Kamanda wa polisi mkoa wa Kipolisi wa kinondoni Charles Kenyela (pichani) anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika pambano la kutetea ubingwa Afrika mashariki na kati kati ya bondia Mtanzania Thomas Mashali na Bernad Mackoliech wa Kenya Jumamosi katika Ukumbi wa Friends Corner Manzese jijini Dar es salaam.
Mratibu wa pambano hilo Aisha Mbegu amesema wameamua kumualika kamanda Kenyela ili kuhakikisha wanatumia nafasi hiyo kutoa Elimu ya Ulinzi shirikishi na kwa kutambua mchango wa jeshi la polisi kudumisha amani katika michezo.
“ Jeshi la polisi ni wadau wetu wakubwa katika michezo hasa ngumi na mchango wao umekuwa ukionekana kwani sasa hakuna vurugu zinazojitokeza katika mapambano yeyote ya ngumi yanayofanyika tofauti na Miaka ya Nyuma ambapo Ngumi ilikuwa Watoto hawawezi kwenda kuangalia,”alisema Aisha.
Aisha alisema katika pambano la awali ambalo lilifanyika katika Ukumbi wa Friend corner hakukuwa na vurugu na idadi ya watoto na wanawake kuangalia ngumi imekuwa ikiongezeka siku hadi siku na nhivyo kutoa hamasa kwa wazazi na watoto kupenda mchezo huo.
Mbali na Kenyela Mbunge wa Kinondoni Iddi Azan na Mbunge wa ubungo John Mnyika wamealikwa ili kushuhudia vipaji vya vijana wa kinondoni katika Ngumi.
Bondia Mackoliech anatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari leo (Alhamisi) katika Uwanja wa Karume na Ijumaa wanatarajiwa kupima Uzito saa Nne asubuhi katika Ukumbi wa Friends Corner Manzese .