NaFrank Shija – MAELEZO, Dar es Salaam.
WAFANYABIASHARA ndogondogo katika Soko la Machinga Complex Jijini Dar es Salaam wameshauriwa kubadilika na kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria badala ya kufanya biashara zao kimazoea.
Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene alipofanyaa ziara ya kikazi katika Soko hilo ili kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara wa soko hilo.
“Nawapa pole sana ndugu zangu wafanyabiashara wa Machinga Complex mnaendesha biashara zenu bila kuzingatia sheria jambo linalo wagharimu hivi sasa katika biashara zenu leo nimekuja kuwarejesha kwenye mstari,” alisema Simbachawene.
Aidha Waziri Simbachawene amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kuwachukulia hatua baadhi ya viongozi wa menejimenti ya Machinga Complex kwa kile kinachodaiwa utendaji wao mbovu na kujaza nadfasi zote zilizo wazi.
Wakati huohuo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuteua Wajumbe wa Bodi ya Machinga Complex ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa Soko hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene (wapili kutoka kushoto) akitembelea baadhi ya vizimba vya wafanyabiasha katika soko la wafanyabiashara wadogowadogo la Machinga Complex leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, Meneja wa Soko hilo, na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Theresia Mmbando.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Machinga Complex alipofanya ziara kwa ajili ya kusikiliza changamoto zao leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Sipora Liana, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Theresia Mmbando, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema.
Mmoja wa wafanyabiashara katika Soko la Machinga Complex akielezea changamoto wanazokumbana nazo katika soko hilo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene (hayupo pichani) alipotembelea katika soko hilo leo Jijini Dar es Salaam. Waziri Simbachawene amefanya ziara katika Soko hilo hili kusikiliza changamoto kutoka kwa wafanyabiashara hao na kukagua utekelezaji wa agizo alilolitao wakati wa ziara yake ya kwanza sokoni hapo.