Na Greyson Mwase, Njombe
Kaya 1600 katika vijiji kumi mkoani Njombe zinatarajiwa kupata umeme wa uhakika mara baada ya kukamilika kwa mradi wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia maporomoko ya maji wa Luponde Hydro Ltd unaotekelelezwa na kampuni ya Rift Valley Energy.
Hayo yalielezwa leo na Meneja Mradi wa Luponde Hydro, Mugombe Maxwell katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika mkoa wa Njombe ili kujionea maendeleo ya miradi midogo ya umeme wa maporomoko ya maji na nishati jadidifu inayotekelezwa katika mkoa huo.
Maxwell alisema kuwa kampuni ya Rift Valley Energy ina miradi miwili ambayo ni Mwenga Hydro Grid wenye uwezo wa Megawati 4.1na Luponde Hydro Ltd utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 3 mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wake hivyo kuwezesha vijiji kumi katika mkoa huo kupata umeme wa uhakika ifikapo mwakani.
Akielezea mradi huo wa Luponde Hydro Ltd, Maxwell alisema kuwa mradi ulianza mwaka 2016 na kuongeza kuwa mradi huo upo katika maeneo mawili ambayo ni Luhololo na Igola yote yakiwa mkoani Njombe.
Akielezea ujenzi wa mradi huo, Maxwell alieleza kuwa mradi umegawanyika katika awamu mbili na kuendelea kusema kuwa awamu ya kwanza inahusisha usambazaji wa umeme wa uhakika katika vijiji saba vyenye kaya 1120, shule tisa na vituo vya afya vitano.

Mtaalam kutoka Sehemu ya Nishati Jadidifu, Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Stephan Kashushura (kulia) akibadilishana mawazo na Sister Richardis Chiwinga katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu katika mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Benedict Sisters of Saint Agnes Chipole, Mbinga mkoani Ruvuma.

Sister Richardis Chiwinga kutoka katika mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Benedict Sisters of Saint Agnes Chipole (katikati) akielezea hali ya maji katika bwawa la mradi huo kwa wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

Sehemu ya bwala la maji katika mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Benedict Sisters of Saint Agnes Chipole, Mbinga mkoani Ruvuma.

Sister Richardis Chiwinga kutoka katika mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Benedict Sisters of Saint Agnes Chipole (kushoto) akiongoza watalam kutoka Idara ya Nishati Jadidifu, Wizara ya Nishati Jadidifu katika ziara kwenye eneo la mradi.