Charles James
USIKU flani wa zamani. Usiku wa Ulaya katika dimba la Stanford Bridge. Ronaldinho Gaucho alikua akiionesha Dunia maajabu yake.
Machi 7 mwaka 2005. Chelsea ya Mropokaji Jose Mourinho walikua wakiikaribisha Barcelona ya Frank Rjikaard katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa.
Dakika ya 38 ya mchezo, Chelsea wakiwa wanaongoza 3-1 ndipo Gaucho alipotuonesha uchawi wake.Anapokea pasi kisha kwa maringo makubwa huku Ricardo Carvalho, John Terry wakimuangalia anaanza kucheza ‘sankoro’ kabla hajapasia mpira wavuni.
Licha ya Chelsea kushinda 4-2 goli lile la Gaucho linabakia kuwa miongoni mwa magoli bora ya muda wote kwenye michuano ya Ulaya.
Tusogee hapa: Zinedine Zidane Yazid, alikua bora hewani na miguuni, aliuchezea mpira alivotaka.
Alijawa na kiburi cha miguu kilchotawaliwa na ubabe wake dimbani, Zidane aliujua mpira bwana. Ballon d'Or tatu ziko kabatini kwake.Alichowafanya wa-Brazil wedi kapu ya 1998 wanabaki kusimualiana wenyewe kwa wenyewe.
Goli mbili za dhahabu ziliwapa ubingwa Ufaransa mbele ya wanamajinuni wa Kibrazil. Zidane alikua fundi wa ukweli.Zimeenda wapi faulo za kidigitali katika zama za Analojia kutoka kwa Samba Boy, Juninho Pernambucano?
Juninho anatajwa kuwa mkali wa mipira iliyokufa ‘free kick’ kuwahi kutokea Duniani. Leo hii mchezaji akifunga goli la faulo inakua gumzo.David Beckham kuna nyakati aliweza kupiga kona ikaenda moja kwa moja nyavuni.
Una muda gani hujaona ajabu kama hilo? Najua utaniletea kumbukumbu ya Shiza Kichuya dhidi ya Yanga. Achana na hizo stori wewe.Shiza aliotea tu. Ukitaka kuamini ni bahati hajawahi kurudia tena. Haikua mikato yake.
Ebwana umaridadi wa Ronaldo de Lima mbele ya lango la adui umekwenda wapi siku hizi?Mbona Dunia haina tena washambuliaji wa aina yake? Tumepoteza wanaume wenye uwezo wa kufunga na miguu yote miwili na mwenye matumizi mujarabu kichwani.
De Lima hajawahi kuwa na mfanano wake, tunammiss na tunapoelekea tunapoteza watu hodari mbele ya maadui.Nani hakumbuki goli tatu za kitemi alizomtungua Fabian Barthez na Manchester United yake pale Old Trafford?
Wakati anatolewa wahuni wa Kiingereza wakasimama kumpigia makofi mtu aliewachapa tatu mzuka.Ni kitambo kirefu sijashuhudia tukio kama hilo katika ardhi ya Malkia Elizabeth. Tukio la heshima mbele ya Mshambuliaji wa kifahari.
Temana na Ronaldo. Kisanga cha Philipo ‘Pippo’ Inzaghi, Rud Van Nestorooy hakikua na mfanano wake.Mbobezi Alex Ferguson aliwahi kunukuliwa akisema “ Pippo amezaliwa kuwa mviziaji”.
Hawa ni washambuliaji waliopachikwa jina la ‘poacher’ walifunga magoli ya ajabu katika mazingira magumu ambayo wangewaacha mabeki wa Timu pinzani wakinyoosha mikono juu kuomba ‘offside’.
Dunia ya sasa haiwataki tena waviziaji, watu wanaosubiri mjisahau wawape adhabu ya kifo.Haishangazi tunapomuona Lukaku akionekana bora mbele ya mhafidhina Javier Hernandez Chicharito.
Makocha wengi wanapenda washambuliaji viungo, Bobby Firmino anamfanya Klopp asifikirie kusajili namba Tisa pale Liverpool. Maajabu haya.
