WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Viettel ya Vietnam inatekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano vijijini ambao umefanikisha kuweka miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye shule 417 hapa nchini.
Amesema mradi huo ambao unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2015-2017, umewezesha pia ofisi za Halmashauri za Wilaya 123, Hospitali za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya 131 na Ofisi za Posta 68 kufikiwa na mtandao huo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 6, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2016/2017 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake ukiwemo Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018
Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2016/2017, baadhi ya kazi zilizofanyika kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano; Mradi wa Anuani za Makazi na Postikodi; na kuanzisha huduma ya kituo cha Jamii Centre kitakachorahisisha utoaji wa huduma muhimu katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni, ankara na huduma za kibenki.
“Sekta ya mawasiliano inatekeleza Programu ya Miundombinu ya Kikanda ambayo inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school), Mradi wa Video Conference ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na ufungaji wa vifaa vya TEHAMA katika mikoa 26 na taasisi za Serikali,” amesema.