Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharikialifanya ziara ya kikazi jijini Seoul, Jamhuri ya Korea tarehe 24 Aprili 2017 kwa mwaliko kutoka kwa Mhe. Yun Byung-se, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea. Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea mwaka 1992.
Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Mhe. Yun Byung-se ambapo Waziri Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kumpatia mwaliko wa kutembelea taifa hilo hususan wakati huu inapoadhimishwa jubilee ya miaka 25. Mhe. Mahiga aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kimkakati katika uwekezaji kwa kipindi cha kuanzia 2016 -2020.
Kwa kipindi cha miaka 25, Serikali ya Korea imeisaidia Tanzania kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo Ujenzi wa Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi unaojumuisha madaraja matatu yenye jumla ya urefu wa meta 275 pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 48; Ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 600imejengwa na kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya digitali, vinavyotumia zaidi teknolojia ya Tehama zikiwemo mashine za X-ray, MRI, CT-Scan, mashine maalum kwa ajili ya kupimia magonjwa ya wanawake.
Vilevile, Ujenzi wa Hospitali ya mama na mtoto Chanika yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 160 inatarajiwa kufunguliwa siku za karibuni.Aidha, Watanzania zaidi ya 1000 wamenufaika kwa kupata ufadhili wa kusoma katika vyuo mbalimbali vya Jamhuri ya Korea.
Waziri Mahiga pia alikutana na baadhi ya Wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Korea ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania mathalani ujenzi wa Reli ya Kati katika viwango vya kimataifa; uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme; ujenzi wa maeneo ya viwanda; na huduma ya kutoa ushauri katika miradi mikubwa.
Aidha, Mhe. Waziri aliwahakikishia wawakilishi wa makampuni ya Jamhuri ya Korea kuwa, Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji na biashara pamoja na taasisi muhimu zinazotoa huduma mbalimbali katika sekta hiyo.