Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amesema raia wa Kenya na Uganda wataendelea kuajiriwa katika hoteli zetu kama Watanzania hawataweza kubadilika kwa kuachana na tabia sizizofaa ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na watalii wengi wanaofikia katika hoteli hizo.
Amesema baadhi ya wafanyakazi katika hoteli hizo wamekuwa na tabia za udokozi, uvivu na kiburi akitolea mfano amesema unaweza ukafika katika hoteli ukakaa zaidi ya nusu saa bila kusikilizwa huku wahudumu wakikupita tu kana kwamba hawajakuona, hali inayochangia kwa watalii wanaotembelea vivutio vya utalii kwa mara ya kwanza kutokurudi tena.
Sendeka aliyasema hayo wakati akifunga mafunzo yaliyofanyika kwa muda siku tatu mkoani Njombe kwa wahitimu 90 katika fani ya ukarimu na Utalii, alisema ni lazima wabadilike kwa kufanya kazi kwa kujituma pasipo kusimamiwa na mameneja wa hoteli hizo la sivyo wataendelea kulalamika huku nafasi zao zikiendelea kuchukuliwa na wageni.
Amesema wamiliki wengi wa hoteli wamekuwa wakipenda kuajiri wafanyakazi kutoka nchi hizo kutokana na uchapakazi wao na si kwa ajili ya wanajua lugha ya kiingereza ‘’Wamiliki wananchohitaji ni kupata faida na sio kung’ang’ania kuajiri wazawa ambao hata kumkaribisha mgeni kwa bashasha imekuwa ni shida’’ alisisitiza Sendeka
Kwa upande wa Mratibu Msaidizi wa Mradi wa SPANEST, Edmund Murashani alisema mradi huo umeamua kujikita katika kuwezesha wahudumu wa hoteli, migahawa na nyumba za kulala wageni wanapata mafunzo kwa kuwa wao ni mojawapo ya nguzo muhimu katika kuhakikisha utalii unakua katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
‘’ Tunataka mtalii akifika katika hoteli hizo kitu cha kwanza kabla hajatembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana katika ukanda huo awaze kuongeza siku za kulala katika hoteli zetu kutokana na huduma stahiki anazopata kutoka kwa wahudumu hao’’ Murashani alisema Naye, Mhitimu wa Mafunzo hayo, Tulizo Sanga aliomba siku za mafunzo hayo ziweze kuongezwa kwani siku tatu hazitoshi kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo kwao.
Mafunzo kama hayo yanatarajiwa kufanyika mkoani Iringa na Songwe chini ya Usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia Mradi wa SPANEST unaotekelezwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka akizungumza na jumla ya wahitimu 90 wakati alipokuwa akifunga jana mafunzo katika fani ya Utalii na Ukarimu yaliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na Mradi wa SPANEST yaliyofanyika Mkoani Njombe kwa muda wa siku tatu. na Wengine ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Njombe, Joseph Choya (kulia) Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya Utalii, Paskasi Mwiru (kushoto).
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka akikabidhi cheti kwa Mhitimu wa mafunzo katika fani ya ukarimu na utalii wakati alipokuwa akifunga mafunzo hayo jana yaliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na Mradi wa SPANEST yaliyofanyika Mkoani Njombe.
Mkufunzi kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Dawson Kyungai akiwaelekeza Washiriki 90 wa Mafunzo ya Ukarimu na Utalii namna ya kumimina mvinyo kwenye glasi pamoja na kuwaonyesha kiwango kinachotakiwa. Mafunzo hayo yametolewa kwa muda wa siku tatu katika fani ya mapokezi, utoaji huduma ya chakula na vinywaji pamoja na upishi yaliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Mradi wa SPANEST ambayo yamefungwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka .
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na Maofisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Mradi wa SPANEST na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mara baada ya kufunga mafunzo ya muda wa siku tatu kwa jumla ya wahitimu 90 katika fani ya Utalii na Ukarimu yaliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na Mradi wa SPANEST. (Picha na Lusungu Helela- WMU).