Quantcast
Channel: MICHUZI BLOG
Viewing all 118915 articles
Browse latest View live

VIONGOZI KATA YA KIBADA WAHAMASISHA USAFI WA MAZINGIRA,WANANCHI KUJIKINGA NA CORONA

$
0
0


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

VIONGOZI wa ngazi mbalimbali katika Kata ya Kibada wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam wameshiriki kuhamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira pamoja na kuwahimiza kuchukua tahadhari ili kukabiliana na janga la Corona.

Miongoni mwa viongozi walioshiriki kufanya usafi kwa kushirikiana na wananchi wa Kibada ni Ofisa Tarafa wa Somangila Augusta Safari, Diwani wa Kata ya Kibada Amiri Sambo, Mwanasheria wa Manispaa ya Kigamboni Charles Lawiso , maofisa watendaji Kibada pamoja na wenye viti wa mtaa.

Akizungumza na waandishi wa habari ,Diwani wa Kata ya Kibada Amiri Sambo amesema viongozi hao wameamua kuhamasisha usafi na wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya Corona kwa kuvaa barakoa na kunawa maji kwa sabuni na maji tiririka.

"Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan ametuhamasisha tuchukue tahahadhari kwa ajili ya Corona, hivyo tumekuja kuwaambia wananchi umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya na watalaamu wa afya.

"Pia tumekuja kuhamasisha usafi, kwa hiyo leo viongozi wa Kata ya Kibada tukiongozwa na Ofisa Tara wetu tumekutana kufanya safi wa pamoja katika eneo hili.Hali ya usafi Kata ya Kibada sio mbaya lakini ni vema tukaendelea kusimamia kwani tusipoasimamia uchafu utakuwa mwingi na kuhatarisha afya za wananchi.

Aidha wakati wakiendelea kuhamasisha usafi, amefafanua kuna mipango mizuri ya Serikali kwa wafanyabiashara wa wananchi wa Kibada ambapo hivi sasa ujenzi wa soko unaendelea na Oktoba mwaka huu litakuwa limekamilika , litakuwa na vizimba 173.

"Tunaishukuru Serikali ilivyojitoa kwa ajili yetu, kwa hiyo wafanyabiashara wadogo wadogo 173 watapa vizimba ,wenye bucha watapata na hii inakwenda kuondoa kero ya wafanyabishara kupanga biashara kando ya barabara."

Kwa upande wake Ofisa Tarafa Somangila wilayani Kigamboni Augusta Safari amesema wameendelea kuhamasisha usafi katika meneo ya Wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya kipaumbele cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala.Pia Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa amekuwa akiwahimiza viongozi kusimamia usafi kwenye maeneo yao.

"Kwa hiyo sisi viongozi ambao ni wasadizi wa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni leo tumekuja Kibada kuhamasisha usafi kwa kuwashirikisha viongozi wa kata na mitaa. Lakini lengo letu kubwa ni kukumbusha wananchi lazima tushirki kufanya usafi katika maeneo yetu kwani tunakinga afya zetu, pia tunapofanya usafi tutajikinga na magonjwa yakiwemo ya mlipuko.

"Tumepita kwenye hospitali, vituo vya afya, maeneo ya sokoni na kwa wananchi ambako kote huko tumeshiriki kufanya usafi na kuhamasisha wananchi kuweka mazingira yao katika usafi.Pia wakati tukiendelea kufanya yote haya Rais wetu ameendelea kusisitiza tuendelee kujenga uchumi lakini tusisahau kuchukua tahadhari dhidi ya Corona,"amesema Safari.

Wakati huo huo Mwanasheria wa Wilaya ya Kigamboni Charles Lawiso amewakumbusha wananchi hasa wafanyabiashara kwamba kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ni jambo ambalo lipo kwa mujibu wa sheria, hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kufanya usafi bila kushurutishwa na watakaokaidi kuna faini inayoanzia Sh.50,000 hadi Sh.300,000.

"Hivyo kila ifikapo Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi wafanyabiashara wanatakiwa kufanya usafi kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa tatu asubuhi na baada ya hapo ndipo watafungua maeneo yao ya biashara, hivyo tumendelea kuhamasisha na kutoa elimu katika Kata mbalimbali na leo tuko Kata ya Kibada , tumetoa elimu kwa baadhi ya wananchi ambao wamefungua maduka yao bila kufanya usafi lakini na adhabu ambazo wanaweza kuzipata iwapo watakaidi kwa miezi inayokuja,"amesema.

Amesema siku ya usafi imewekea sheria, hiyo kwa watakaokiuka watatozwa faini,lakini kikubwa wamewaelimisha wananchi hakuna sababu ya kusubiria faini."Hapo baadae tutaanza kutoza faini kwa watakaoshindwa kufanya usafi."

Ofisa Tarafa wa Somangila Augusta Safari(kulia) akiwa na Diwani wa Kata ya Kibada wilayani Kigamboni Amiri Sambo(kushoto)wakiwa wamebeba tenga lenye uchafu kwa ajili ya kupeleka kwenye gari la kubeba taka wakati viongozi wa ngazi mbalimbali walipokuwa wakihamasisha usafi wa mazingira ndani ya Kata hiyo na Wilaya kwa ujumla.
Diwani Kata ya Kibada Amiri Sambo(katikati) akiwa kwenye kijiwe cha bodaboda akihamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira na kuwakumbusha kuvaa barakoa na kunawa maji kwa sababu na maji tiririka ili kujikinga na Corona.
Mwanasheria wa Manispaa ya Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam Charles Lawiso(wa pili kulia) akizungumzia umuhimu wa wananchi kufanya usafi yakiwemo ya biashara kila ifikapo Jumamosi ya mwisho ya kila mwezi na wale ambao watakaidi watatozwa faini ambayo ipo kwa mujibu wa sheria.
Ofisa Tarafa wa Somangila wilayani Kigamboni Augusta Safari (wa pili kushoto) akisisitiza jambo wakati wa kampeni hiyo ya kuhamasisha wananchi kufanya usafi na kuendelea kuchukua tahadhari ya Corona.Wa kwanza kulia ni Ofisa Afya Kata ya Kibada Yusar Aboubakari na wa pili kulia ni Ofisa Mtendaji Kata Kibada Salome Nyoni.
Diwani wa Kata ya Kibada wilayani Kigamboni Amiri Sambo(kushoto) akiwa na mmoja watendaji katika kata ya Kibada wakiweka maji kwa ajili ya kuwezesha wananchi kunawa mikono kama sehemu ya jitihada za kukabiliana na Corona.
Ofisa Tarafa wa Somangila wilayani Kigamboni Augusta Safari (kulia) akiwa na viongozi wengine wa Kata ya Kibada wakizoa taka wakati wa kampeni ya kuhamasisha usafi wa mazingira ndani ya Kata hiyo.
Diwani wa Kata ya Kibada Amiri Sambo(kulia) akisisitiza jambo.Kushoto ni Ofisa Tarafa wa Somangila Augusta Safari.
Kazi ya uzoaji taka ikiendelea kufanywa na viongozi wa ngazi mbalimbali walioshiriki kufanya usafi wa mazingira Kata ya Kibada wilayani Kigamboni.
Mwanasheria wa Manispaa ya Kigamboni Charles Lawiso (kushoto) akishiriki kufanya usafi baada ya kuwahamasisha wafanyabiashara kushiriki usafi na hasa kila ifikapo Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi ambayo ipo kwa mujibu wa sheria.Kulia ni Augusta Safari ambaye ni Ofisa Tarafa wa Somangila.
Viongozi wa Kata ya Kibada wakisafisha tenki la kuweka wakati walipokuwa eneo la Kibada Centre kuhamasisha usafi wa mazingira na wananchi kuchukua tahadhari ya Corona.


Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kampeni ya viongozi wa Kata ya Kibada wakihamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira.
 


Wanafunzi 12 mkoani Njombe wafanya vizuri kwenye utafiti sasa kushindanishwa Dar

$
0
0

Na Amiri Kilagalila,Njombe

Wanafunzi 12 kwa mara ya kwanza kutoka shule tofauti mkoani Njombe wamefanikiwa kufanya vizuri kwenye maonesho ya wanasayansi chipukizi (Young Scientists Tanzania) kwa kuandaa utafiti (Reserch) mzuri hatua inayowawezesha wanafunzi hao kujiandaa vizuri ili kushiriki maonesho katika hatua nyigine yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar Es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kuwavisha medali pamoja na vyeti ,Mwalimu Charles John ambaye ni afisa taaluma mkoa wa Njombe amesema program hiyo imefanyika kwa mara ya kwanza katika mkoa wa Njombe lakini wanafunzi wamefanikiwa kuonesha vizuri maandalizi yao mazuri ya utafiti katika mazingira yao.

“Watoto wameandaa vitu vizuri na ninajua mbele ya safari katika maonesho mengeni watakayokwenda kuonesha Dar es Salaam wana nafasi nzuri sana ya kuonyesha uwezo wao walio nao.Na nimewakumbusha kuwa watakaoshinda kwenye maonyesho ya kitaifa watapata nafasi ya scholarship kutoka kwenye shirika kwa ajili ya kwenda kusoma chuo kikuu chochote ndani ya nchi au nje ya nchi”alisema Mwalimu Charles John

Fadhil Mwasomola ni mratibu wa Young Scientist mkoa wa Njombe,amesema anaamini wanasayansi chipukizi waliofanikiwa wataendelea kufanya vizuri kama ambavyo malengo ya shirika hilo kwa wanafunzi kukabiliana na chanagamoto za mazingira tuliyo nayo.

“Kwa kuwa tunawaandaa wanafunzi kuweza kukabiliana na mazingira tuliyo nayo kwa hiyo tunaamini kulingana na tafiti wanazozifanya kutona na mazingira yao basi watatusaidia kuibadilisha Tanzania kwa kufanya lolote”alisema Fadhil Mwasomola.

Jesca Mwalongo ni mwanafunzi kutoka shule ya sekondari Hagafilo walioandaa utafiti wa kilimo na Alex Mgimba ni kutoka shule ya sekondari Matola waliondaa utafiti kwenye maswala ya mitandao.Wamesema wamevutiwa kuingia katika mashindano hayo ili kutanua uwezo wao wa kufikiri.

“Niliingia kutokana na uelewa nilioupata ili kujitanua zaidi namna ya kufikiri kutokana na changamoto ambazo tunakutana nazo watanzania”alisema Alex Mgimba

Naye Jesca Mwalongo amesema “Mkoa wetu umekuwa ukikabiliwa na tatizo la utapiamlo kwa hiyo tumeona ni vema kufanya utafiti ili kutatua tatizo la utapiamlo kwa kupata baadhi ya virubisho kutoka kwenye mboga mboga ambazo tunazalisha”.

Wanafunzi 12 kutoka shule tofauti za mkoa wa Njombe waliofanikiwa kufanya vizuri zaidi kwenye utafiti wakiwa wamevalishwa medali ya ushindi na tayari kwa kujipanga ili kushiriki mashindano mengine jijini Dar es Salaam

WAZIRI CHAMURIHO AWATAKA WAHANDISI KUCHANGAMKIA FURSA YA MIRADI

$
0
0

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho amewataka wahandisi washauri kuchangamkia fursa zinazotolewa katika miradi ya kielelezo hapa nchini, ili kuweza kukua kitaaluma na kukuza uchumi wa Taifa.

Alitoa rai hiyo wakati akifungua mkutano wa 35 wa mwaka wa wahandisi washauri ulioandaliwa na Umoja wa Wahandisi Washauri  (ACET), mkoani Dar es Salaam uliobeba kaulimbiu ya uhusikaji wa wahandisi washauri wazawa katika miradi ya kielelezo.

Dk. Chamuriho alisema: "kuhusika kwa wahandisi washauri katika miradi kunasaidia kuendana na Dira ya Taifa ya mwaka 2020-2025 ya kuwa Taifa la uchumi wa kati wa chini kwa miaka mitano kabla ya wakati wake"

Aliongeza: "Mafanikio haya kwa kiasi kikubwa yanahusishwa na ninyi wahandisi kwani miradi hii ndiyo inayoleta mafanikio makubwa katika uendelezaji wa miundombinu ambayo ndiyo chachu ya ukuaji wa uchumi"

Alisema ni jukumu la wahandisi kuhakikisha miradi mikubwa ambayo ni ya kielelezo inatendewa haki kwa weledi na kuzingatia thamani ya fedha, ili kuleta tija  kwa taifa na kuwawezesha kupata fursa zaidi katika miradi  inayotekelezwa hapa nchini.

Aidha, aliwakumbusha wahandisi hao kuwa sayansi na teknolojia vinakuwa kwa kasi, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanajijengea uwezo ili kuendana na kasi hiyo kwa kuhudhuria kozi mbalimbali zinazotolewa ndani na nje ya nchi.

Kuhusu changamoto za kutoaminiwa katika utekelezaji wa miradi mkubwa, Dk. Chamuriho alisema Serikali imeweka sera yenye mambo makuu matatu ambayo ni kujenga uwezo wa upatikanaji wa masoko, kupiga chapuo kwanye teknolojia ili  kukuza wakandarasi wazawa.

"Sera hii ya ndani inawezesha makandarasi wa nje kuwahusisha makandarasi wa wazawa ili kuweza kuwainua hivyo hakikisheni mnazijua sera hii ya ndani, Sheria ya Manunuzi ya umma pamoja na kanuni zake ili muweze kuzitekeleza," alisema Dk. Chamuriho

 Alisema ili kuwafanya wahandisi washauri waweze kuaminiwa zaidi ni vema wakajiunga ili kuweza kutengeneza kampuni kubwa zenye uwezo wa kutekeleza miradi kwa weledi zaidi.

Naye Rais wa Umoja wa Wahandisi Washauri (ACET),  Mhandisi Deogratius Mugishagwe, aliiomba serikali kuhakikisha wahandisi wanahusishwa katika mpango wa maendeleo wa serikali wa miaka mitano pamoja na kuwawezesha kulipwa kwa wakati kwa kupanga miradi inayotekelezwa kwa kufuata vipaumbele.

