Na MatukiodaimaBlog
WACHIMBAJI wawili wadogo wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Masuluti kata ya Magulilwa tarafa ya Mlowa wilaya ya Iringa mkoani Iringa wamefariki dunia baada ya kukosa hewa wakiwa kazini ndani ya mgodi.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Masuluti Venjaslaus Kiunosile amesema kuwa tukio hilo limetokea leo Majira ya saa 5 asubuhi, na kwamba taarifa ya tukio hilo alipewa na mchimbaji mwenzao aliyewatembelea marehemu hao kwa ajili ya kuwasalimia.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Julius Mjengi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa miili ya marehemu hao imetolewa katika mgodi huo. Aliwataja waliofariki dunia kwa kukosa hewa kuwa ni Haus Kaijage (32) mkazi wa Bukoba na James Mlawa(22) mkazi wa Magulilwa.
Alisema chanzo cha watu hao kupoteza maisha ni kukosa hewa baada ya kuingiza jenereta la kuvuta maji mgodini kwa lengo la kuvuta maji, na baada ya kuliwasha walikosa hewa.
Alisema alisema wachimbaji hao walichukua mashine hiyo na kuiingiza ndani na mgodi baada ya awali kuharibika na kuwa jeshi la polisi linamshikilia kwa mahojiano mmiliki wa mgodi huo Samweli Msigwa.
Kamanda Mjengi alitoa wito kwa wachimbaji wadogo katika mkoa wa Iringa kuzingatia usalama katika uchimbaji wa madini.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mgama Dkt Baraka Mwifune alisema uchunguzi alioufanya unaonyesha watu hao walipoteza maisha kwa kukosa hewa.
Mmiliki wa mgodi huo Samweli Msigwa alisema kuwa akiwa njiani kuelekea eneo la mgodi kwa ajili ya kusaidia kutengeneza mashine ya kuingiza hewa katika mgodi huo ndipo alipopata taarifa ya wachimbaji hao wawili kati ya Sita kupoteza maisha kwa kukosa hewa.
Alisema mgodi huo ulikuwa na wachimbaji sita kabla ya wanne kwenda mgodi mpya wa Ismani na hivyo walibaki hao wawili na kuwa anamiliki mgodi huo kihalali na ana kibali kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Julius Mjengi kushoto akitazama shimo la mgodi katika kijiji cha Msuluti kata ya Magulilwa wilaya ya Iringa ambalo wachimbaji wawili wadogo wawili walipoteza maisha kwa kukosa hewa wakati wakichimba madini jana asubuhi
Mmiliki wa mgodi huo Samweli Msigwa (kulia) akihojiwa na polisi. Katikati ni kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Julius Mjengi
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Julius Mjengi kushoto akikagua mazingira wa mgodi huo katika kijiji cha Msuluti kata ya Magulilwa wilaya ya Iringa ambalo wachimbaji wawili wadogo wawili walipoteza maisha kwa kukosa hewa wakati wakichimba madini jana asubuhi
Wananchi wa Msuluti kata ya Magulilwa wilaya ya Iringa wakiwa wamebeba mmoja kati ya miili ya wachimbaji wadogo wawili waliokufa mgodini kwa kukosa hewa leo.