Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) wamesaini makubaliano ya mafunzo yatakayowaongezea uwezo na namna bora ya ukusanyaji mapato (kodi) ili kuweza kufikia malengo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa kutiliana saini makubaliano hayo, Kamishna wa TRA Tanzania, Alphayo Kidata amesema kuwa mafunzo hayo yatakayokuwa na kozi 64 yataendeshwa na chuo cha Kodi Tanzania (ITA) kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa katika kozi hizo, ambazo zinatarajiwa kuchukua miezi mitatu (Machi hadi Juni), mwaka huu, watumishi wote wa ZRB wanatarajiwa kupewa mafunzo hayo ambapo mpaka sasa kozi ya kwanza imeishaanza kufundishwa chuoni hapo.
“Tangu serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani imekuwa ikiweka mikakakti ya kukusanya kodi kwa wingi ili kuinua uchumi na kuifanya miundombinu ya nchi kuwa mizuri kwa hiyo tunaimani mafunzo hayo yatatuwezesha kufikia malengo” alisema Kidata.
Naye Kamishna wa Mapato Zanzibar, alisema wanatarajia mafunzo hayo yataiwezesha Zanzibar kupata matokeo mazuri katika ukusanyaji wa kodi Zanzibar na pia kuwajengea uwezo mzuri watendaji wake yatakayoleta mabadiliko katika kukuza uchumi.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata akizungumza na waandishi wa wakati wa kutiliana saini ya makubaliano ya pamoja ya mafunzo juu ya namna ya kuongeza uwezo wa ukusanyaji wa kodi baina ya TRA na ZRB jijini Dar es Salaam leo.
Kamishna wa bodi ya mapato Zanzibar Bw. Amour Bakari akizungumzia mafanikio wanayotarajiwa kuyapata baada ya kusaini makubaliano ya mafunzo juu ya namna ya kuongeza uwezo wa ukusanyaji kodi kwa watumishi wote wa Zanzibar katikati ni Kamishna Mkuu wa TRA Tanzania na kushoto ni mkuu wa chuo cha Kodi (ITA), Prof. Isaya Jairo leo kwenye ukumbi wa Makao makuu ya TRA jijini Dar.