Na Bashir Yakub
MAKALA haya yataeleza tofauti kati ya kibarua na ajira ili isiwe unaitwa kibarua kumbe kisheria umeajiriwa na unastahili stahiki zote za kiajira.
Wako watu wengi wanafanya kazi lakini hawajui wanafanya kazi katika mwavuli upiyawezekana mtu akawa amefanya kazi miaka mingi lakini bado kazi anayofanya haitambuliki anaifanya kama nani.
Na mara nyingi hii hujitokeza katika kazi zile ambazo si za kitaaluma,Kazi zisizo za kitaaluma ni kama kufanya kazi za ndani, kusaidia mashambani, kusaidia katika ujenzi na nyingine zinazofanana na hizo.
Lakini pia siku hizi kutokana na ongezeko la ukosefu wa ajira hata kazi ambazo ni za kitaaluma nazo zimekumbwa na janga hili.
Kwa sasa katika ofisi nyingi wapo watu wanafanya kazi za kitaaluma lakini haijulikani kama wameajiriwa au ni vibarua.
Wapo watu wamekaa maofisini hata miaka mingi wakiitwa wafanya mazoezi ( intern) Wapo wahasibu, madaktari, walimu, wachumi, na wengine wengi.
Waajiri hupenda sana hali hii kwakuwa huwapatia faida kubwa, Kwanza huwalipa kiduchu watu hawa lakini pili hukwepa kulipa stahiki zao nyingine za kiajira kama malipo ya muda wa ziada,matibabu, likizo, kuumia kazini na stahiki nyinginezo.
1.NINI MAANA YA AJIRA.
Ajira ni mahusiano ya kikazi kati ya mwenye kazi na mfanyakazi ambapo mwenyekazi huwa na mamlaka ya kutawala, kudhibiti, na kuelekeza namna , jinsi, na wakati gani kazi husika ifanyike.
Wako watu wanafikiria na kujua kuwa ili kazi iitwe ajira ni lazima yawepo maandishi ya kimkataba, hapana hili si lazima, muhimu ni kama inavyoelekezwa katika tafsiri hapo juu.
Hii ina maana ili kazi iitwe ajira vipo vigezo vinavyozingatiwa na hasa hivyo nilivyotaja kwenye tafsiri, kimsingi yapo mambo matano ambayo yakitokea kazi yoyote unayofanya itaitwa ajira na utastahili kupata haki zote za kiajira kama muajiriwa, tutaona mambo hayo hapa chini.
2. JE WE NI KIBARUA AU MUAJIRIWA.
Yapo mambo matano yatakayokujulisha kuwa we si kibarua bali ni muajiriwa.
( a ) Kwanza ikiwa una mkataba maalum unaoeleza aina kazi unayofanya, sehemu ya kazi, pesa unazolipwa, , muda wa kazi, likizo na mengine usiambiwe wewe ni kibarua.
Makubaliano ya kimaandishi ya namna hii yanakupa hadhi ya muajiriwa na unastahiki haki zote za muajiriwa kwakuwa we utakuwa ni muajiriwa na si kubarua.
( b ) Pili ikiwa vitendea kazi unavyotumia vinamilikiwa na mwenye kazi, mfano we ni dereva na gari si la kwako ni la tajiri, unafanya usafi lakini vifaa vyote vya usafi ni vya tajiri, unafanya kazi za ndani na kila kitu ndani ni cha tajiri. Basi ikiwa hilo liko hivyo ni kigezo kuwa hiyo ni ajira na si kibarua.
( c ) Tatu ikiwa mamlaka ya kuamua kazi ifanyike vipi, kwa namna gani na kwa wakati gani anayo yule aliyekupa kazi basi nacho ni kipimo kuwa hiyo ni ajira. Kwa mfano bosi na sekretari wake. Kwakuwa bosi ndiye huagiza kazi ifanyike vipi, kwa namna gani n.k bosi huyo hawezi kusema kuwa hajamuajiri huyo sekretari. Hii ni tofauti na pale unapomleta fundi ujenzi nyumbani. Utamuonesha kazi lakini hutakuwa na uwezo wa kumuelekeza afanyeje kazi kwakuwa yeye ndiye fundi na anajua namna ya kufanya kazi yake.
( d ) Nne suala la nani anawajibika na hasara inapotokea nalo ni kipimo iwapo umeajiriwa au ni kibarua. Kwa mfano ukimkodisha dereva hata kwa miaka miwili ikiwa kila gari linapoharibika au kupata ajali hutengeneza yeye hawezi kusema umemuajiri, lakini ikiwa utatengeneza wewe unayemkodi dereva basi itakuwa ni kipimo kuwa yupo katika ajira.
( e ) Tano ni faida. Nani hunufaika na faida nacho ni kipimo ikiwa umeajiriwa au ni kibarua.
Haya ndiyo mambo makuu yatakayokuashiria ikiwa umeajiriwa au unafanya kibarua na si mengineyo.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com