Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Hatimaye kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imekaa leo na kumsikiliza beki wa Simba Abdi Banda aliyesimamishwa na kamati ya saa 72 baada ya klabu ya Kagera Sugar kutuma malalamiko dhidi yake.
Kamati hiyo, imefikia maamuzi ya kumfungia mechi mbili kwa kosa la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla Aprili 2, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Adhabu hiyo inamuweka huru Banda kuweza kuendelea kucheza mechi tatu zilizosalia za timu hiyo baada ya kuwa nje kwa mechi mbili dhidi ya Mbao na Toto Africa zilizochezwa mapema wiki iliyopita.
Katika mchezo huo dhidi ya Kagera Banda alimpiga ngumi Kavila pasi na kuwa na mpira lakini mwamuzi wa mchezo huo hakumpa kadi na kupelekea adhabu yake kuwa nyepesi kulingana na ushahidi alioupeleka katika kamati hiyo.
Kamati iliweza kubaini kuwa Banda hakupewa adhabu yoyote na refa kwa sababu hakuona tukio hilo, alifanya kitendo cha aina hiyo kwenye mechi namba 169 kati ya Simba na Yanga iliyofanyika Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam akimpiga kiungo Said Juma ‘Makapu’.
Awali, Klabu ya Kagera Sugar iliwasilisha malalamiko dhidi ya kitendo cha beki wa Simba, Abdi Banda kumpiga ngumi kiungo wao George Kavilla wakati akiwa hana mpira, na Mwamuzi wa mechi hiyo kutochukua hatua yoyote.