Alisema changamoto kubwa wanazokabiliana nazo ni pamoja na kuingiliwa na watu wasiokuwa na ujuzi wa fani, kuchelewa kwa malipo.

Mugishangwe alisema ACET wanachokifanya ni kuhakikisha wahandisi washauri wanajengewa uwezo kila wakati ili waweze kuwa na uwezo wa kushindana na wahandisi washauri kutoka nje ya nchi.


 

SPIKA NDUGAI AKIZUNGUMZA NA WAKURUGENZI WA OFISI YA BUNGE

$
0
0

Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai akizungumza katika kikao cha wakurugenzi na wakurugenzi wasaidizi wa Ofisi ya Bunge kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge Zanzibar

 

TAARIFA YA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI KUHUSU UTEKELEZAJI WA SERIKALI YA AWAMU YA SITA, AGOSTI 1, 2021

$
0
0

 

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa

 

Ndugu waandishi wa habari, habari za mchana.

 Leo ni mara yangu kwa kwanza kukutana nanyi waandishi wa habari wenzangu wa hapa Jijini Dar es Salaam tangu nilipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.

 Kabla ya kukutana nanyi hapa Dar es Salaam nimekutana na Waandishi wa Habari wenzetu wa Jijini Dodoma mara mbili na hata taarifa ya mwisho ya Msemaji Mkuu wa Serikali ambayo tunaitoa kila mwezi niliitoa Dodoma tarehe 04 Juni, 2021.

 Awali ya yote kabisa naomba kuwashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa mlionipa katika kipindi chote cha miaka 5 na miezi 5 nilipokuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU. Kwa pamoja tulifanya mambo mengi na kwa dhati ya moyo nataka kusema kazi yangu ilikuwa nyepesi kutokana na jinsi mlivyokuwa tayari muda wote kufanya kazi za Ikulu.

 Matarajio yangu ni kuwa tutaendelea kushirikiana katika majukumu haya mapya niliyopangiwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeniteua kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali tangu Aprili 04, 2021.

 Nami nataka kuwahakikishia kuwa nipo tayari kushirikiana nanyi kuikuza sekta hii ya habari. Nitamani kuona tunashirikiana sio tu kusimamia sheria na taratibu bali kuileta, kuiheshimisha na kupandisha thamani yetu machoni mwa tunaowahudumia.

 Sasa ndugu zangu mwezi uliopita sikufanya mkutano na waandishi wa habari wa kila mwezi kwa sababu niliona tuupishe mwezi huo kwa ajili ya kupata hotuba muhimu ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipozungumza na Wahariri kuhusu siku 100 za tangu aingie madarakani.

 Kwa niaba ya Serikali naomba kuwashukuru waandishi wa habari wote kwa jinsi mlivyoshiriki ipasavyo kutoa taarifa mbalimbali na muhimu kuhusu utendaji wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha siku 100 za kwanza. Mmefanya kazi kubwa ya kuandaa Makala za magazeti, Makala za redio na televisheni, habari mbalimbali, vipindi vya majadiliano na kutangaza maudhui mbalimbali yaliyohusu utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi hicho.

 Mhe. Sami Suluhu Hassan anawashukuru sana kwa jitihada hizi kubwa mnazozifanya na anawaomba muendelee kufanya hivyo kwa kuwa sote kwa pamoja tunaijenga Tanzania yet una sisi waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuitangaza sura njema ya Tanzania ndani na nje ya mipaka yetu. Mhe. Samia Suluhu Hassan anasema anawapenda waandishi wa habari wote na anawaamini sana katika jukumu hilo, hatarajii kuona mnamzingua.

 

Leo nitakuwa na masuala kadhaa ya kuwapa taarifa kutoka Serikalini.

 

1.   Hali ya Serikali

Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea vizuri kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na Sheria.

 

Kwa ujumla Serikali inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kiutawala na kimaendeleo.

 

Hali ya ulinzi na usalama ni nzuri, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha nchi ipo salama, mipaka ya nchi yetu inalindwa ipasavyo na Watanzania wanakuwa na hali ya amani na utulivu ambayo inawawezesha kufanya shughuli zao mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

 Ulipaji wa mishahara ya wafanyakazi, unaendelea kufanyika kama kawaida. Wafanyakazi wanalipwa mishahara yao kabla ya mwezi kuisha, wafanyakazi wenyewe watakuwa mashahidi mishahara wanaipata kabla ya tarehe 25 ya kila mwezi bila kukosa. Tunalipa takribani shilingi Bilioni 630 kwa mwezi.

 Pamoja na kulipa mishahara ya wafanyakazi, kama ilivyoahidi kwa mara ya kwanza mwezi Juni 2021 Serikali imetekeleza ahadi yake ya kuanza kuwalipa Madiwani moja kwa moja kutoka hazina. Katika Mwezi Juni huu Madiwani wamelipwa shilingi Bilioni 1.8, hawa ni Madiwani wote isipokuwa wale wanaotoka Majiji na baadhi ya Manispaa zenye ukusanyaji mkubwa wa mapato (yaani halmashauri ambazo zipo katika daraja la A).

 Kwa kufanya hivi Serikali imeondoa tatizo ambalo katika baadhi ya halmashauri Madiwani walikuwa wanakosa malipo ya mwezi kutokana na uwezo mdogo wa halmashauri, na kulazimika kukopwa. Sasa kila Diwani analipwa moja kwa moja kutoka hazina kiasi cha shilingi 350,000 kwa mwezi na wenyeviti wao wanalipwa shilingi 400,000.

 Serikali inaendelea kulipa madeni ya ndani ya wazabuni na watoa huduma mbalimbali na kwa kufanya hivyo mzunguko wa fedha umeendelea kuongezeka, na mzunguko wa fedha unapoongezeka maana yake vipato vya wananchi vinaongezeka na ajira zinaongezeka.

 Serikali imeendelea kugharamia miradi ya maendeleo. Kama mnavyojua tunayo miradi ya maendeleo ya kimkakati, na tunayo miradi ya maendeleo ya kawaida ikiwemo ya ujenzi wa barabara, miradi ya maji, hospitali, vituo vya afya na zahanati, ujenzi wa majengo mbalimbali, umeme, viwanja vya ndege n.k

 Katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2020/2021 ambayo ni kati ya Aprili na Juni Serikali imetoa kiasi cha shilingi Trilioni 2.785 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimali ya maendeleo. Humu ndani yake kuna miradi ya maji, barabara, madaraja, viwanja vya ndege, kununua ndege, umeme, majengo ya shule, elimu bila malipo, mikopo ya elimu ya juu, maabara, madarasa, reli, meli, nyumba, dawa na vifaa tiba na mengineyo.

 

Hali ya kichumi.

Uchumi wetu umeendelea kuwa imara.

Mfumuko wa bei kwa mwezi Juni ulikuwa 3.6% ambayo ni chini ya ukomo uliopangwa wa 5%.

 Serikali imeendelea kuimarisha viashiria vya ukuaji wa uchumi ili kufikia ukuaji wa asilimia 5.6 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 wa mwaka 2020.

 Aidha, akiba yetu ya fedha za kigeni hadi Julai 2021 ilikuwa ni Dola za Marekani Bilioni 5.5 ambazo zinatosheleza kununua bidhaa na huduma kwa takribani miezi 6.5. kiwango hiki ni zaidi ya lengo la utoshelevu la akiba ya miezi 4.5 lililowekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

2.   Chanjo ya Uviko -19 (ugonjwa wa Korona)

Tarehe 24 Julai, 2021 nchi imepokea shehena ya kwanza ya chanjo 1,058,400 kutoka nchini Marekani. Chanjo hizi ni aina ya Johnson & Johnson (Jansen) na zimeletwa chini ya mpango wa Shirika la Afya Duniani uitwao (Covax Facility) ambao unatoa msaada wa chanjo za kukabiliana na Uviko 19 kwa nchi mbalimbali duniani hasa zinazoendelea.

Chini ya utaratibu wa mpango huu, Tanzania kama ilivyo kwa nchi zingine itapatiwa chanjo za kutosheleza asilimia 20 ya wananchi wote wa Tanzania (ukifanya hesabu utaona chanjo zitakazoletwa ni takribani dozi 11,000). Kwa hiyo chanjo 1,058,400 zilizoletwa ni sehemu ya chanjo hizi.

 Kama sote tunavyojua Mhe. Samia Suluhu Hassan juzi amezindua chanjo hizi, kwa yeye mwenyewe kuchanja na viongozi wengine kuchanja huku vyombo vya habari vikionesha zoezi hilo Mubashara.

 Kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakamilisha taratibu za kupeleka chanjo katika vituo mbalimbali vya Mikoa yote hapa nchini. Vimeainishwa vituo 550 lakini maelekezo ya Wizara ya Afya kuwepo flexibility katika mikoa yenyewe wakiona kuna umuhimu wa kuongeza kituo basi wafanye hivyo lakini kwa kuzingatia muongozo wa utoaji wa chanjo uliowekwa na Wizara.

 Tangu zoezi limeanza mambo yanakwenda vizuri hakuna malalamiko ambayo Serikali imeyapata kutoka kwa wanaopokea chanjo hiyo. Wataalamu wetu wamezikagua chanjo zilizoletwa na wametuhakikishia kuwa chanjo hizi ni salama na zinafaa. Pamoja na viongozi wetu wao wenyewe wataalamu wanachoma chanjo kwa ajili ya kujikinga wao wenyewe na kuwakinga watu wengine.

 Serikali inawasihi Watanzania wote kufuata maelezo na miongozo inayotolewa na Wataalamu wetu.

 Kumekuwa na uchochezi na upotoshaji mwingi kwenye jamii unaoenezwa na watu wasiokuwa wataalamu katika masuala haya, upotoshaji huu kwa sehemu kubwa unafanywa kupitia mitandao ya kijamii. Natoa wito kwa vyombo vya habari, tufanye kazi zetu kwa kuzingatia weledi na kutovunja sheria za nchi yetu. Tusije tukajiingiza kwenye kuchochea uchochezi huu na kusababisha wananchi kutotumia fursa hii ya kukabiliana na ugonjwa wa korona.

 

Tunasisitiza chanjo hii ni hiari, ukiona inafaa kuchanjwa nenda kwenye vituo vilivyotengwa nchi nzima kachanje ukiona vipi hulazimishwi. Kumekuwa na watu ambao wanatumia picha na majina ya viongozi kuwatisha wananchi, naomba watu hao waache mara moja kwa sababu wanachokifanya ni uhalifu na yeyote atakayefanya uhalifu atafikiwa. Hata waliotengeneza upotoshaji kwa kutumia picha yangu wamekamatwa na watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria taratibu zikikamilika.

 

Aidha, Serikali inaendelea kusisitiza Watanzania wote kuzingatia tahadhari zote zilizotolewa na wataalamu wa afya juu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu.

 

Msimamo wa Serikali ni kuwa shughuli za maisha yetu ya kawaida ziendelee lakini tuzingatie mwongozo ambao wataalamu wetu kupitia Wizara ya Afya wameutoa utakaotusaidia kukabiliana na maambukizi. Mwongozo huu ndio unaotutaka kuvaa barakoa, kunawa maji tiririka kwa sabuni, kutumia vitakasa mikono, kujiepusha na misongamano na pale inapobidi basi tuzingatie umbali usiopungua meta moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine, kufanya mazoezi na pia kupimwa joto tunapoingia katika maeneo ya jumuiya.

 

Na ndugu zangu waandishi wa habari kwa kuwa nasi ni moja ya makundi yaliyokatika hatari ya kuambukizwa virusi vya korona leo Ofisi yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto tumeandaa utaratibu ambapo kwa wale watakaokuwa tayari kuchoma chanjo watachoma.

 

3.   Hali ya utoaji wa huduma za kijamii.

Serikali imeendelea kutekeleza jukumu lake la utoaji wa huduma za kijamii kama vile matibabu, maji, umeme na nyinginezo.

 

Kwa matibabu pamoja kuendelea na ujenzi wa miundombinu ikiwemo Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati katika maeneo mbalimbali. Serikali imetoa shilingi Bilioni 130 kwa ajili ya kuagiza dawa kufuatia dawa kupungua katika vituo vya kutolea tiba, na hili limekwenda sambamba na kuwalipa wazabuni ambao walisambaza dawa na kukawa na madeni (hawa wazabuni wamelipwa shilingi Bilioni 39).

 

Aidha Serikali imetoa shilingi Bilioni 14 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mipira (gloves), vidonge vya rangi mbili, dawa za maji za watoto na vidonge vya kawaida katika eneo la Idofi, Makambako Mkoani Njombe. Hii ni hatua kubwa na muhimu kwa nchi yetu kwa sababu inatuondoa kwenye utegemezi wa dawa. Kwa kujenga kiwanda hiki pekee Serikali itaokoa shilingi Bilioni 33 ambazo zingetumika kama dawa na mipira ya mikono inayozalishwa katika kiwanda hiki ingeagizwa kutoka nje ya nchi.

 

Kwa Maji, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji kwa Watanzania. Kama mnavyojua lengo ni kuhakikisha ifikapo 2025 Watanzania waishio mijini wanapatiwa maji kwa asilimia 95 na Vijijini kwa asilimia 85. Kwa sasa mijini maji yamewafikia wananchi kwa asilimia 86 na vijijini ni asilimia 72.3.

 

Kuna miradi ya maji ambayo imekamilika kwa asilimia 100. Baadhi yake ni;

·        Mradi wa maji ya Ziwa Victoria kwenda Tabora, Igunga na Nzega uliogharimu shilingi Bilioni 617.

·        Mradi wa maji wa Magu uliogharimu shilingi Bilioni 16.

·        Mradi wa Misungwi uliogharimu shilingi Bilioni 13.

·        Mradi wa maji wa Kagongwa – Isaka uliogharimu shilingi Bilioni 24.

·        Mradi wa maji wa Lamadi uliogharimu shilingi Bilioni 12.

·        Mradi wa maji wa Sumbawanga ambao umegharimu shilingi Bilioni 35.

Hii ni baadhi tu ya miradi.

 

Kuna miradi ya maji ambayo utekelezaji wake unaendelea.

