Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe katikati ya wiki hii aliongoza ujumbe wa Tanzania nchini Zambia katika kikao cha 58 cha Baraza la Mawaziri wanaosimamia uendeshaji wa Reli ya Tazara. Kikao hiki cha siku mbili kiliwajumuisha Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Mhe. Saada Salum (Fedha) na Mhe. Dkt. Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara) na Mawaziri wa sekta husika kutoka Zambia. Aidha, kikao hiki kilitanguliwa na kikao cha Bodi ya TAZARA. Ujumbe wa Tanzania ukiwa nchini humo uliweza kumtembelea Rais wa kwanza wa Zambia Mhe. Kenneth Kaunda katika ofisi zake ambapo katika kikao cha pamoja na Rais huyo, Mhe. Kaunda alisisitiza mshikamano na upendo miongoni mwa waafrika na kuwahimiza ‘vijana’ viongozi waliopewa jukumu la kusimamia TAZARA kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza ufanisi wa RELI hii ili iendelea kuwasaidia wananchi wa nchi zote mbili.
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Dkt. H. Mwakyemba, (Aliyesimama) akiongea mbele ya Rais wa kwanza wa Zambia Mhe. Kenneth Kaunda wakati wajumbe kutoka Tanzania walipomtembelea Rais huyo katika ofisi zake. Wengine katika picha ni wajumbe wa Bodi ya Tazara kutoka Tanzania.
Rais wa Kwanza wa Zambia Keneth Kaunda wa nne kutoka kushoto akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Tanzania na Zambia. Kulia kwa Mhe. Kaunda ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia mama Grace Mujuma na anayefuata ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Eng. Omar Chambo. Kushoto kwa Mhe. Kaunda ni Waziri wa Uchukuzi Mhe. Dkt. Mwakyembe, akifuatiwa na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Saada Salum na anayefuta ni Waziri wa Uchukuzi wa Zambia Mhe. Christopher Yaluma, Wengine katika picha ni Wajumbe wa Bodi ya TAZARA kutoka Tanzania.