NA ESTOM SANGA-TASAF
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wametembelea kijiji cha Mlanda wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa kukagua shughuli zinazotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini-PSSN.
Wakiwa kijijini hapo wajumbe wa kamati hiyo wameonyesha kuridhishwa kwao na namna Mpango huo ulivyohamasisha wananchi kuboresha maisha yao ikiwemo ujenzi wa nyumba za mabati,kusomesha watoto,kuanzisha miradi midogo midogo ya kuichumi na kuboresha afya za familia za kaya hizo.
Akizungumza na walengwa wa Mpango huo na viongozi, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Venance Mwamoto, ametaka serikali wilayani humo kuhakikisha kuwa wataalamu wa ugani wanawatembelea walengwa wa Mpango huo kuwapa ushauri wa namna bora ya kuendesha miradi wanayoianzisha.
‘’Tusiiachie TASAF kwani nyie ndiyo mko karibu na walengwa hao,ili waweze kufanikiwa zaidi wanahitaji hamasa na utaalamu wenu’’ alisisitiza Mhe. Mwamoto.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakionyeshwa mabati aliyoyanunua mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Mlanda ,Iringa Vijijini ,Bi. Konjeta Lyambafu aliyevaa kitambaa kichwani. Kushoto kwake Mwenyekiti wa kamati hiyo Venance Mwamoto akimkabidhi fedha zilizochangwa na wajumbe kuongeza uwezo wa mlengwa huyo kukamilisha mabati ili aezeke nyumba yake iliyoko nyuma yao kwa bati.
‘’Ninaishukuru serikali kupitia TASAF kwa kuniwezesha kuboresha maisha kwa kujenga nyumba ya bati na kumudu kuwatunza na kuwasomesha wajukuu zangu wanane ’’ ndivyo mmoja wa walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya masikini Bi. Claudia Kanyita mkazi wa kijiji cha Mlanda, wilaya ya Iringa Vijijini anavyoelekea kuwaeleza wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki .
Mmoja wa walengwa wa TASAF katika kijiji cha Mlanda wilaya ya Iringa Vijijini Claudia Kanyita akiwa na wajukuu zake watatu alioachiwa baada ya watoto wake kufariki, akitoa maelezo kwa kamati ya kudumu ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyotembelea kijiji hicho kuona utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na TASAF. Nyumba inayoonekana nyuma yao imejengwa na Mlengwa huyo kwa ruzuku ya TASAF.Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Ladislaus Mwamanga.
‘’Mgeni njoo mwenyeji apone ’’ndivyo ilivyo kwa mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini wa kijiji cha Mlanda wilaya ya Iringa vijijini Konjeta Lyambafu aliyechangiwa fedha na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ili aweze kuongezea fedha anazozipata kupitia ruzuku inayotolewa na TASAF kuanzisha mradi wa kujiongezea kipata. Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Venance Mwamoto akimkabidhi fedha hizo mlengwa, kulia kwao ni Waziri Angellah Kairuki . Nyumba iliyoko nyuma yao imeezekwa na mlengwa huyo kwa bati alizozinunua kupitia ruzuku kutoka TASAF na hivyo kuboresha makazi yake.