Bw. Alvaro Rodriguez ambaye ni Mwakilishi Mkazi wa Mashirika matatu ya Umoja wa Maifa nchini Tanzania (IOM, UNICEF na UNDP) akiongea na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu mara baada ya kuwasili ofisini kwake.
Na: Sylvester Raphael
Umoja wa Mataifa kupitia Mkurugenzi wake Mkazi nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez umetembelea, kukagua na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na umoja huo Mkoani Kagera ambapo zaidi ya Dola za Kimarekani (618,000 USD) zimetolewa ili kufadhili na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama Elimu na Afya pia na miradi ya kijamii.
Bw. Alvaro Rodriguez ambaye ni Mwakilishi Mkazi wa Mashirika matatu ya Umoja wa Maifa nchini Tanzania (IOM, UNICEF na UNDP) aliwasili Mkoani Kagera Machi 13, 2017 na ujumbe wake ili kutembelea na kukagua miradi ya Maendeleo na Kijamii inayofadhiliwa na Umoja huo katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Miradi aliyoitembelea Bw. Rodriguez ni pamoja na mradi wa ujenzi wa vyoo, madarasa, mabweni na jengo la utawala katika shule ya Msingi Mgeza Mseto Manispaa ya Bukoba ambapo mara baada ya kukamilika mradi utagharimu Dola za Kimarekani (318,000 USD) ambapo ujenzi wa vyoo umekamilika, madarasa mabweni na jengo la Utawala ujenzi upo katika hatua ya msingi.
Bw. Rodriguez akiongea na wanafunzi, walimu na wananchi waliofika kumpokea katika shule hiyo alisema kuwa amefurahishwa kufika katika shule hiyo na kujionea hali halisi ya watoto wenye ulemavu wa albinizimu na walemavu wengine aidha, alisema kuwa Umoja wa Mataifa uliamua kutoa fedha hizo ili kurejesha miundombinu ya shule hiyo baada ya kuharibiwa na Tetemeko la Ardhi lilitokea Septemba 10, 2016.
“Nilipokuwa Dar es Salaam niliambiwa na Waziri Profesa Joyce Ndalichako kuwa nikifika Kagera nitembelee Shule ya Msingi Mugeza Mseto pia nilipofika Kagera Mkuu wa Mkoa ameniambia nitembelee shule hii sasa nimejionea na kujua ni kwanini walinisistiza, shule inahitaji msaada mkubwa. Aidha, Umoja wa Mataifa unapenda kusaidia lakini Tanzania shule za namna hii zipo nyingi na ndiyo maana tunasaidia kidogo kidogo ili kuongeza mahitaji muhimu.” Alisistiza Bw. Rodriguez.