Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameipa miezi miwili Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), kuhakikisha kuwa inapata Dola za Kimarekani milioni 50 ili kuongeza pato kwa Kampuni na Taifa kwa ujumla kupitia Mkongo wa Taifa.
Akitoa agizo hilo leo, wilayani Bukoba mkoani Kagera, Waziri Prof. Mbarawa amesema agizo hilo limetokana na Serikali kuongeza masafa kwa kampuni hiyo kutoka 10 hadi 200 (MHZ) ambayo yana uwezo wa kuunganisha wateja wengi na wakubwa zaidi.
Amesisitiza makampuni ya Simu nchini kuchangamkia fursa ili kupata masafa yenye uwezo mkubwa kupitia mkongo huo.
“Hakikisheni mnajipanga kuipata hiyo fedha ndani ya miezi miwili na kuwapatia masafa ya kutosha wateja mlionao ndani na nje ya nchi na kujitahidi kuongeza wateja wengi zaidi”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, ameitaka TTCL kusogeza wigo wa kuwasiliana na wateja wakubwa ili kuwashawishi kununua masafa hayo kulingana na mahitaji yao na hivyo kutanua wigo wa kibiashara na kuiwezesha kampuni hiyo kupata faida zaidi.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), akioneshwa taarifa ya mapato na Meneja wa Kampuni ya Simu Nchini (TTCL), mkoa wa Kagera, Bw. Salum Mbaya, wakati alipotembelea ofisini hapo leo.

Fundi Mitambo kutoka Kampuni ya Simu Nchini (TTCL), Eng. Godfrey Mbise, akimpa maelezo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), kuhusu mfumo wa utoaji huduma katika mkongo wa taifa mkoani humo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa uongozi wa Kampuni ya Simu Nchini (TTCL), mkoa wa Kagera, leo, mara baada ya kukagua mitambo na mifumo iliyopo ofisini hapo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akishuka katika ndege ya Kampuni ya Ndege Nchini (ATCL), katika uwanja wa ndege wa Bukoba, mkoani Kagera alipowasili kwa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo.