Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MHANDISI wa maji katika halmashauri ya Mji wa Kibaha,Grace Lyimo,amewataka wakazi wa mji huo kulinda na kuitunza miundombinu na mifumo ya miradi mbalimbali ya maji safi kwani maji ni uhai kwa afya na maisha yao.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakiharibu miundombinu hiyo kwa kuikata ama kupasua kwa makusudi hali inayosababisha uchafuzi wa mazingira ikiwemo matope na kusababisha hasara .
Akizungumza wakati akiwa kutembelea miradi mbalimbali ya maji Grace alisema ,miradi mingi inatumia fedha nyingi kutoka bank ya dunia na mengine serikali kuu hivyo kila mmoja athamini miradi hiyo.
Alieleza kwamba ujumbe wa maadhimisho ya wiki ya 29 ya maji 2017 unaenda sambamba na shughuli zitakazofanywa mjini hapo. Hata hivyo mhandisi huyo wa maji alisema,walianza kutembelea kituo cha maji cha jumuiya ya maji Zojosa ,kituo ambacho kinalisha maji mitaa mitatu ya Zogowale,Jonung’ha na Saeni na kupanda miti 50.
"Tutakagua pia miradi mbalimbali na viwanda ikiwemo kiwanda cha ngozi na kiwanda cha viuadudu vya kuzuia mazalia ya mbu ambapo march 22 tutaadhimisha wiki ya maji kwenye mradi wa maji Saeni huko Viziwaziwa " alibainisha Grace.
Nae katibu wa kituo cha jumuiya ya maji ZOJOSA, Said Kondo alisema,mradi huo umefadhiliwa na bank ya dunia kwa gharama ya mil .109. Alielezea watumiaji maji hadi sasa ni 2,500 kwa siku wanalisha lita 50,000 na kupampu maji masaa sita.
Kondo alisema walianza na vituo 8 sasa vipo 56 na malengo yao ni kufikia wanachi kwa asilimia 80 na zaidi ya hapo . "Tunachangamoto ya wateja wetu kutolipa bili kwa wakati lakini tuna zaidi ya mil.3.4 bank kwa sasa " alisema Kondo .
Mgeni rasmi ambae ni mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Kibaha,Leonard Mloe aliomba mradi huo utunzwe na kusimamia makusanyo.
Uzinduzii wa wiki ya maji duniani umeanza march 16 na kilele chake kitakuwa march 22 .