Na Zawadi Msalla-MAELEZO Dodoma
Vyombo vya Habari nchini vimeaswa kutumia uhuru wake vizuri bila kusababisha madhara ndani ya nchi kama ilivyotokea katika baadhi ya nchi za Afrika.
Akichangia hotuba ya wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mhe.Jaddy Simayi Jaddy mbunge wa Mkwajuni alisema baadhi ya vyombo vya habari vilivyopo hapa nchini vinaweza kuchangia machafuko ndani ya nchi kwani mwelekeo wa mambo yanayoandikwa yana dalili ya uchochezi.
Alisisitiza kuwa hata kama wananchi wanavihitaji vyombo vya habari lakini vikiachiwa vifanye vinavyotaka vitaipeleka nchi pabaya. “Ni kweli tunavihitaji sana vyombo hivyo ila kwa sasa inabidi viangaliwe kwa umakini sana” Alisema mchangiaji.
Aliiomba Serikali iwasilishe sheria ya vyombo vya habari kama ilivyo ahidi ili kuweza kudhibiti baadhi ya mambo yasiyo sahihi yanayoonekana kwa sasa kwenye vyombo vya habari.
Akielezea uwezo wa vyombo vya habari alisema vyombo hivyo vina nguvu kubwa katika kujenga nchi na kuleta maendeleo ya nchi yeyote ile duniani.
Naye Mbunge wa Bunda Mh. Stephen Wasira akichangia hoja hiyo alisema uhuru lazima uwe na mipaka . Kama hakuna nidhamu ya vyombo vya habari uwepo wa demokrasia inapotea.
Alisema Tanzania ni kati ya nchi inayojali uhuru wa vyombo vya habari kwani mpaka sasa ni nchi pekee Afrika Mashariki iliyo na vyombo vingi vya habari. Takwimu zinaonesha mpaka sasa kuna jumla ya magazeti na majarida 781, magazeti yanayotoka kila siku 13 na magazeti na majarida yanayotoka kwa wiki 62 na kuongeza kuwa hiyo ni moja ya mafanikio makubwa ya kutekeleza uhuru wa Vyombo vya Habari nchini.
Hata hivyo aliwaomba waandishi wa habari waache kuandika habari zisizo na ukweli ndani yake kwani wanao athirika na hilo ni wengi. Alisema uandishi wa habari ni taaluma hivyo wanaoitumikia taaluma hiyo inawapasa kufanya kazi kwa weledi na kufuata kanuni na taratibu za taaluma hiyo.
Akichangia hoja ya vijana alisema vijana ni Taifa la leo. Iwapo Serikali itatoa kipaumbele kwa vijana ajira itapatikana. Hata hivyo aliisifu Serikali kwa jitihada inazochukua za kusaidia vijana katika mikopo inayo wanyanyua, mpango mkakati wa maendeleo ya vijana ni moja ya njia ya kuinua vijana nchini.