Mikoa mitatu ya Tanga, Morogoro na Iringa, imenufaika na kiasi cha shilingi bilioni 6.5 zilizotolewa kama mkopo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) tangu benki hiyo ianzishwe mwaka 2015.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu swali na msingi lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Felister Aloyce Bura, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza kutoa huduma kwa wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Dodoma.
Dkt. Kijaji ameeleza kuwa hadi kufikia mwezi Desemba, 2016, TADB imetoa mikopo ya jumla ya shilingi 6,489,521,120 kwa ajili ya kutekeleza miradi ishirini (20) ya kilimo katika mikoa hiyo mitatu ya Iringa, Morogoro na Tanga.
“Sambama na utoaji mikopo, Benki inatoa mafunzo kwa wakulima ambapo hadi sasa vikundi 336 vya wakulima wadogowadogo vyenye jumla ya wanachama 44,400 wamepatiwa mafunzo hayo katika mikoa hiyo mitatu” aliongeza Dkt. Kijaji
Amesema kuwa Benki hiyo inatarajia kuanza kutoa huduma hiyo kwa wakulima wadogowadogo wa Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine jirani wenye sifa.
“Benki imepata nafasi kwa ajili ya kufungua ofisi katika jengo la PSPF mjini Dodoma na itakabidhiwa ofisi hiyo mwezi Julai, 2017, baada ya mkandarasi kukamilisha ujenzi wa jengo hilo” Alisisitiza Dkt. Kijaji
Dkt. Kijaji amesema kuwa tayari Benki hiyo imemwandikia barua Katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma ili kuomba aipatie miradi mizuri ya kilimo ambayo mkoa unapendekeza Benki iifikirie katika zoezi la kutoa mikopo itakayoanza kutolewa mwishoni mwa mwaka 2017.