Jovina Bujulu- MAELEZO.
Kila mwaka ifikapo Machi 8 kila mwaka, wanawake duniani kote huadhimisha siku yao ambapo hujitathmini kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo walizofanya, changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo.
Akiongea hivi karibuni katika kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, Katibu mkuu wa Wizara ya Afya na Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi Sihaba Nkinga alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Tanzania ya Viwanda; Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko”
Kauli mbiu hii inasisitiza kuwajengea wanawake uwezo wa kitaaluma, kibiashara, upatikanaji wa mitaji, masoko na biashara ili waweze kushiriki kwa usawa, na kunufaika na fursa zilizopo badala ya kuwa wasindikizaji.
“Ujumbe wa kauli mbiu hii umezingatia sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000 na ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu hususani lengo namba 5 kuhusu usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi” alisema Bi Nkinga.
Kauli mbiu ya mwaka huu imetotolewa kutokana na kauli mbiu ya Umoja wa Mataifa (UN) isemayo “Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi katika Dunia ya Mabadiliko ya Kazi”.