MKOA wa Mbeya nao umechaguliwa kubeba jahazi la kufanyika Tamasha la Pasaka Aprili mosi mwaka huu.
Mapema wiki hii waandaaji wa tamasha hilo walisema kuwa siku yenyewe ya sikukuu ya Pasaka, Machi 31 litafanyika jijini Dar es Salaam na kwamba walikuwa wakihangaika kutafuta mahali litakapofanyika siku inayofuata.
“Tumekubaliana kuwa Jumatatu ya Pasaka, ambayo itakuwa Aprili mosi, tamasha letu lifanyike mkoani Mbeya. Hivyo tayari tumepata mikoa miwili ambayo tamasha litafanyika bado mingine mitano.
“Mkoa wa Mbeya umechukua jukumu la kufanyika Jumatatu ya Pasaka kutokana na idadi kubwa ya mashabiki waliokuwa wameomba awali siku yenyewe ya tamasha ifanyike mkoani humo, lakini kwa kuwa Dar es Salaam iliongoza tukaamua Mbeya iliyoshika nafasi ya pili basi ipewe jukumu la kuandaa Jumatatu ya Pasaka,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo,Bwa. Alex Msama.
Alisema kamati yake ilikuwa ikiendesha kura za maoni kwa mashabiki wao wa eneo lipi tamasha hilo lifanyike na kwamba Dar es Salaam na Mbeya ndizo zimeshika nafasi za juu.