Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
Na Hassan Silayo-MAELEZO
Kuanzia 02 Machi, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alianza ziara ya kikazi ya siku 4 katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara iliyolenga kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Ziara hiyo kwa kiasi kikubwa imeonesha dira na mwelekeo wa serikali ya awamu ya tano hasa katika utekelezaji wa miradi inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo bila kujali Imani,kabila na itikadi za vyama vyao vya siasa.
Siku ya kwanza ya ziara yake Rais Dkt. Magufuli aliweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Tanzania Goodwill Ceramic Tiles Ltd. kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani ambacho ni kikubwa Afrika Mashariki na Kati kilichogharimu Dola za Marekani Milioni 50 kwa awamu ya kwanza.
Akiongea katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika kiwanda chenye uwezo wa kuzalisha mita za mraba 80,000 za vigae kwa siku Rais Magufuli alifurahishwa na teknolojia ya kuyeyusha mchanga wa kutengenezea vigae inayotumiwa na kiwanda hicho na kuhoji kama kuna haja ya serikali kuendelea kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi.
Rais Magufuli alisema kuwa “Nchi hii tumechezewa vya kutosha, sasa nyinyi hapa mnayeyusha mchanga kwa kuuchemsha hadi nyuzi joto 1,000 wakati wengine wanasafirisha mchanga nje ya nchi wakati uchemshaji wake hauhitaji kufika hata nyuzi joto 1,000, naiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Wizara ya Nishati na Madini kuwa kuanzia sasa ni marufuku kusafirisha mchanga nje ya nchi".