Na Bashir Yakub.
Ni wangapi wamefanyiwa utapeli katika harakati za kununua viwanja au nyumba. Ni wangapi wamepata hasara kubwa kutokana na michezo ya utapeli iliyotamalaki katika ardhi nchini. Ni kesi ngapi ziko mahakamani zinazohusisha utapeli katika mauzo na manunuzi ya ardhi. Idadi ni kubwa mno na huu ndio ukweli.
Siku zote huwa tunasema ni vigumu kujua ukubwa na hatari ya jambo hili mpaka likukute au limkute mtu wako wa karibu. Lakini swali ni ikiwa watu wamekuwa wakijifunza kupitia wenzao ambao wamekutwa na haya. Kama na wewe bado hujajifunza basi ni muhimu sasa kujifunza.
Mtu anauza ardhi moja kwa watu hata zaidi ya wanne tofauti, mtu anauza ardhi asiyokuwa yake huku akijua kabisa sio ya kwake, mtu anaghushi hati au leseni ya makazi kisha anauza kiwanja au nyumba ya mtu, kiongozi wa serikali ya mtaa anashiriki kuuza ardhi ya mtu huku akijua kuwa juzi mtu mwingine alinunua ardhi hiyohiyo, kwa ufupi hali ni mbaya na ni vema kusema ili watu wachukue tahadhari.
Wizara ya ardhi imeshasema mara nyingi kuwa moja ya sababu kubwa inayopelekea watu kutapeliwa katika manunuzi ya ardhi ni wanunuzi wenyewe kutozingatia taratibu za kisheria za manunuzi. Migogoro mingi imezalika hapa.
Mara kadhaa tumewahi kueleza kwenye makala mbalimbali namna salama ya kununua ardhi kwa kuepuka utapeli. Zipo makala nyingi ambazo zimeeleza hatua za kufuata ili uwe salama. Hata hivyo leo kitaelezwa kitu kingine ambacho hakikuwahi kuelezwa. Ni namna ya kuhakiki hati au leseni ya makazi ili kujua ikiwa ni halisi (original) au feki kabla ya kununua kiwanja au nyumba.
1.UHAKIKI ULIOWAHI KUSHAURIWA.
Kabla ya kueleza njia nyingine ya uhakiki inayotakiwa kuelezwa leo hebu tujikumbushe njia iliyowahi kuelezwa katika makala zilizopita. Ni uhakiki wa hati kwa njia ya upekuzi rasmi( official search). Tulisema kuwa kupitia njia hii utaandaa maombi kwenda kwa msajili wa hati(Registrar of Title) ukitaka kujua ikiwa nyumba /kiwaja unachotaka kununua kama kina mgogoro au ikiwa kuna mtu mwingine mwenye maslahi juu yake.
Mgogoro ni kama kuna zuio la kifamilia( caveat), zuio kutoka mahakamani na mengine yanayofanana na hayo. Na kuwapo mtu mwingine mwenye maslahi ni kama kiwanja au nyumba hiyo kuwa imesimama kama dhamana ya mkopo n.k. Majibu ya vitu vyote hivi utayapata utakapojibiwa maombi yako ya upekuzi rasmi ( official search).