pamoja na watendaji wa CCM Wilaya hiyo na wamiliki wa mashamba yaliyopakana na shamba hilo.
Msafara wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala "Mabodu" na baadhi ya wananchi wakiongozwa na Viongozi wa CCM Wilaya ya CCM Kaskazini “B”, wakikagua shamba hilo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala "Mabodi" akishauriana masuala mbali mbali na baadhi ya wananchi wakiwa ndani ya shamba hilo.