Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Pili wa Zanzibar Mheshimiwa Aboud Jumbe Mwinyi na Makamu Mwenyekiti wa Kwanza wa CCM kilichotokea leo jijini Dar es Salaam.
Rais Mstaafu amemuelezea Mzee Aboud Jumbe kama kiongozi mwenye mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa Zanzibar na mwenye mchango mkubwa katika uhai wa Muungano wetu. Amesema, “Historia ya Chama cha Mapinduzi na ile ya Muungano wetu haziwezi kukamilika bila kumtaja Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi”.
Rais Mstaafu amewatumia salamu za rambirambi Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa msiba huu mkubwa katika taifa letu. Amesema:
“Naungana nanyi na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuomboleza msiba huu mkubwa kwa Taifa letu. Mwenyezi Mungu na awape familia ya Marehemu moyo wa subra na uvumilivu. Inna Lillahi Wainna Ilaihi Rajuun.”
Imetolewa na:
Ofisi ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne
Dar es Salaam, 14 Agosti, 2016