WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali ina kazi kubwa ya kushughulika na kundi dogo linalojihusisha na lugha za uchochezi wa kidini ambao unachangia kudhoofisha amani ya nchi.
“Tunajua nia yao ni kufanya nchi isitawalike lakini sisi tumesema hatukubali. Tumekubaliana na Waziri wa Mambo ya Ndani, ulinzi uimarishwe kila mahali, mshingae kuona watu wanawahoji lakini nia njema, ya kurudisha amani yetu,” alisema Waziri Mkuu.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Mei 10, 2013) wakati akiwasilisha salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali wakati wa ibada ya mazishi ya waumini watatu wa Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, jijini Arusha waliofariki dunia kutokana na mlipuko wa mabomu uliotokea Jumapili iliyopita, Mei 5, mwaka huu kanisani hapo.
Waziri Mkuu amewaomba wanachi kutoka ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia kwenye upelelezi wa tukio hilo.