Ghafla nimezikumbuka bangi za waapolo Roy Keane na Patrick Vieira. Dunia ilisimama kila Man U walipovaana na Arsenal.Ubabe ulitamalaki katikati, ngumi, karate na Judo zilihusika, viatu vilichapwa kisawa-sawa.
Leo hii pale Arsenal kuna Mateo Gundeouzi, United kuna Fred hakuna hata ishu. Soka limeenda wapi jameni?Gennaro Gattuso angeweza kumchapa mtu vibao uwanjani bila sababu yoyote. Ubabe tu ubayani ubayani. Mambo mbaya.
Kulikua na refa anaitwa Corina huyu alikua mbabe wa watukutu kama Keane na Gattuso.Sura yake mpalazo, macho yake ya Paka na kipara chake kichwani viliwatisha hata wale wachezaji waliojiona wababe.
Eti Martin Athkson leo ndo tunamuona bora na wa mechi ngumu. Futbol imepoteza mvuto.Diego Maradon alikua bora sana, kijitu kifupi hivi, chenye nguvu kuanzia juu hadi chini. Mfalme wa chenga za maudhi haswa.
Goli lake la mkono dhidi ya Waingereza mwaka 1986 linabaki katika historia ya Dunia. Siyo refa wala lezman ambaye aliona Diego ameshika ule mpira. Ladha ya soka ilionekana. Ule ubishi wa alishika au hakushika ulikuepo.
Leo tuna ‘goal technology na VAR, hakuna mikwaruzano ya vibandani ‘lile siyo goli, ni goli mara aliotea yule’. Soka limekua la kisayansi sana. Inatukera sisi.
Hebu nambieni hamjamiss Higuanita? Yule Golikipa ambaye angeruka sarakasi kabla hajadaka mpira. Kipindi flani Juma Kaseja alifanya hii michezo.
Upiganaji wa kutokata tamaa kutoka kwa Liverpool je? Hawa jamaa ungewafunga tatu bila lakini bado wangepambana kuhakikisha wanarudisha magoli yote.
Fainali yao ya UEFA na AC Milan 2005 na ile ya FA na West Ham 2006 zinabaki kuwa kielelezo chao angalau mchezo wa pili wa nusu fainali dhidi ya Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa msimu ulioisha walitukumbusha sifa yao.
Wapi mchuano wa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Dunia? Eti siku hizi ni rahisi kutabiri kwamba asipobeba Lionel Messi atatwaa Cristiano Ronaldo, huyu Modric kaokota dodo tu.
Miaka 10 wanapokezana wenyewe kwa wenyewe. Fikiria wakati Luis Figo anashinda mwaka 2000 Ballon d'Or washindani wake walikua Zidane, Raul Gonzalez.
Pavel Nedved anashinda 2003 akiwapiku akina Lampard, Gaucho. Ushindani ulikuepo bwana.Messi na Ronaldo unafikiri wangeshinda vipi mfululizo kama wangekutana na akina Nesta, Gattuso, Keane au Hierro dimbani?
Wangeshinda vipi mara tano mfululizo mbele ya uchawi wa Gaucho, De Lima, Nedved au Thienry Henry?
Wanangu wa Chelsea mnaangaika baada ya Eden Hazard kuondoka hamjamiss ile Zola Zone ya Giafranco Zola? Wenyewe wataliano waliita Traquartista.
Bwana ee nyakati zime-expire soka limebadilika ladha haipo kama zamani sasa kuna biashara tu.
Ngoja nikalale napoona nafasi ya Rashid Yekin anacheza Iwobi pale Nigeria, siyaoni matege ya Mohammed Aboutrika kule Misri.
Kwamba Afrika imeshindwa kuzalisha George Weah mwingine wa kuwapa homa Wazungu? Ujuha huu. Afrika haina Jay Jay Okocha tena. Tumebaki kujisifia na Pierre Aubameyang.
Uko wapi Ukompyuta wa Sunday Manara katika ubongo wa Ibrahim Ajib Migomba? ‘Football is Dead’
0683 015145