·        Mradi mkubwa wa maji wa Arusha utakaogharimu shilingi Bilioni 520 hadi kukamilika umefikia asilimia 71.

·        Mradi wa maji wa Mgango – Kiabakari  utakaogharimu shilingi Bilioni 70 umefikia asilimia 15.

·        Mradi wa maji wa Orkesument – Simanjiro utakaogharimu shilingi Bilioni 40 umefikia asilimia 97.

·        Mradi wa maji wa Tinde – Shelui utakaogharimu shilingi Bilioni 24 umefikia asilimia 20.

·        Mradi wa Maji wa Isimani- Kilolo – Iringa utakaogharimu shilingi Bilioni 9.5 umefikia asilimia 40.

·        Na kuanzia mwezi Novemba mwaka huu 2021 tutaanza kujenga mradi wa maji wa Simiyu utakaogharimu shilingi Bilioni 444.

 

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam kazi kubwa imefanyika kuhakikisha Mkoa huu unapata maji ya kutosha. Dhamira hii imefanikiwa kwa sehemu kubwa baada ya kukamilisha miradi ya maji ya Kisarawe, Pugu – Gongolamboto  na Mkuranga. Kazi inayoendelea sasa ni kushughulikia matatizo ya maji yaliyopo Kigamboni, Chalinze na Kibamba.

 

Lakini mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kutumia vyanzo vya maji vya uhakika ikiwa ni pamoja na mito na maziwa makuu yakiwemo Victoria, Nyasa na mito ya Ruvuma, Kagera, Rufiji na Kiwira. Hii itasaidia kuondoa tatizo la kujenga mradi ambao baadaye utapata changamoto ya chanzo cha maji.

 

Kwa hiyo kuna miradi mikubwa zaidi ya maji inakuja. Dhamira ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha anamtua Mama ndoo, na ameshasema kwamba kwenye eneo hili atatupia macho sana. Kwa hiyo wadau wote wa maji tujue mwelekeo huu wa Mhe. Rais na tusimzingue.

 

Kwenye umeme, Serikali imeendelea kutoa huduma ya nishati ya umeme kupitia gridi ya Taifa ambayo kwa sasa uzalishaji wake ni Megawati 1,604 kiasi ambacho ni zaidi ya mahitaji yetu ya nchi nzima ya sasa ambayo ni megawati 1,200. Sasa hivi Tanzania ukisikia mgao wa umeme basi ujue hautokani ni uhaba wa uzalishaji bali sababu zingine labda kujenga njia za umeme, kubadilisha transifoma ama kurekebisha mifumo katika maeneo mbalimbali.

 

Kuhusu upelekaji umeme vijijini kazi ya kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini inaendelea vizuri. Hadi sasa Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeshafikisha umeme katika vijiji 10,324 kati ya vijiji vyote 12,268. Kwa hiyo vijiji vilivyobaki ni 1,944 na hivi vyote wakandarasi wapo tayari site wanapeleka umeme ili ifikapo Desemba 2022 vifikiwe na umeme na tubakiwe na kazi ya usambazaji tu.

 

MSISITIZO (Gridi ya Taifa – ningependa kueleza kidogo)

Pamoja na juhudi zilizofanyika, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kujenga njia za umeme za gridi ya Taifa, zitakazosafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400. Tunayo miradi mikubwa ambayo kazi zinaendelea na mingine ipo mbioni kuanza.

                                i.            Tunao mradi wa ujenzi wa kujenga njia ya umeme ya kuunganisha nchi tatu Zambia, Tanzania na Kenya (ZTK).

·        Sehemu ya mradi huu imekamilika kwa asilimia 100 ambayo ni Iringa – Dodoma – Singida – Shinyanga (Kilometa 617) kwa gharama ya shilingi Bilioni 753, kulikuwa na kazi ya kuboresha kituo cha Dodoma na imekamilika pia.

·        Kinachoendelea sasa ni kujenga njia ya kuanzia Singida – Namanga – Arusha (kilometa 414) na hii ndio itaunganisha hadi Isinya nchini Kenya. Kazi hii imefikia asilimia 85 na itakamilika Desemba 2021 kwa ghama ya shilingi Bilioni 594.

                             ii.            Tunao mradi wa ujenzi wa njia ya umeme ya Iringa – Tunduma – Sumbawanga – Kigoma – Nyakanazi (Inaitwa Gridi ya Kaskazini Magharibi). Kipande cha kwanza cha Iringa – Sumbawanga kilometa 418 ujenzi utaanza Novemba mwaka huu kwa gharama ya shilingi Trilioni 1.07 na kipande cha tatu cha Kigoma – Nyakanazi (kilometa 128) ambacho ujenzi wake utagharimu shilingi Bilioni 283 unatarajiwa kuanza mwezi Septemba mwaka huu.

·        Sehemu ya njia hii pia itatumika sasa kuunganisha njia ya kwenda Zambia kukamilisha ile ZTK (Zambia, Tanzania, Kenya).

                           iii.            Tunayo miradi ya ujenzi wa njia za umeme ya kilovoti 220.

·        Tunajenga njia ya umeme ya Nyakanazi – Geita kilometa 114 kwa gharama ya shilingi Bilioni 421. Kazi hii imefikia asilimia 86.

·        Tumekamilisha ujenzi wa njia ya umeme ya Geita – Bulyakhulu kilometa 53 kwa gharama ya shilingi Bilioni 123.

·        Tumekamilisha ujenzi wa njia ya umeme ya Kurasini – Kigamboni Mkoani Dar es Salaam kilometa 14 kwa gharama ya shilingi Bilioni 290. Kazi hii imekamilika mwezi uliopita wa Juni.

 

                           iv.            Tuna mradi wa ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Rufiji (kwenye mradi wa Bwawa la umeme la Julius Nyerere) hadi Chalinze ili ukaungane na Gridi ya Taifa kilometa 167. Ujenzi huu umeanza na unatarajiwa kukamilika Aprili 2022 kwa gharama ya shilingi Bilioni 158. Mkandarasi yupo site. Kazi ni lazima ikamilike mapema kwa sababu Juni 2022 Bwawa la Julius Nyerere litakuwa linaanza kuzalisha umeme na litahitaji njia ya kuusafirisha kwenda gridi ya Taifa.

·        Kutoka hapo Chalinze tutatekeleza miradi miwili ya kujenga njia za msongo wa kilovoti 400.

Kwanza, ni kutoka Chalinze – Kinyerezi (Dar es Salaam) kilometa 115. Kazi hii itaanza Januari 2022.

Pili, ni kutoka Chalinze – Dodoma kilometa 325. Mchakato wa kupata mkandarasi kwa ajili ya kazi hii unaendelea na matarajio ni kuwa mradi huu pia uanza haraka iwezekanavyo.

 

Nimeitaja miradi hii kwa sababu nchi yetu inakwenda kuongeza uzalishaji mkubwa wa umeme kuanzia Juni 2022. Tukianza kuzalisha Megawati 2,115 pale Bwawa la Julius Nyerere nchi yetu itakuwa na zaidi ya Megawati 3,715. Umeme huu tutahitaji kuuza kwa majirani zetu, na ndio maana kuna kazi hizi kubwa zinazoendelea.

 

Kwa elimu, Serikali imeendelea kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari. Katika robo ya mwisho ya mwaka 2020/21 imetoa shilingi Bilioni 62.416. Serikali pia imeendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambapo katika robo hiyo ya mwisho imetoa shilingi Bilioni 137.373.

 

Kwenye eneo la elimu ya juu, katika bajeti ya mwaka 2021/22 Serikali imepanua uwigo zaidi ambapo imeongeza fedha kutoka shilingi Bilioni 450 hadi kufikia shilingi Bilioni 570. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mwanafunzi atakayehitaji mkopo wa elimu ya juu na anakidhi sifa apatiwe mkopo. Na haya ni mafanikio makubwa sana.

 

Lakini fedha nyingine nyingi zimetengwa kwa ajili ya kumalizia maboma ya shule, kujenga nyumba za walimu na kujenga shule moja ya sekondari ya wasichana ya masomo ya sayansi kwa kila mkoa.

 

Kwa sekta ya afya, kazi kubwa imeendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma kwa kuendeleza huduma zinazotolewa na kuanzisha huduma mpya. Kama mnavyojua Serikali inaendelea na maandali ya kutekeleza mpango bima ya afya kwa wote. Katika Bunge la Septemba mwaka huu, Serikali itawasilisha mswada wa sheria ya Bima ya Afy kwa wote ambapo katika mwaka huu wa 2021/2022 imetenga shilingi Bilioni 149.7 kwa ajili ya kuanza kuwapatia bima za afya wananchi watakaotambuliwa kuwa hawana uwezo wa kugharamia malipo ya Bima. Kwa hiyo safari hii ni safari halisi, hakuna maneno maneno. Tunataka Watanzania wote wawe na uhakika wa kupata matibabu.

 

Katika juhudi hizi hizi za kuimarisha huduma za afya, kazi kubwa imeendelea kufanyika katika kuimarisha matibabu ya kibingwa. Mnafahamu lengo la Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa UTALII WA MATIBABU (Medicine Tourism).

Sasa katika kutimiza hili Serikali imeendelea kusambazavifaa vya uchunguzi na tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kama ifuatavyo;

 

                                i.            Imekamilisha usimikaji wa mitambo ya kuzalisha hewa-tiba katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 7 (Geita, Manyara, Dodoma, Dar es Salaam-Amana, Mtwara, Ruvuma-Songea, Mbeya). Mradi huo umegharimu jumla ya shilingi bilioni 8.7. Na hii ndio inayotusaidia katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Uviko – 19, nab ado juhudi nyingine mbalimbali zinahitaji katika kuwezesha hospitali nyingine kuwa na mitambo ya kuzalisha hewa ya oksijeni.

                             ii.            Vilevile, serikali imekamilisha kufunga mashine kwa ajili ya kupasua ubongo bila kufungua kichwa (Angio Suite iliyogharimu 7.9 bilioni) katika Hospitali ya Mifupa ya MOI. Huduma zimeanza kutolewa.

                           iii.            Mtambo wa kisasa wa pili wa Cathlab na Carto 3 wenye thamani ya Shilingi bilioni 4.6 umefungwaa na kuanza kufanya kazi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete. Mtambo huu utatumika kufanya uchunguzi na kutibu magonjwa ya moyo katika ubora wa hali ya juu sana.

                           iv.            Katika Taasisi ya Kansa ya Ocean Road yanaendelea maandalizi ya kusimika mtambo wa Pet Scan itakayogharimu shilingi Bilioni 18 na tayari 14.5 bilioni imeshatolewa.

                             v.            Serikali imenunua mashine 18 za Digital X-rayzenye thamani ya Tzs. Bilioni 5.3, mashine hizi zimepelekwa katika Hospitali za Halmashauri. Hospitali 14 za Wilaya kati ya hizo 18 ambazo ni; Mangaka, Tunduru, Mbinga, Kasulu, Nyamagana, Butiama, Makambako, Makete, Mbarari, Tukuyu, Itumba, Nkasi, Usangi, na Same zimeanza kutoa huduma, na hospitali 4 za Wilaya bado hazijafungwa kwa sababu ukarabati na ujenzi wa majengo yake bado unaendelea.

                           vi.            Pale Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza (Sekou Toure) Serikali imenunua vifaa ambavyo ni CT scan, Ultra Sound na vifaa vya mama na mtoto, upasuaji, utakasaji naincinerator. Vifaa hivi vimeshasimikwa na vinatoa huduma katika. Thamani ya vifaa tiba hivyo vyote ni Tzs. Bilioni 2.2.

                        vii.            Tunasimika mtambo wa MRI katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa (Bugando) wenyethamani shilingi bilioni 2.43.

                      viii.            Tumeshasimika CT Scan katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Mwananyamala– Dar es Salaam) wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.444.

                           ix.            Pia kuna vifaa vingine vyenye thamani ya shilingi Bilioni 6 ambavyo ni Fluoroscopy, Digital X-ray, ultrasound, mama na mtoto, upasuaji, utakatisaji, incinerator vinasimikwa katika hospitali 9 hapa nchini; Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma (Maweni), Bukoba, Misungwi, Musoma, Bukombe, na Chato.

Aidha, Kwa miundombinu Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 150 kukamilisha majengo ya hospitali za Mikoa na Kikanda ambazo zimefikia hatua zifuatazo; Hospitali za Mkoa ya Njombe, Geita, Songwe umekamilika kwa zaidi ya asilimia 98. Sekou Toure-Mwanza ujenzi wake upo zaidi ya asilimia 80. Hospitali za Kikanda, Mtwara ni zaidi ya asilimia 97, Burigi/Chato umekamilika kwa asilimia 100 na Hospitali ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Meta) ipo zaidi ya asilimia 80.

Lakini pia Serikali imeajiri watumishi wa afya zaidi ya 4,127 kwa ajili ya kukabiliana na uhaba wa watumishi katika vituo vya kutolea huduma.

 

 

 

4.   Miradi ya kimkakati.

Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kama ambavyo Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaahidi Watanzania.

 

                     i.        Ujenzi wa Reli ya Kati.

Mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge Railway – SGR) kipande cha kuanzia Dar es Salaam mpaka Morogoro (kilometa 300) ujenzi umefikia asilimia 92. Mkandarasi ameshalipwa shilingi Trilioni 2.181.

TANESCO wameshakamilisha ujenzi wa njia ya umeme kwa ajili ya kuendesha treni yenye urefu wa kilometa 160 kwa gharama ya shilingi Bilioni 73.3.

Katika kipande hiki tunatarajia Treni ya abiria ya majaribio ya kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro inatarajiwa kuanza Novemba 2021.

 

Kipande cha kuanzia Morogoro – Makutupora ya Singina (kilometa 422) kimefikia asilimia 66 na kazi inaendelea vizuri. Mkandarasi ameshalipwa shilingi Trilioni 1.218.

 

Ujenzi wa reli hii kutoka Dar es Salaam – Morogoro Makutupora utagharimu shilingi Trilioni 7.02.

