MKUU wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu (mwenye miwani) amefanikiwa kutatua mgogoro wa ardhi wa mipaka uliodumu kwa takribani miaka 33 sasa kati ya wananchi,kituo cha kufundishia wanyama kazi(OTC) na kituo cha utafiti wa mifugo(Veterinary)vilivyopo katika kijiji cha Muungano wilayani humo.
Machi 4 mwaka huu Mtaturu alifanya kikao cha awali na familia zipatazo 21 ambazo zilieleza kutoridhishwa na kitendo cha kituo kumiliki hekari 320 ambapo mipaka yake iliongezwa bila ya kuwashirikisha hali iliyomlazimu kuamua kutembelea eneo husika ili kuona namna ya kutatua mgogoro huo.
Baada ya saa nne za mjadala akiwa eneo la tukio alibaini uwepo wa mipaka iliyosogezwa kwenye maeneo ya wananchi bila ya kuwashirikisha ikiwemo kuingilia makaburi na hivyo kushauri wananchi kurejeshewa hekari 100 kutoka kituo cha OTC na eneo la mita za mraba 3,093 kutoka kituo cha Veterinary..
“Ili mgogoro huu umalizike inabidi tufanye maridhiano na katika maridhiano kuna utaratibu hufanyika wa nipe nikupe yaani give and take na katika maeneo ambayo wananchi wameingia kwenye mpango mji ufidiwaji utazingatiwa kwa mujibu wa sheria namba 4 ya mwaka 1999,”alisema Mtaturu.
Baada ya maridhiano hayo wataalam wa ardhi waliweka alama kwa kupima upya kwa GPS mbele ya wananchi ambapo aliwashukuru wazee,viongozi na wananchi kwa ushirikiano uliosaidia kufikia maridhiano na kumaliza mgogoro huku akitoa agizo kwa halmashauri kupitia idara ya ardhi na kilimo kuweka alama za kudumu kwenye mipaka zitakazosaidia kuondoa migogoro isiyo ya lazima.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Muungano Hussein Galawa kwa niaba ya wananchi alimshukuru mkuu huyo kwa kukubali kusaidia kutatua mgogoro huo wa muda mrefu na kumuomba kwenda kutatua mgogoro wa mipaka kati ya shule yao ya msingi na sekondari Unyahati na wananchi na kusisitiza wananchi kuwa watulivu badala ya kutuhumiana na kuchafua viongozi pindi inapotokea migogoro.
Wakizungumzia historia ya kituo cha OTC mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho mzee Emmanuel Humme,mwenyekiti wa zamani wa kamati ya uendeshaji kituo cha OTC mzee Juma Mwati na mzee Andrea Chima walisema kituo hicho kilianzishwa mwaka 1970 kikiwa na lengo la kufundisha wakulima na wafugaji ili kuleta tija na kilitumiwa kama kituo cha kugawa pembejeo mbalimbali za kilimo.