Na: Lilian Lundo – MAELEZO.
Operesheni ya kuondoa pombe kali zilizofungwa katika vifungashio vya plastiki (viroba) inayoendelea nchi nzima imeibua wafanyabiashara wanaofanya biashara ya pombe bila kuwa na vibali vya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Hayo yamebainishwa na Afisa Afya na Mratibu wa Masuala ya Chakula wa Manispaa ya Temeke Rehema Sadick, leo Jijini Dar es Salaam wakati wa operesheni hiyo inayoendelea nchini.
“Katika operesheni hii ya kuondoa pombe za viroba tumegundua wafanyabiashara wengi wanaojihusisha na uuzaji wa pombe kutokuwa na kibali cha TFDA ambacho hutolewa katika Halmashauri husika,” alifafanua Rehema Sadick.
Aidha amebainisha kuwa katika msako uliofanyika leo Kigamboni, ambapo wamekagua zaidi ya maduka matano yanayouza pombe kwa jumla, ni duka moja tu la Mangale Store lililoko Tuangoma ndilo lililokutwa na kibali cha TFDA.