·        Jambo muhimu katika utekelezaji wa miradi hii ni kuwa malipo kwa Wakandarasi yanafanyika vizuri, kila wanapoleta hati za madai ya malipo (Certificates) Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan inawalipa bila kuacha deni lolote.

·        Kwa hiyo Watanzania tuendelee kumuombea Rais wetu, tuiombee Serikali yetu kwa kuwa yale mashaka ambayo baadhi walidhani baada ya kuondokewa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya Tano kwamba miradi ingekwama yameondoka na Mhe. Rais Samia anaendelea na miradi yote kwa kasi kubwa.

 

Kipande cha Tano cha Mwanza – Isaka (kilometa 341), Mkandarasi anaendelea na kazi ya kusafisha njia kwa ajili kujenga tuta la reli.

 

Tayari, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo ya kuanza kwa ujenzi wa kipande Tatu cha kuanzia Makutupora – Tabora na kipande cha nne cha Tabora – Isaka. Maandalizi yanaendelea ikiwa ni pamoja kupata wakandarasi wa kuanza ujenzi.

 

Pia Mhe. Rais ameagiza maandalizi yaanze kuunganisha reli hii kwenda Kigoma na pia kuunganisha reli hii kuanzia Kaliua (Tabora) hadi bandari ya Kalema (Ziwa Tanganyika). Maandalizi haya yote yanaendelea.

 

                   ii.        Bwawa la Julius Nyerere.

Ujenzi wa Bwawa la umeme la Julius Nyerere katika mto Rufiji.

Kazi inaendelea, ujenzi umefikia asilimia 56. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Juni 2022 ambapo utatuzalishia megawati 2,115 zitakazoingia katika gridi ya Taifa.

 

Tayari Mkandarasi ameshalipwa zaidi ya shilingi Trilioni 2.5 na kila anapotoa hati ya madai (Certificate) analipwa papo hapo.

 

Kama mnavyofahamu mradi huu utaambatana na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Kuna eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji la ukubwa wa hekta 150,000.

Bwawa litakusanya maji mengi kiasi cha Meta za ujazo Bilioni 35, katika eneo la urefu wa kilometa 100. Hii itatuwezesha kuzalisha umeme hata wakati usio wa mvua.

 

Kinachoendelea hivi sasa Serikali ni maandalizi ngazi ya Wizara kuweka mpango wa kitaifa wa namna ambavyo fursa za uvuvi, utalii, kilimo na mengine yatavyotumika. Na Kamati hii ipo chini ya Makatibu Wakuu.

 

                 iii.        Ununuzi wa Ndege.

Kama wote mnavyojua Serikali imeshanunua ndege 11, ndege 9 zimewasili na ndege nyingine mbili aina Air (A220-300) zitawasili wakati wowote kuanzia sasa. Hizi ni juhudi za kulijenga shirika letu la ndege la ATCL ambalo linafanya kazi nzuri na kuleta matokeo katika ukuaji wa uchumi na kurahisisha usafiri wa anga kwa Watanzania na wageni wakiwemo watalii.

 

Japo kumekuwa na changamoto ya ugonjwa wa Uviko 19, lakini Shirika letu linaendelea kukabiliana nayo kwa kuhakikisha linafanya kazi kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu ya kuzuia maambukizi.

 

Ndani ya Tanzania ATCL ina vituo 15 inavyotua, na nje ya Tanzania kuna 7 vya kikanda. Hivi Karibuni ndege zetu zinatarajia kurejesha safari zake za Lubumbashi, Msumbuji na Johannesburg. Pia safari za Mumbai-India na Guanzhou-China zinaendelea kufanyiwa kazi ili zirejee hivi karibuni.

 

Upo mpango wa kuongeza ndege zingine 5 ukiondoa hizi 11 ambazo tayari zimeshanunuliwa. Tayari ATCL imetiliana sahihi na watengenezaji wa ndege hizo. (Kati ya ndege hizo1 masafa marefu, 2 masafa ya kati, 1 masafa mafupi na 1 ya mizigo)

 

                 iv.        Ujenzi na uendelezaji wa Jiji la Dodoma (Makao Makuu)

Kazi mbalimbali zinaendelea zikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato utakaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 620, ujenzi wa kilometa 112 za barabara za mzunguko (Ring Roads) utakaogharimu takribani shilingi Bilioni 500, kuna ujenzi wa majengo ya Serikali kwa ajili ya kutolea huduma katika Mji wa Serikali Mtumba, kuna ujenzi wa barabara za ndani ya Jiji la Dodoma.

 

Kuna mradi wa maji wa FARKWA, AfDB wameridhia kutoa fedha za masharti nafuu (kiasi cha shilingi Bilioni 910) kwa ajili ya kujenga Bwana na kulaza mabomba yatakayopeleka maji Chema, Dodoma Mjini, Chamwino na Bahi. Mradi huu utatekelezwa kwa awamu mbili. Kwa sasa maandalizi yanaendelea

                             v.             

 

 

5.     Ujenzi wa Miundombinu (Barabara na madaraja)

Serikali inaendelea na jukumu lake la kupanua mtandao wa barabara, kuna miradi iliyokamilika na miradi mingine inaendelea kutekelezwa. Wakandarasi wanaotekeleza miradi hii wanalipwa kulingana na wanavyozalisha hati za madai ya kazi zao.

 

Barabara.

·        Upanuzi wa barabara kuu ya Kimara – Kibaha (kilometa 19.2) umefikia 90%

·        Ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya pili (kilometa 20.3) kazi imefikia asilimia 22.

·        Ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga - Mpanda (kilometa 356) umefikia asilimia 75.

·        Ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbambabay (kilometa 66) umekamilika kwa 100.

·        Ujenzi wa barabara ya Kabingo – Kasulu – Manyovu (kilometa 260.6) umefikia 7%

·        Ujenzi wa barabara ya Lusitu – Mawengi (kilometa 50) umefikia 69%

·        Ujenzi wa barabara Njombe – Moronga – Makete (kilometa 107.4) umefikia 77%

·        Ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga (kilometa 112) umekamilika kwa 100%

Madaraja

·        Daraja la Tanzanite linalounganisha Coco Beach na Aga Khan Dar es Salaam (kilometa 1.03) limefikia 90%

·        Daraja la JP Magufuli linalounganisha Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria Mkoani Mwanza (kilometa 3.2) limefikia 28%.

·        Daraja la Wami katika mto Wami (meta 510) limefikia 51%

 

 

Lakini kupitia TARURA, mwaka huu Serikali imeamua kuja na mpango maalum kabisa wa kukabiliana na hali mbaya ya barabara. Kwa kutenga shilingi Bilioni kwa kila jimbo kwa ajili ya barabara. Sasa itakuwa ni uamuzi wa jimbo husika kutumia fedha hizo kujenga barabara ya lami ya kilometa 2 au kujenga barabara za changarawe za urefu wa kilometa 20.

 

 

6.   Kuvutia uwekezaji, kuboresha mazingira ya kufanya biashara.

Kufuatia maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyetaka kuongeza jitihada za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, hatua madhubuti zimechukuliwa kuhakikisha vikwazo mbalimbali vinaondolewa. Miongozi mwake ni kutekeleza ule mpango wa kuvutia wawekezaji uitwao Blue Print.

 

Ukusanyaji wa kodi wa maguvu na kutisha walipa kodi umedhibitiwa na sasa walipa kodi wanalipa kodi zao kwa amani na hali inaonesha kuwa nzuri.

 

Mhe. Rais yeye mwenyewe amekutana na viongozi wa taasisi ya sekta binafsi (TPSF) na kuzungumza nao na amekuwa akiambatana nao katika safari zake alizozifanya nchini Kenya na Burundi. Matokeo ni mazuri sana, na wafanyabiashara na wawekezaji wengi wanakuja kuwekeza hapa Tanzania.

 

 

7.   Kuhusu Sensa ya Watu na Makazi.

Kama mnavyojua, nchi yetu hufanya Sensa ya watu na Makazi kila baada ya miaka 10. Sensa inafanyika kwa lengo la kupata idadi ya watu na Makazi ili takwimu hizo zitumike katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaendelea na Sensa ya Majaribio inatarajiwa kufanyika Agosti 2021.

 

Tumeandaa Mkakati wa Mawasiliano kwa ajili ya kutoa elimu na taarifa mbalimbali kwa jamii. Kwa sehemu kubwa mkakati huu utatuhusisha sisi Waandishi wa Habari, niwaombe Waandishi wa Habari wenzangu tutoe ushirikiano katika jukumu hili. Kutakuwa na vipindi, Makala, majarida na kazi nyingine mbalimbali za uandishi na utangazaji, naomba tujitoe kufanya jukumu hili lenye maslahi makubwa kwa Taifa letu.

 

Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (OCGS) tutakuwa tayari muda wote kushirikiana na Vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari kufanikisha jukumu hili muhimu.

 

8.   Hali ya ukusanyaji wa mapato.

Kama mtakumbuka, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipoingia madarakani aliagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iachane na ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mabavu ikiwemo kutumia vikosi kazi na vitisho dhidi ya walipa kodi. Utekelezaji wa maelekezo hayo umefanyika na kumekuwa na hisia miongoni mwa jamii kuwa pengine hatua hii ingeshusha mapato kwa kiasi kikubwa na kuathiri utendaji kazi wa Serikali.

 

Nataka kuwahakikishia kuwa hali ya ukusanyaji wa mapato ni nzuri. Katika robo ya mwisho ya mwaka 2020/2021 yaani kuanzia Aprili hadi Juni 2021 hali ya ukusanyaji wa mapato ilikuwa wastani wa Shilingi Trilioni 4.41 sawa na wastani wa shilingi Trilioni 1.51 kwa mwezi. Na mwezi Juni ambao ni mwezi wa mwisho wa mwaka makusanyo yalipanda hadi kufikia shilingi Trilioni 1.85.

 

Serikali inawashukuru na kuwapongeza Watanzania wote kwa kulipa kodi na inawasihi kuendelea kufanya hivyo kwa kuwa kodi hizi ndizo zinajenga barabara, zinanunua dawa hospitali na katika vituo vyote vya tiba, inagharamia elimu bila malipo katika shule za msingi na Sekondari na ndio inapeleka maji na umeme vijijini.

 

9.   Hali ya Ukusanyaji wa Mapato katika Halmshauri.

Halmashauri zetu zimeendelea kukusanya mapato ambayo pia hutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Katika mwaka 2020/2021 halmashauri zimekusanya shulingi Bilioni 757 ambayo ni asilimia 93 ya malengo ya kukusanya shilingi Bilioni 815. Fedha hizo ni ongezeko la shilingi Bilioni 40 ikilinganishwa na mwaka 2019/2020.

 

Serikali imeshatoa maelekezo kwa halmashauri zote ambazo mapato yake ni chini ya shilingi Bilioni 5 kuhakikisha asilimia 40 ya mapato hayo yanaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi, na kwa halmashauri ambazo mapato yake yanazidi shilingi Bilioni 5 kuhakikisha asilimia 60 ya mapato yake yanaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

 

10.               Kuhusu Tozo ya miamala ya simu.

Natambua kuwa jambo hili ndilo limetawala vinywa vya Watanzania wengine. Serikali imesikia madai ya wananchi na baada ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ya kufanyiwa kazi kwa madai hayo kwa Mawaziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile, Mawaziri hawa wamekutana na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanyia kazi jambo hili.

 

Ndugu zangu waandishi wa habari napenda kuwajulisha kuwa jana Jumamosi Waheshimiwa Mawaziri wamekutana na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwa ajili ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais.

 

Baada ya kupokea taarifa hiyo Mhe. Waziri Mkuu ametoa maelekezo mengine ya kuboresha zaidi taarifa ya Waheshimiwa Mawaziri ili hatimaye madai ya wananchi ya zingatiwe na miradi ya wananchi ambayo inapaswa kutekelezwa kutokana na fedha zilizopangwa kukusanywa katika tozo hizo itekelezwe.

 

Napenda kusisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha inaongeza nguvu katika kukabiliana na matatizo ya hali mbaya za barabara hasa vijijini, kujenga vituo vya afya, hospitali, zahanati, kupeleka maji na huduma nyingine za kijamii.

 

11.               Sekta ya Madini.

Serikali imeendelea kusimamia vizuri sekta ya madini ambayo imepiga hatua kubwa katika miaka mitano iliyopita. Kama mnavyojua katika kipindi hicho mapato ya madini yamepanda kutoka shilingi Bilioni 191 kwa mwaka hadi kufikia shilingi Bilioni 584 katika mwaka uliopita wa 2020/2021.

 

Sitaki kurudia mambo mengi ambayo yamefanyika katika sekta hii lakini naomba niwajulishe kuwa katika mwezi Juni uliopita nchi yetu imeandika historia nyingine kubwa katika sekta ya madini kwa kutoa leseni kubwa mbili za migodi ya madini.

 

Tumetoa leseni kubwa ya mgodi wa madini wa Nyanzaga uliopo Sengerema Mkoani Mwanza na tumetoa leseni kubwa ya madini adimu (Rare Earth Elements) kule Songwe.

 

Zinaitwa leseni kubwa kwa sababu uwekezaji kwenye kila mgodi ni zaidi ya Dola za Marekani Milioni 100 (sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 2.3). Migodi hii kila mmoja utaajiri zaidi ya watu 1,000.

 

Kwenye ule mgodi mkubwa wa Songwe pia kutakuwa na mradi mwingine wa kujenga kiwanda cha kusafisha hayo madini adimu (rare earth elements) hiki nacho kitajengwa hapa hapa Tanzania na kinatarajiwa kuongeza mahitaji ya tindikali ambayo inatumika katika usafishaji. Kwa hiyo wazalishaji wa tindikali dili hilo limekuja kazi kwenu.

 

Lakini mkumbuke sheria yetu ya madini inaipa Serikali umiliki wa asilimia 16 ya migodi hii na bado itakusanya kodi na tozo mbalimbali. Ndio maana tunasema huu ni ushindi mwingine mkubwa katika sekta ya madini.

 

 

12.               Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Kuna kazi kubwa inaendeleza mkongo wa Taifa.

Kama mnavyojua mkongo wetu wenye urefu wa kilometa 8,319 umeunganishwa katika Mikoa yote, na sasa kazi inayoendelea ni ya kuunganisha wilaya zote.

 

Tumefanikiwa kufikisha huduma za mkongo wetu katika nchi zinazotuzunguka ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi na sasa tunaekea kupeleka mkongo katika nchi za Msumbiji na Kongo.

 

Kwa kutambua umuhimu huu katika bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, safari hii Serikali imeongeza bajeti katika Wizara hii ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoka shilingi Bilioni 15 hadi Bilioni 240.

 

Tunataka kujikita zaidi katika eneo hili ambalo lina fursa nyingi za kutuletea mapato na kuzalisha ajira kwa Watanzania wengi. Kwa hivi sasa kazi kubwa inayoendelea kuendelea kuboresha mazingira kwa kupunguza urasimu, na jana mmeona TCRA imezindua mfumo wa kidijitali kwa ajili ya kuchakata maombi ya leseni. Mfumo huu utapunguza muda wa kuomba leseni kubwa na sasa leseni kubwa itapatikana ndani ya siku 45 na leseni ndogo itakuchukua siku zisizozidi 5.

 

13.               Usafiri wa anga.

Serikali imeendelea kuimarisha usafiri wa anga kwa kuchukua hatua kadhaa wa kadhaa za kukamilisha miundombinu ikiwemo viwanja vya ndege 11 vinavyojengwa na kukarabatiwa. Katika robo ya mwisho iliyopita shilingi Bilioni 8.6 zimetolewa katika eneo hili na kazi zinaendelea kukamilishwa.

 

Serikali imelipa fedha za ununuzi wa ndege kiasi cha shilingi Bilioni 38.437 moja kati ya ndege 3 zilizonunuliwa mmeiona jana imepokelewa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ile ndege inaitwa De Havilland Canada – 8 (DHC-8). Ndege hizo haziitwi tena Bombardier Dash 8 Q400 kwa sababu kiwanda hicho sasa kimeuzwa kwa mmiliki mwingine.

 

Lakini ndege nyingine 2 za aina ya Airbus (A220-300) hizo zitafika wakati wowote kabla ya kuisha kwa mwaka huu. Mambo ni moto…….

 

 

 

14.                Sekta ya Kilimo.

Juhudi mbalimbali zinaendelea. Mojawapo kwa sasa ni kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei ya mbolea, tayari Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imechukua hatua ya kukutana na wafanyabiashara wa mbolea. Moja kati ya hatua ilizochukua ni kuondoa utaratibu wa watu wachache kuagiza mbolea na badala yake imeruhusu muagizaji wa mbolea yeyoye kuleta mbolea ilimradi iwe bora kwa uthibitisho wa Mamlaka yetu ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na Shirika la Viwango (TBS).

 

Lakini tungependa wananchi wajue kuwa kupanda kwa bei ya mbolea kunakotokea sasa kwa sehemu kubwa kumesababishwa na kupanda kwa bidhaa hiyo katika masoko ya dunia. Tangu kulipuka kwa ugonjwa wa Korona ziko baadhi ya nchi ambazo ziliamua kujifungia (Lockdown) na zikaacha kuzalisha mazao ya kilimo. Matokeo yake ni kuwa hata viwanda vilisitisha uzalishaji wa mbolea. Sasa baada ya kuondoa lockdown wakulima wamerudi mashambani mahitaji ya mbolea yamepanda ghafla na mbolea imepanda bei.

 

Matarajio yetu ni kuwa hatua ambazo zimechukuliwa na Wizara ya Kilimo kuondoa urasimu na ucheleweshaji wa mbolea pale bandarini zitasaidia kupunguza bei.

 

Habari njema katika eneo hili ni kuwa mwekezaji Aliko Dangote yule aliyejenga kiwanda cha Saruji kule Mtwara ambako amewekeza zaidi ya Dola za Marekani Milioni 770 (Sawa na zaidi ya Trilioni 1.7) ameahidi kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea, na pia kuna wawekezaji kutoka Burundi (Kampuni ya Intracom) wameahidi kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea bila kutumia kemikali Jijini Dodoma kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha tani laki 5 kwa mwaka. Na ukichanganya na mbolea yetu ya Minjingu, mambo yatakaa sawa.

 

15.               Katika Sekta ya Michezo.

Tunafanya vizuri katika michezo.

 

Juzi wote mmeona timu yetu Taifa ya vijana chini ya miaka 23 imeibuka mabingwa wa CECAFA 2021 kule Ethiopia. Timu hii inarejea mchana hu una Mhe. Innocent Bashungwa Waziri wetu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amewaandalia vijana chakula cha mchana ambacho atakula nao na kuwapa neno la pongezi.

 

Tumeanza kuondokana na ombaomba katika kuendeleza michezo, Serikali ya Awamu ya 6 imeanza kutoa fedha kupitia mfuko wa maendeleo ya michezo uliopo BMT. Kuna fedha ambazo huenda hazina kutoka michezo ya kubashiri, sasa Serikali imekubali asilimia 5 ya fedha hizo zipelekwe kwenye mfuko wa kuendeleza michezo.

 

Pia Serikali imeondoa VAT katika nyasi bandia, ili kuondoa gharama kubwa katika nyasi na hivyo kuchochea uboreshaji wa miundombinu ya michezo.

 

Serikali imefufua michuano ya UMITASHUMITA na UMISETA, ambayo mwaka huu imefanyika Kitaifa Mkoani Mtwara. Na Wizara yenye dhamana ya Michezo imeamua kunogesha mashindano haya kwa kuwahusisha wasanii na wote mmeona jinsi mambo yalivyokuwa kule Mtwara.

 

Tumeunda kamati ya Kitaifa ya kurudisha TAIFA CUP na imeanza kazi tayari. Tunataraji michuano hii itafanyika mwaka huu.

16.                       ..

Article 6

$
0
0

 


Adeladius Makwega,Chamwino- WHUSM

 

Katika sehemu ya awali ya makala haya nilimalizia juu ya taarabu asilia kuwa ipo ile inayochezwa na wanawake pekee na ile inayochezwa na wanaume. Hii ni kulingana na mazingira ya watu hao, haswa kwa kuiga mitindo ya taarabu za Kiarabu.

 

Makala haya katika sehemu ya pili leo yanatupia jicho juu ya mianisho ya mashairi ya taarabu asilia. Kulingana na Bi Hadija Kisubu Afisa Utamaduni wa Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo anasema kuwa Waswahili wameainisha ushairi wao katika mistari mitatu: shairi lenye mistari minne katika kila ubeti, utenzi-shairi refu lenye mistari mitatu au minne katika kila ubeti na ambalo huwa limetungwa kama utenzi) na wimbo (shairi lenye mistari mitatu lililotungwa ili liimbike).

 

“Taarabu imeainishwa katika aina ya tatu ya wimbo wenye mistari mitatu katika kila ubeti na mistari wa nne ujulikanao kama kiitikio au kibwagizo. Hata hivyo, kwa mujibu wa wanajadi wa taarabu, kuna Taraab aina moja tu ambayo hufuata mtindo wa mapigo ya taratibu huku wasikilizaji wake wakiwa wametulia tuli kama maji ya mtungini na kusikiliza wakiwa wameketi kitako.” Anaongezea Bi Kisubi.

 

Tofauti na maoni haya ni yale ya wanamapinduzi ambao wanasema kuwa kuna taarabu ya sasa ambayo imeiga midundo mipya na mabadiliko katika uchezaji ngoma na mavazi ya wasanii. Hili limesababishwa na haja ya muziki huu kubadilika kadri wakati ulivyozidi kubadilika kiuchumi, kisiasa na kijamii.

 

Mtaalamu huyu wa masuala ya utamaduni anaelezea kuwa historia ya taarabu imepitia katika vipindi vinne, cha kwanza ni mwaka 1905 hadi 1920. Huu ndio wakati ambapo Sultan Seyyid Bargash alikuwa mtawala wa Zanzibar. Taarabu iliimbwa katika ikulu yake kwa lugha ya Kiarabu kama ilivyokuwa imeigwa kutoka Misri.

 

Wachunguzi mbalimbali wa muziki huu wanasema kuwa uliletwa Zanzibar mnamo 1870 na kikundi cha wanamuziki kutoka Misri kilichokuwa kimealikwa na Sultan Barghash kuimba ikuluni mwake (kama nilivyokudokeza katika makala ya kwanza).

 

Kwa kipindi hiki Zanzibar ilikuwa ngome muhimu ya kibiashara chini ya utawala wa Kiarabu wa Sultani wa Oman. Nyimbo za taarabu katika nyakati hizo zilitumiwa katika kuwatumbuiza viongozi wenye asili ya Kiarabu, wafanyibiashara na mabepari. Sultan Sayyid Bargash aliishi maisha ya anasa na alipenda raha na starehe sana.

 

Baada ya kufanikiwa katika wajibu wake huu, Mohammed alirudi ikuluni mwa Barghash, na baadaye akawa mshairi wa kibinafsi wa Barghash. Mohammed pia aliwafunza marafiki zake kucheza muziki huu, ujuzi walioutumia baadaye walipoanzisha kikundi cha kwanza cha taarabu kilichojulikana kama Nadi Ikhwani Safaa, mwaka 1905 kule Zanzibar.

 

“Taarabu ilisambaa kwingineko katika mwambao wa Afrika Mashariki ikiwemo Mombasa na Lamu. Maudhui katika nyimbo za taarabu zilizoimbwa katika ikulu ya mfalme yalihusu kuomba dua ya mapenzi kati ya Sultan na Malkia, kumwombea Sultan maisha marefu katika utawala wake, kusifu maumbile, huku nyimbo zingine zikiimbwa kwa nia ya kumchangamsha na kumchekesha mfalme. “ Anasema Bi Amne Kassam Afisa Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo.

 

Bi Kassam anasema kuwa watu wa tabaka la juu wakati huo walivaa mavazi yao nadhifu na kuketi vitini wakingoja kutumbuizwa na kikundi hiki cha Nadi Ikhwani Safaa .

 

Mwaka wa 1920 hadi 1940 hiki kilikuwa ni kipindi cha pili cha taarabu. Katika muhula huo, lugha ya Kiswahili ilitumika katika nyimbo za taarabu baada ya enzi ya utawala wa Sultan Barghash kufikia kikomo. Mabadiliko ya muziki wa huu yalisababisha kubadilika kwa hadhi ya nyimbo hizi kutoka kuwa nyimbo za watu wa tabaka la juu katika jamii hadi kuwa nyimbo za makabwela (akina yakhe). Mabadiliko haya yalihusishwa na mhusika wa taarabu aliyesifika sana Zanzibar na nchi za nje,Bi Siti binti Saad.

 

Taarabu ilianza kuwafikia watu wengine mbali na watawala na matajiri baada ya kuwepo kwa utendaji hai wa bendi mbele ya umma na pia kuwepo kwa mbinu ya kurekodi nyimbo hizi. Watu wa tabaka la kati waliweza kuzinunua na kuzisikiza nyimbo za taarabu. Huu ndio wakati ambao Siti Binti Saad, aliyeishi miaka ya 1880-1950, alianza kuimba akitumia lugha ya Kiswahili Zanzibar na Tanganyika.

 

“Siti alifanikiwa kuimba nyimbo nyingi sana za Kiarabu na Kiswahili katika santuri na sahani.Taarabu wakati huo iliweza kuenea hata zaidi kwani Siti alikuwa na uwezo wa kuimba kwa lugha za Kihindi, Kiarabu na Kiswahili. Uwezo huu wa kuchanganya lugha tofauti tofauti katika uimbaji wake uliweza kumpa Siti hadhi kubwa visiwani na kulikokuwa na utamaduni mseto wa Kiarabu na Kiswahili.” Anaongeza Bi Kassam.

 

Ndiyo maana baadhi ya watafiti wa muziki huu wanadai kuwa kwa Waafrika wengi, taarabu kwao ilianza na Siti. Aidha, Siti alianzisha aina ya taarabu iliyojulikana kama Womens’ taarabu ambayo ilikopa sana kutoka utamaduni wa nyimbo za Waswahili na za Kihindi. Siti aliifanya Taarabu kuwa ya Kiafrika kwa kuimba kwa Kiswahili na kuitoa nje ya kasri la kifalme kwa kuiwasilisha kwa watu wa kawaida.

 

Mwaka 1950 hadi 1960 kilikuwa ni kipindi cha tatu cha taarabu ambapo iliweza kuwa huru zaidi kutokana na kuwepo kwa upeperushaji wake katika mawimbi ya redio mbalimbali. Muziki wa taarabu uliweza kusambaa sana katika awamu hii. Katika kipindi hiki utakumbuka kuwa watawala wa kikoloni na Sultan wa Zanzibzr waliweza kusimika mitambo ya kurushia matangazo ya redio na ya kurekodi muziki na nyimbo  za kila aina.

 

Kuanzia mwaka wa 1970 hadi sasa. kumekuwa na ufanisi mkubwa zaidi wa taarabu uliochangiwa na kuwepo kwa runinga, video, tepurekoda,simu za mikononi, na mitandao hivyo ni miongoni mwa vifaa vingine vya kisasa vya kielektroniki. Taarabu imeweza kuenea hadi Msumbiji, Afrika Mashariki, sehemu za Maziwa Makuu kama vile Kongo, Afrika Kaskazini, Magharibi na Mashariki, Bahrain, Yemeni, Saudi Arabia, Uturuki na Bara Hindi.

 

“Mabadiliko katika uimbaji na utendaji yanayoonekana katika muziki wa taarabu ya kileo yamesababishwa na haja ya kuubadilisha muziki huu ili uweze kuambatana na mitindo na aina ya muziki wa kisasa. Utendaji wa muziki wa taarabu umeiga mengi kutoka tanzu nyingi.” Alimalizi Bi Kisubi.

 

Basi kwa leo naweka kalamu yangu chini ili kuweza kukuandalia makala ijayo kwa heri.



WAZIRI MKUU ATEMBELEA SHAMBA NA KIWANDA CHA PARACHICHI RUNGWE

$
0
0


*Awahamasisha wananchi waongeze mashamba, parachichi zina faida kubwa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea shamba la parachichi na kiwanda cha kuchakata mazao ya parachichi na kuwasisitiza wananchi walime zao hilo kwa kuwa faida yake ni kubwa.

Ametembelea shamba hilo leo (Jumapili, Agosti 1, 2021). Shamba lipo katika kijiji cha Ilolo wilaya ya Rungwe, Mbeya na linamilikiwa na kampuni ya Kuza Africa na Moravian Farming PVT.

“Kilimo cha parachichi kina manufaa makubwa sana, wananchi ongezeni ukubwa wa mashamba ya parachichi na Serikali italisimamia kuanzia hatua za maandalizi ya shamba hadi masoko.”

Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote zinazolima zao la parachichi zianzishe vitalu vya kuotesha miche na kuigawa kwa wakulima ili kuhamasisha wananchi wengi kulima zao hilo.

Amesema zao la parachichi ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na linazalishwa kwa gharama nafuu, hivyo amewahimiza wananchi kulima zao hilo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Naye, Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewapongeza wawekezaji hao kwa kuwa wamewezesha wakulima kutatua changamoto ya soko la uhakika wa zao la parachichi.

Naibu Waziri huyo amesema mbali na kupatikana kwa soko la parachichi katika kiwanda hicho pia Serikali itahakikisha soko la parachichi za Tanzania nchini Afrika Kusini linafunguliwa.

Awali, Meneja Rasilimali Watu wa kampuni hizo Noel Kabuje alisema wamewezesha wakulima kupata soko la uhakika la parachichi kupitia ununuzi wa matunda ya parachichi kutoka kwao.

“Mbali na kulima parachichi sisi wenyewe pia tunanunua matunda ya parachichi kutoka kwa wakulima wadogo, tunayachakata na kufungasha matunda ya parachichi na kuyauza nje.”

Meneja huyo alisema mbali na kusafirisha parachichi pia kampuni yao inauza mbegu za matunda ya parachichi zitokanazo na miparachichi ya asili (kienyeji) kwenye soko la dunia.

Alisema kwa sasa kampuni yao imeanza kupanda parachichi za kisasa (Hass Avocado) kwenye mashamba yao pamoja na kwenye mashamba ya wakulima wakubwa na wadogo.Alisema mbali na kuwapandia miche hiyo ya kisasa pia inatoa huduma za ugani na pembejeo kwa wakulima. “Tumeshawafikia wakulima zaidi ya 10,000 ambao tumewapa miche ya kisasa.”

Meneja huyo alisema kwa sasa masoko ya parachichi yameongezeka ambapo wanauza katika nchi za Ujerumani, Italia, Ufaransa, Mashariki ya Kati, Uingereza na Hong Kong. 




SERIKALI YAIAGIZA TIPER KUTOA TAARIFA ZA UENDESHAJI KAMPUNI KWA WAKATI

$
0
0

Na Dorina G. Makaya – Dar-es-salaam

Serikali imeiagiza Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) kuhakikisha inatoa taarifa za uendeshaji wa kampuni hiyo kwa wakati, ili kuepusha changamoto ambazo zinaweza kujitokeza baadaye kutokana na kutokutoa taarifa kwa wakati.

Agizo hilo limetolewa jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Kheri Mahimbali wakati wa ziara yake kwenye kampuni hiyo iliyolenga kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kampuni ya TIPER.

Katika ziara yake, Naibu Katibu Mkuu Mahimbali, ametembelea kwenye maeneo mbalimbali ya kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na matenki ya kuhifadhia mafuta jambo ambalo ameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi wa kampuni hiyo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja, ameishukuru Serikali kwa kufika katika eneo hilo ambapo wameweza kukubaliana masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupeana taarifa kwa wakati.

Amesema, licha ya mafanikio waliyonayo, bado kuna changamoto zinazowakabili huku kubwa ikiwa kuharibika kwa vifaa vya kusukuma mafuta pindi wanapoyatoa kwenye meli, vifaa ambavyo havipatikani nchini hadi viagizwe nje ya nchi.

Kufuatia hali hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali amesema, endapo taarifa hizo zitatolewa mapema, itakuwa mwarobaini wa changamoto hizo.

Ziara hiyo ni mwanzo wa ziara nyingine katika taasisi zote zenye ubia na Serikali katika Sekta ndogo ya Mafuta hapa nchini kwa lengo la kuboresha ufanisi na utendaji.

Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Kheri Mahimbali, aliambatana na baadhi ya viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Nchini Tanzania (EWURA) na Kampuni ya Serikali ya Uagizaji na Usambazaji wa Mafuta nchini (TANOIL).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Mtendaji mkuu wa Kampuni hiyo Michael Mjinja pamoja na baadhi ya viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Nchini Tanzania (EWURA) na Kampuni ya Serikali ya Uagizaji na Usambazaji wa Mafuta nchini (TANOIL) wakipata maelezo ya usalama kabla ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kampuni hiyo tarehe 31 Julai, 2021.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali na Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta wa TPDC Dkt. Wellington Hudson wakimsikiliza Mkurugenzi  Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja (hayumo pichani) mara baada ya kuwasili TIPER tarehe 31 Julai, 2021.



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akizungumza na Waandishi wa Habari wakati alipotembelea Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) iliyopo jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kampuni hiyo.



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja wakati alipotembelea Kampuni hiyo iliyopo jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kampuni hiyo.


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja akitoa maelezo kuhusu utendaji wa Kampuni ya TIPER kufuatia ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali kwenye kampuni hiyo tarehe 31 Julai, 2021.
Watumishi wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali alipokuwa akizungumza nao (Hayumo pichani) alipotembelea kampuni hiyo ya TIPER tarehe 31 Julai, 2021.




WAZIRI AWAOMBA WADAU KUSAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM

$
0
0
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesisitiza kwamba itaendelea kufanya jitahada mbali mbali katika kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika nyanja zote za uchumi na kutoa wito kwa wadau kutoa mchango wao katika kuwawezesha watu wenye ulemavu hususan watoto wadogo ili waweze kupata elimu na malezi bora yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao na hatimaye kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Watu Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, alipokuwa akikabidhi vifaa mbali mbali vya msaada katika shule za watu wenye ulemavu ambavyo vimetolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ikishirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Amesema watoto wenye ulemavu wana uwezo mkubwa ambao hautofautiani na watu wasiokuwa na ulemavu hivyo endapo watalelewa vizuri na kupata elimu stahiki wanaweza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

“Niwashukuru OSHA kwakushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kufanya ziara katika shule tatu za watoto wenye ulemavu. OSHA imekuwa ni taasisi ya faraja sana kwa watu wenye ulemavu kwani katika kile kidogo wanachokipata wameona ni vema wakashirikiana nami na Ofisi nzima ya Waziri Mkuu kuja kuwatembelea hawa watoto. Hivyo, binafsi nimefarijika sana,” amesema Naibu Waziri huyo wa Nchi anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu na kuongeza;

“Natamani kuona watu wenye ulemavu wanajumuishwa ipasavyo katika sekta zote na ndio maana nimekuwa nikipita katika maeneo mbali mbali ikiwemo ajira, elimu, afya, uchumi ili kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata nafasi katika kila fursa inayotokea na katika mipango mbali mbali ya serikali.”

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema serikali itaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo zikiwemo Taasisi, Asasi zisizo za kiserikali, makampuni na watu binafsi katika kuwawezesha watu wenye ulemavu ili nao waweze kutoa machango wao katika kuijenga nchi yao.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, ambao ndio wameandaa vifaa hivyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, amesema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taasisi yake wa kusaidia jamii kwenye sekta za elimu, afya, majanga na uboreshaji wa mazingira ya kazi.

“Sisi tumekuja katika shule hizi za watu wenye ulemavu kwa ajili ya kutoa faraja kwa wanafunzi na watumishi wenzetu ambao wanafanya kazi katika mazingira yenye changamoto nyingi na vihatarishi vingi vikiwemo vihatarishi vya kisaikolojia hivyo wanahitaji kutiwa moyo ili waendelee kuifanya kazi hii ambayo kimsingi ni kazi kubwa na muhimu sana katika maendeleo ya Taifa letu,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Aidha, wanafunzi na viongozi wa baadhi ya shule zilizopatiwa msaada wa vifaa hivyo, wameishukuru Taasisi ya OSHA kwa msaada uliotolewa na kuwaomba wadau wengine kuendelea kusaidia kutatua changamoto mbali mbali zinazozikumba shule za watoto wenye ulemavu.

“Binafsi nimefarijika sana kwasababu sikujua kuwa OSHA watakuja kwani walinipigia tu simu wakiniuliza changamoto tulizonazo hivyo namshukuru sana Naibu Waziri Ummy ambaye kwakushirikiana na OSHA wameona waje watutembelee na kutuletea zawadi. Kiukweli mahitaji waliyotuletee ni ya muhimu sana kwetu na hatujawahi kuwa nayo tangu shule hii ilipoanzishwa kwa mfano wametuletea vifaa vya kuzimia moto na kompyuta ambayo itatusaidia sana katika kuandaa mitihani ya wanafunzi,” alisema Kajika Gallan, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazinyungu.

Msaada huo wenye thamani ya takribani milioni 15 ambao ulihusisha ukaguzi wa usalama na afya hususan katika mabweni ya wanafunzi, umetolewa katika shule za za msingi za watoto wenye ulemavu za Uhuru Mchanganyiko ya Ilala-Dar es Salaam, Mazinyungu ya Kilosa-Morogoro na Buigiri ya Chamwino-Dodoma. Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa ni pamoja na; kompyuta, vifaa vya kuzimia moto, taulo za kike, vifaa kinga, vifaa vya usafi, karatasi na vibao maalum ya kuandikia watu wenye ulemavu.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda (mwenye kiremba chekundu) akishiriki zoezi la kugawa chakula kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Buigiri Wasioona, ambacho kiliandaliwa sambamba na msaada wa vifaa mbali mbali vilivyokabidhiwa katika shule hiyo na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderianaga. Viongozi hao walishiriki chakula hicho pamoja na wanafunzi, walimu na watumishi wengine wa shule hiyo.

Mkaguzi wa Usalama wa Umeme wa OSHA, Mhandisi Maria Ndaskoy, akifanya ukaguzi wa mifumo ya umeme katika bweni la shule ya Uhuru Mchanganyiko iliyoko Wilayani Ilala Mkoani Dar es Salaam wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderianaga na Mtendaj Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda kwa lengo la kutoa vifaa wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderianaga akishiriki chakula cha mchana pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Buigiri Wasioona ambacho kiliandaliwa sambamba na msaada wa vifaa mbali mbali vilivyokabidhiwa katika shule hiyo na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderianaga. Viongozi hao walishiriki chakula hicho pamoja na wanafunzi, walimu na watumishi wengine wa shule hiyo.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderianaga (watatu kushoto) na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (wapili kushoto) wakikabidhi vifaa mbalimbali vya msaada kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazinyungu ya Kilosa, Morogro, Kajika Gallan, wakati wa ziara ya kukabidhi msaada wa vifaa wezeshi kwa watoto wenye mahitaji maalum katika shule tatu za Msingi zilizopo Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.

Waziri Ummy azindua makasha ya kusambazia Kondom

$
0
0
Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu akionyesha kondom aina ya safari mara baaa ya kuitoa kwenye mashine ya kuuzia kondom kwa bei nafuu wakati wa uzinduzi wa makasha ya kondom mjini Dodoma jana. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Tayoa, Peter Masika ambaye alisema wanatarajia kusambaza makasha 80,000 nchini.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu akiwasili kwenye uzinduzi wa makasha ya kondom mjini Dodoma jana. Kulia kabisa Mkurugenzi Mkuu wa Tayoa, Peter Masika ambaye alisema wanatarajia kusambaza makasha 80,000 nchini. Mwingine ni Mbunge wa Dodoma Mjini Antony Mavunde.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu akiwa kwenye picha na viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo jijini Dodoma
Vijana wa kikundi cha ngoma cha mjini Dodoma wakitumbuiza kwenye uzinduzi wa makasha ya kusambazia kondom mjini Dodoma uliofanywa na Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu ambapo shirika la vijana Tayoa linatarajia kusambaza makasha 40,000 nchi nzima.
Mkurugenzi Mkuu wa Tayoa Peter Masika akimfafanulia jambo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu namna makasha ya kusambazia kondom yanavyofanyakazi, mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa makasha hayo jijini Dodoma.

*Aimwagia sita asasi ya Tayoa kwa ubunifu

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeshauri Shirika la Vijana Tanzania (Tayoa) kusambaza makasha ya kusambazia mipira ya kinga (kondom) na ATM za mipira hiyo kwenye halmashauri zote 184 nchini kama sehemu ya kuchochea mapambano dhidi ya Ukimwi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, amesema hayo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa makasha ya kusambazia kondom aina ya safari zinazosambazwa na Tayoa sehemu mbalimbali nchini kupitia kampuni yake ya Vijanatz Industries Ltd .

Amesema watu wengi wanaona haya kwenda kununua mipira hiyo madukani kwa hofu kuwa wataonekana wahuni hivyo ubunifu wa Tayoa utasiadia watu wengi kuwa na faragha ya kwenda kununua kinga hiyo wanapotaka kufanya mapenzi.

Amesema angependa kuona makasha hayo na ATM hizo zinasambazwa maeneo yote nchini ili watu wajihudumie wenyewe kwani kwa sasa baadhi ya watu wanashindwa kwenda kuzinunu madukani kwa hofu ya kuonekana wahuni.

“Nawapongeza Tayoa huu ni ubunifu mkubwa saba kwasababu itasaidia sana watu wengi wanunue kondom na imekuwa mbaya sana hasa kwa wasichana kwasababu wakinunua mipira hii ya kinga wanaonekana malaya, mimi nawashauri wakina dada kwamba mkishindwa kujizuia kabisa kufanya ngono ni heri kuwa na kinga kuepuka mambo mengine,” alisema Ummy

Ummy ameongeza kuwa, shirika hilo ambalo mwakani linatimiza miaka 24 halijawahi kupoteza mwelekeo wa malengo yao tangu kuanzishwa kwake kwani siku zote wamekuwa wakisimamia kupambana na ugonjwa wa Ukimwi ambao alisema bado upon a unaua watu wengi hapa nchini.

“Tayoa nawajua na tumefanyakazi nanyinyi hata kabla sijawa Naibu Waziri na baadaye Waziri, kwa muda wote niliowafahamu nyinyi mwelekeo wenu ni kupambana na ugonjwa wa Ukimwi hivyo nawapongeza kwa msimamo wenu thabiti wa kupambana na janga hili,” alisema Ummy.

Waziri Ummy aliwaomba viongozi wa serikali kwenye ngazi zote kuipa ushirikiano taasisi hiyo itakapokuwa inasambaza mipira hiyo na kuhakikisha makasha na ATM za mipira hiyo zinatunzwa kwaajili ya matumizi ya muda mrefu kwenye maeneo yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tayoa, Peter Masika alisema hadi sasa wameshasambaza makasha 40,000 katika Wilaya 169 nchini na kwamba wanatarajia kusambaza mengine 40,000 kwenye maeneo mbalimbali nchini hivyo kufikisha 80,000.

Amesema wanatarajia kuanza kusambaza mashine 5,000 za kutolea mipira hiyo (ATM) katika miaka miwili ijayo na kwamba makasha watakayosambaza yana pande mbili na yatasambazwa kwenye wilaya zote za Tanzania Bara.

Masika aliwashukuru wafadhili wa shirika hilo ambao ni Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi (Global Fund), Wizara ya Afya, Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) na Wizara ya TAMISEMI.

Amesema kwa sasa Tayoa kwa kushirikiana na AMREF wanatekeleza mradi wa Global Fund unaowalenga wasichana walio katika umri wa kubalehe na wanawake vijana katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Tanga, Singida na Geita kwani kundi hilo ndilo lililo katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU.

WATALII 700 KUTOKA ISRAEL KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII VYA TANZANIA

$
0
0

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Miyaho ametangaza kuwa, Tanzania imeanza kupokea makundi makubwa ya watalii kutoka nchi ya Israel. Ujio huu ni matokeo ya juhudi zinazofanywa na Wadau wa utalii wa Tanzania wakishirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Israel.

Jaji Mihayo ameyasema hayo wakati akiongea kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 31/7/2021 katika ofisi za TTB Makao Makuu zilizopo jijini Dar es Salaam. Jumla ya watalii 700 wanatarajia kuja Tanzania katika makundi matano tofauti na kila kundi litakuwa nchini kwa muda wa siku Saba (7).

Jaji Mihayo amesema kundi la kwanza la watalii 150 linatarajia kuwasili nchini tarehe 2/8/2021, kundi la pili litakuwa na watalii 200 litafika nchini Tanzania tarehe 9/8/2021, kundi la tatu la watalii 150 litawasili tarehe 10/8/2021 na kundi la mwisho litaingia nchini tarehe 17/8/2021, watalii hawa watatembelea vivutio vya Tanzania Bara na Visiwa vya Zanzibar.

“ Ujio wa makundi haya ya watalii ni ishara kuwa Tanzania inaaminika kuwa katika maeneo yote ya vivutio vya utalii, Watoa huduma wanazingatia vigezo vilivyowekwa na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto pamoja na Shirika la Afya Duniani za kuchukuwa tahadhali dhidi ya maambukizi ya virusi vya UVIKO -19, ambapo tunahakikisha kwamba Watalii wanapokuja Tanzania wanatembelea vivutio vyetu na wanarudi nchini kwao wakiwa salama”

Aidha, “Tunaupongeza Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa kushirikiana na kampuni ya utalii ya Excellent Guide, Tours and Safaris kufanikisha kuleta makundi haya makubwa ya watalii. TTB inaendelea kushirikiana na Ofisi za Balozi za Tanzania zilizopo katika nchi mbalimbali duniani na Wadau wa utalii wa Tanzania kushwishi mawakala wakubwa kuleta watalii Tanzania”. alisema Jaji Mihayo.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2019 Tanzania ilipokea watalii 16,348 kutoka Israel, mwaka 2020 idadi ya watalii imeshuka kutokana janga la UVIKO-19 na kufikia 6,889.

TUSIPOJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA UVIKO-19 SASA,TUTAKUJA KULIA-RC IBUGE

$
0
0

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameendelea kuwatahadharisha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kujikinga na virusi  vya corona(UVIKO 19) kwa  kutumia njia zinazotolewa na wataalam wa afya ili kupunguza maambukizi.

RC Ibuge ametoa tahadhari hiyo wakati anazungumza na wananchi kwenye kilele cha tamasha la Majimaji Selebuka ambalo lilifanyika kwa siku nane ndani ya uwanja wa Majimaji mjini Songea.

“Suala la maambukizi kama hatutasisitiza kujikinga sasa tutakuja tulie’’alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Amesema  ukanda wote wa kusini ikiwemo Mkoa wa Ruvuma upo katika tishio la UVIKO 19 kwa sababu serikali  imeboresha miundombinu ya barabara hivyo Mkoa wa Ruvuma na ukanda wa kusini unafikika kwa siku moja.

Amesema katika mji  wa Songea kuna usafiri wa anga siku za Jumapili na Jumatano hivyo mtu anaweza kusafiri kwa saa moja na nusu toka Dar es salaam na kuingia mkoani Ruvuma hivyo ametoa rai kuzingatia maelekezo yote yanayotolewa na wataalam wa afya kuzuia maambukizi mapya.

Amesema kuanzia sasa matamasha na mikusanyiko isiyokuwa na umuhimu  haitafanyika,hata hivyo amesisitiza  mikusanyiko na matamasha yatafanyika kwa kibali maalum cha mamlaka mahalia baada ya kujiridhisha endapo taratibu za kujikinga zimefuatwa.

 Amewakumbusha wananchi kuendelea kunawa kwa kutumia maji tiririka na sabuni,kutumia barakoa na elimu endelevu  dhidi ya corona ambayo itajenga uelewa kuondoa hofu kwa wananchi hivyo kuwaondoa hofu na kutojifungia ndani badala yake kuendelea kuchapa kazi kwa kujikinga.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ligunga wilayani Tunduru kuhusu kujikinga na maambukizi ya KOVID 19 alipofanya ziara ya kikazi hivi karibuni

ZIARA YA MHESHIMIWA WAZIRI MKUU MKOANI MBEYA

$
0
0



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya, Agosti 1, 2021. Wengine pichani kutoka kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako na kulia ni Mbunge wa Busokelo, Atupele Mwakibete. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na aliyekuwa Waziri katika serikali ya Awamu ya Nne, Profesa Mark Mwandosya (kulia) na mkewe Lucy Mwandosya (wa pili kulia) wakati alipowasili kwenye viwanja vya Chuo cha Ufundi cha wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya kuzindua Chuo hicho, Agosti 1, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Agosti 1, 2021 amekabidhiwa zawadi ya picha aliyopiga akivuka mto Rufiji kwa kutumia ngalawa mwaka 2010 akiwa Mkuu wa wilaya ya Rufiji wakati alipompokea Profesa Mark Mwandosya aliyekuwa ni Waziri katika serikali ya Awamu ya Nne. Picha hiyo ilikabidhiwa kwake na Profesa Mwandosya (kushoto) na mkewe Lucy Mwandosya (wa pili kushoto) baada ya Mheshimiwa Majaliwa kuzindua Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazma kaunda suti wakati alipotembelea darasa la mafunzo ya ushonaji nguo katika Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya, Agosti 1, 2021. Kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

UFUNGAJI WA MAFUNZO YA NDOA MKUPUO WA KUMI.

$
0
0




Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Abdalla Hussein Kombo akimkabidhi Zawadi Shekh Thabit Noman Jongo kutoka kwa Wanafunzi waliohitimu mafunzo ya ndoa mkupuo wa kumi hafla iliyofanyika Msikiti wa Jaamiu Zinjibar uliopo Kiembe Samaki Mjini Zanzibar.

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Abdalla Hussein Kombo akimkabidhi Cheti cha Mafunzo ya ndoa Abdalla Khamis katika hafla ya Ufungaji wa mafunzo hayo yaliyofanyika Msikiti wa Jaamiu Zinjibar Kiembe Samaki Wilaya ya Magharib ‘B’.

Katibu wa Mufti Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume akiwasisitiza Washiriki waliyohitimu Mafunzo ya Ndoa kuitumia elimu walioipata katika Ufungaji wa mafunzo hayo huko Msikiti wa Jaamiu Zinjibar uliopo Kiembe Samaki Mjini Zanzibar .

Baadhi ya Washiriki waliohitimu mafunzo ya ndoa wakiwa katika Ufungaji wa mafunzo hayo yaliyofanyika Msikiti wa Jaamiu Zinjibar Kiembe Samaki Mkoa wa Mjini Magharibi.



Muhitimu wa Mafunzo ya Ndoa Msanif Mohamed Msanif akitoa neno la shukurani kwa Viongozi waliyowezesha mafunzo hayo wakati wa ufungaji wa mafunzo ya ndoa huko Msikiti wa Jaamiu Zinjibar Kiembe Samaki Mkoa wa Mjini Magharibi.

Picha Na Maryam Kidiko- Maelezo Zanzibar.

*****************************

Na Khadija Khamis – Maelezo. 01/08/2021 .

Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Mheshimiwa Abdalla Husein Kombo amewataka wahitimu wa mafunzo ya ndoa kuitumia elimu hiyo kwa kujenga subira na uvumilivu ili kudumisha ndoa zao .

Hayo ameyasema katika Ukumbi wa Msikiti wa Jaamiu Zinjibar Mazizini wakati akikabidhi vyeti kwa Wahitimu wa Mkupuo wa kumi wa mafunzo ya ndoa.

Alisema lengo la kupatiwa mafunzo hayo kwa wanandoa ni kuwa walimu kwa wengine na kujenga imani subira na uvumilivu katika ndoa zao .

“Dawa pekee ya kudumisha ndoa ni kuwa na subira hasa kwa wanaume ingawa changamoto kubwa ni akinamama kukosa uvumilivu katika ndoa”alisema Waziri Kombo.

Aidha alisema katika dini ya kiislamu imetoa miongozo mbali mbali ya kisheria kwa lengo ya kuitunza ndoa na kuipa hadhi na heshima yake kwa kubainisha haki na wajibu kwa wanandoa.

Nae Katibu wa Mufti Shekhe Khalid Ali Mfaume amesema ameridhishwa na muamko wa wanafunzi wanaohitaji elimu ya ndoa jambo ambalo litasaidia kuepusha wimbi la talaka nchini.

Amesema mafunzo mbalimbali waliyoyapata wahitimu hao ni pamoja na maana ya ndoa kisheria, uchaguzi wa mchumba katika uislamu nafasi ya wazazi kwa wanandoa pamoja na sifa za familia ya kiislamu .

Alifahamisha kuwa licha ya mafunzo hayo wahitimu hao amefahamishwa viashiria vya migogoro katika ndoa na matokeo ya migogoro hiyo.

Nao wahitimu hao wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Mufti kwa kuwapatia mafunzo hayo bila ya malipo.

Walisema kuwa wataitumia elimu hiyo waliyoipata kwa vitendo kwa kujenga amani upendo na utulivu ili kudumisha ndoa zao na kupata familia bora.

Mafunzo hayo ni ya Mkupuo wa kumi yalifanyika kwa wiki kumi na kujumuisha Jumla ya Wanafunzi 195 Wakike na Wakiume

RC SINGIDA AHIMIZA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI KUPATA CHANJO YA CORONA

$
0
0

Kaimu Afisa Tarafa ya Ikungi Yahaya Njiku akizungumza kwa niaba ya Mkuu  wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hadhara Tukufu ya Mazazi ya Mtume Mohammad (S.AW) iliyofanyika Issuna  Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana ambayo iliandaliwa na  Jumuiya ya Kinamama wa kiislamu wilayani humo (JUWAKITA)

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, akizungumza na Waislamu mkoani hapa kupitia hadhara hiyo.
Katibu Mkuu Baraza Kuu la Waisalamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida Sheikh Burhan Mlau, akizungumza kwenye hadhara hiyo.
Shekhat wa Mkoa wa Singida Zeana Salum, akizungumza kwenye hadhara hiyo
 Hadhara hiyo ikiendelea.
Viongozi wakiwa meza kuu.
Kaimu Afisa Tarafa ya Ikungi Yahaya Njiku, akiteta jambo na Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro  kwenye hadhara hiyo.

Mdau Shabani Mukee (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu Baraza Kuu la Waisalamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida Sheikh Burhan kwenye hadhara hiyo.



Na Dotto Mwaibale, Ikungi


MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge amewaomba wananchi mkoani hapa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya kujikinga na janga la wimbi la tatu la ugonjwa wa virusi vya Corona.

Ombi hilo limetolewa na Kaimu Afisa Tarafa ya Ikungi Yahaya Njiku kwa niaba ya Dkt.Mahenge ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hadhara Tukufu ya Mazazi ya Mtume Mohammad (S.AW) iliyofanyika Issuna  Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana ambayo iliandaliwa na  Jumuiya ya Kinamama wa kiislamu wilayani humo (JUWAKITA)

"Tumuunge mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kujitokeza kupata chanjo hiyo ambayo aliizindua kwa kuchanjwa na kufuatiwa na viongozi wengine mbalimbali ambapo hapa mkoani kwetu itaanza kutolewa wakati wowote katika vituo vilivyoainishwa kwenye wilaya zote,". alisema Njiku.

Akizungumza na wakina mama hao Njiku alisisitiza kuzidi kuwa wacha Mungu na kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali ili waweze kuinuka kiuchumi bila kusahau kuvaa mavazi ya stara ya kiislamu.

Aidha Njiku aliwahimiza wakina mama hao kuishi vizuri na waume zao na kuzingatia haki za ndoa na kutunza familia zao.

Njiku alipongeza ushirikiano uliopo baina ya Serikali na taasisi za dini jambo lililosaidia kuimarisha amani na mshikamano kwa wananchi kote nchini.

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro amewaomba waislamu mkoani hapa kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa wa corona hasa huu wa wimbi la tatu ambao umeelezwa kuwa ni mkali kuliko wa awamu ya kwanza na wa pili.

Nassoro aliwataka waislamu kuendelea kumuomba Mungu kuwaepusha na ugonjwa huo na kueleza wasifanye mzaha katika jambo hilo.

Alisema Tanzania bado tuna fursa kubwa kutokana na kutokuwepo kwa zuio la kutotoka nje kutokana na janga ili la Corona kama ilivyo nchi zingine ambazo wananchi wake wanashindwa hata kwenda kuswali.

Shekhat wa Mkoa wa Singida Zeana Salum alisema jumuiya hiyo ya akina mama katika  wilaya hiyo imejiwekea mikakati ya kutembelea kata zote 28 na kuwa hadi sasa wametembelea kata 18 huku wakihamasisha kuwepo kwa madrasa za akina mama na watoto katika kila msikiti.

Katika hadhara hiyo walifanya harambee ili kupata fedha za kujenga ofisi yao ya wilaya ambapo walimuomba mkuu wa mkoa awasaidie ambapo mahitaji ya kukamilisha ujenzi huo  ni Sh.19,675,000. 


Benki ya NMB yaendelea kuongoza kwa faida na ufanisi katika sekta ya kibenki Tanzania

$
0
0

 



Benki inayoongoza nchini Tanzania, NMB, imeendeleza ufanisi wake kiutendaji katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2021.  Faida baada ya kodi ya mapato imeongezeka kwa asilimia 43 na kufikia shilingi bilioni 134 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 94 ya kipindi kilichoishia June 2020. Ufanisi huu mkubwa umetokana na ongezeko la biashara na miamala, udhibiti wa gharama za uendeshaji na ubora wa mikopo inayotolewa.

Mapato ya Benki yameongezeka kwa asilimia 20 hadi kufikia shilingi bilioni 463 katika kipindi kilichomalizikia mwezi Juni 2021 ikilinganishwa na shilingi bilioni 387 zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka jana. Mapato haya yamechangiwa na ongezeko la mikopo kwa wateja na uwekezaji kwenye hati fungani za Serikali.

Vilevile mapato yasiyotokana na riba yameongezeka kwa asilimia 17 hadi kufikia shilingi bilioni 140 ikilinganishwa na shilingi 119 ya kipindi kama hicho mwaka 2020. Ongezeko la mapato yasiyo ya riba yalichangiwa na ongezeko la miamala ya kibenki kutokana na hudumu nzuri zinazotolewa na benki, mahusiano mazuri na wateja, na uwekezaji katika mifumo ya kidigitali.

Pia benki ya NMB imeendeleza ufanisi bora wa kiuendeshaji, sanjari na malengo makuu ya kimkakati pamoja na viwango elekezi vya ufanisi vilivyowekwa na msimamizi wa mabenki, yaani Benki Kuu ya Tanzania.  Katika kipindi hiki cha nusu ya kwanza mwaka 2021, uwiano wa matumizi yasiyo ya riba na mapato halisi umeimarika mpaka asilimia 47, kutoka asilimia 56 katika kipindi kama hiki mwaka jana. Uwiano huu wa asilimia 47, uko ndani ya kiwango cha juu cha asilimia 55 kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Benki itaendelea kutilia mkazo uimarishaji wa ufanisi huku ikiboresha sana uwekezaji katika teknolojia na vipaumbele vya kimkakati ili kuendeleza utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Pia katika kipindi hiki cha nusu ya mwaka 2021, ubora wa mali za NMB uliimarika kutokana na mikakati thabiti ya kuimarisha mikopo ya benki. Katika kipindi hiki, uwiano wa mikopo chechefu uliimarika hadi asilimia 4.3 kutoka asilimia 6.9 katika kipindi kama hiki mwaka jana, ikiwa ndani ya kiwango cha juu ya asilimia 5 kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Benki ya NMB imeendelea kuimarisha mizania yake ikiwa na ukuaji endelevu hivyo kuonesha kwa jinsi gani benki imeweka misingi bora na imara ya uhusiano wake na wateja. Mikopo ilikuwa kwa asilimia 11 hadi kufikia shilingi trilioni 4.2 kufikia mwisho wa mwezi Juni 2021 ukilinganisha na shilingi trilioni 4 katika kipindi kama hiki mwaka jana.

Amana za wateja zilikua kwa asilimia 8 hadi kufikia shilingi trilioni 5.8 ikilinganishwa na shilingi trilioni 5.5 katika kipindi kama hiki mwaka jana, hii ikionesha mazingira mazuri yaliyowekwa na benki katika uhusiano wake na wateja. Katika kipindi hiki mali za benki zimeongezeka kwa asilimia 6 hadi kufikia shilingi trilioni 7.6 ukilinganisha na shilingi trilioni 7.2 katika kipindi kama hiki mwaka jana.

Akizungumzia mafanikio haya makubwa yaliyopatikana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema, “Tunajivunia ufanisi bora na uimara wa benki yetu ya NMB. Mafanikio haya makubwa ya nusu ya mwaka 2021 ni kielelezo cha imani kubwa ya wananchi na wateja kwa benki yao ya NMB, ufanisi wa wafanyakazi wa benki ya NMB, utekelezaji bora na usimamizi mzuri wa mpango mkakati wa benki”.  

Aliongeza kusema kuwa, “Tunazidi kujikita katika misingi imara ambayo tumeshaijenga ikiwa ni pamoja na mizania bora ya benki, mtaji mkubwa, matawi mengi, uwezo mkubwa kidijitali, na wafanyakazi bora ili kuweza kusukuma mbele biashara yetu ya benki.

Tukiangalia mbele tunahamasika tukiona  fursa mbalimbali zilizo mbele yetu kutokana na kuzidi kuimarika kwa uchumi wa dunia hasa baada ya madhara makubwa yaliyosababishwa na ugonjwa wa UVIKO-19 pamoja na hatua stahiki zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kuimarisha sekta ya kibenki”.

Aidha, bi Ruth alimalizia kwa kusema “Tutaendelea kuweka mkazo katika kuwahudumia wateja wetu kwa ufanisi na kutoa huduma bora ili kuhakikisha benki inaendelea  kuleta mafanikio kwa wawekezaji wake na pia kuwajibika katika jamii inayotuzunguka.

Newz Alert: Rais Samia afanya uteuzi wa Wakurugenzi Watendaji

$
0
0

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassani






 

MAJALIWA ATEMBELEA SHAMBA LA COCOA KYELA

$
0
0


  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama cocoa wakati alipotembelea shamba la Bw. Elias Mwirubi katika kijiji cha Ipinda wilayani Kyela, Agosti 1, 2021. Wa tatu kulia ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

BILIONI 71.9 KUTEKELEZA REA III MZUNGUKO WA PILI RUVUMA, MRADI WAZINDULIWA TUNDURU

$
0
0



Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani(tatu kushoto) akiweka Jiwe la Msingi katika Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakati akizindua Mradi wa usambazaji Umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa Mkoa huo, uliofanyika wilayani humo, Agosti 01, 2021.



Waziri wa Nishati, Dkt, Medard Kalemani (kushoto) akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakati akizindua mradi wa usambazaji umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa mkoa huo uliofanyika wilyani humo, Agosti 01, 2021.



Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakifurahia jambo, wakati Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) akizungumza kabla ya kuzindua Mradi wa usambazaji Umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa Mkoa huo uliofanyika wilayani humo, Agosti 01, 2021.



Baadhi wa Vijana wa Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani)wakati akizindua Mradi wa usambazaji Umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa mkoa wa Ruvuma uliofanyika wilayani humo, Agosti 01, 2021.


Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani)wakati akizindua Mradi wa usambazaji Umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa Mkoani humo uliofanyika wilayani humo, Agosti 01, 2021.



Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Balozi Brigedia Generali Wilbert Ibuge (kulia) akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakati wa uzinduzi wa Mradi wa usambazaji Umeme Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili kwa mkoa wa Ruvuma uliofanyika wilayani humo, Agosti 01, 2021.
***************************

Na Zuena Msuya, Ruvuma

Imeelezwa kuwa shilingi Bilioni 71.95 zitatumika kutekeleza mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), Mzunguko wa Pili katika vijiji vyote ambavyo havijapekelewa umeme mkoani Ruvuma.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani wakati akizindua mradi huo kwa Mkoa wa Ruvuma,ambapo uzinduzi huo ulifanyika katika Kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mkoani humo Agosti 01, 2021.

Dkt. Kalemani alisema kuwa fedha hizo zitatumika kufikisha na kusambaza umeme katika Vijiji 265 vilivyobakia katika mkoa huo wenye jumla ya vijiji 554, ambapo tayari vijiji 289 vimeshafikiwa na umeme.

“Wanaruvuma hasa Tunduru tulipozindua mradi huu hakikisheni mnautumia umeme huu ipasavyo kwa kujiletea maendeleo pia anzisheni viwanda, Rais wa awamu ya Sita, Samia Suluhu Hasan ametoa fedha za kutosha kuhakikisha vijijini vyote vinapata umeme ifikapo Desemba 2022, sasa kazi kwenu kuandaa nyumba zenu na kwa sasa umeme ni lazima sababu Serikali imegharamia kila kitu, ninyi mtalipia shilingi 27,000 tu, hivyo msichezee nafasi hii, pia ni marufuku kununua nguzo” alisema Dkt. Kalemani.

Alifafanua kuwa kampuni mbili za kitanzania zimepewa dhamana ya kutekeleza mradi huo katika wilaya zote za mkoa husika ambazo ni Songea, Mbinga, Tunduru, Nyasa na Namtumbo,ambapo kazi hiyo imegawanywa katika makundi mawili.

Wakandarasi hao ni Kampuni ya NAMIS itayotekeleza mradi huo katika Wilaya za Songea, Mbinga na Nyasa kwa gharama ya TZS. Bilioni 35.281, na White City itatekeleza katika Wilaya za Tunduru na Namtumbo kwa gharama ya Bilioni 36.678.

Akizungumzia wilaya ya Tunduru ambapo ndipo mradi huo umezinduliwa kimkoa, Dkt. Kalemani alisema kuwa wilaya hiyo ina jumla ya vijiji 157, kati ya hivyo vijiji vyenye umeme ni 72 na visivyo na umeme ni 85.

Vijiji hivyo 85 vilivyosalia vitapelekewa umeme kupitia mradi huo uliozindiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 21.7 ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 12.

Kwa wilaya hiyo ya umeme utaanza kupelekwa katika kata ya Nalasi ikihusisa vijiji,vitongoji na mitaa vyote vya kata hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Balozi Brigedia Generali Wilbert Ibuge aliwataka wakazi wa mkoa huo kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme pamoja na kutoa ushirikiano kwa wakandarasi watakaotekeleza mradi huo.

Balozi Ibuge aliwataka vijana wa maeneo husika kuchangamkia fursa ya kufanya kazi zisizo na taaluma maalum, ili kuweza kujipatia kipato na kunufaika na mradi huo.

Hata hivyo aliwataka wakandasi waliopewa dhamana ya kutekeleza mradi hou kujitambulisha katika ofisi za serikali za mitaa, wakati wa kutekeleza miradi hiyo ili kupata ushirikiano zaidi na kurahisisha utendaji kazi wao.

WAZIRI MKUU ATOA RAI KWA WALIOPATA UFADHILI WA MAFUNZO YA UFUNDI

$
0
0

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana waliopata ufadhili wa Serikali kupitia programu maalumu ya kupata mafunzo ya ufundi stadi watumie vizuri fursa hiyo ili wanufaike.

 Amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fungu la fedha kwa ajili ya kuwasomesha vijana katika fani mbalimbali za ufundi stadi kwa muda wa miezi sita.

 Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumapili, Agosti 1, 2021) wakati wa uzinduzi wa chuo cha Ufundi Stadi kilichopo katika kijiji cha Kipapa kata ya Lufilyo wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya.

 “Kilichotuleta hapa ni kuja kushuhudia vijana wetu wa Kitanzania ambao wameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuwapatia ujuzi ili wakaendeleze kazi hizo.”

 Amesema Tanzania nzima kuna vijana takribani 45,000 ambao wamesambazwa katika vyuo vyote vya Serikali na vya binafsi ambapo watapatiwa mafunzo ya ufundi stadi kwa miezi sita.

 Waziri Mkuu amesema mbali na kupatiwa ujunzi katika vyuo hivyo pia vijana wengine wamepelekwa kwenye maeneo ya kutolea huduma kama za utalii, hoteli ili wapate ujuzi.

 Amesema chuo hicho cha VETA Busokelo ni kimojawapo kati ya vyuo walivyovichagua ili kipokee vijana wa maeneo ya wilaya za Rungwe, Kyela, Chunya na Mbeya ili kuwapa ujuzi.

 “Matarajio yangu vijana wote waliopata nafasi hii hawataipoteza, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anatamani kuona kila Mtanzania akijishughulisha na shughuli za ujasiriamali.”

 Amesema mkakati wa Serikali kwa mwaka 2021 ni kusomesha vijana 80,000 ambapo asilimia 60 ya mafunzo hayo watayapata kwa vitendo na asilimia 40 watafundishwa darasani.

 Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema chuo cha Ufundi Stadi cha Busokelo kimedahili wanafunzi 127 ambao watapa mafunzo ya ufundi kupitia program hiyo.

 Alisema kati ya wanafunzi hao 26 wanasomea ufundi seremala, 45 ushonaji nguo, 28 umeme wa majumbani, 18 ukarabati wa vitarakimishi na 10 utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki.

 Alisema mafanikio ya programu hiyo ni pamoja na kuwawezesha wanafunzi waliopata ujuzi kuweza kujiajiri katika fani za useremala, ushonaji, udereva na matumizi ya vitarakinishi.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya, Agosti 1, 2021. Wengine pichani kutoka kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako na kulia ni Mbunge wa Busokelo, Atupele Mwakibete. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Viewing all 118915 articles
Browse latest View live


<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>