Quantcast
Channel: MICHUZI BLOG
Viewing all 110173 articles
Browse latest View live

KITAMBULISHO CHA TAIFA NA CHA KUPIGIA KURA HAVITAHUSIKA KUPIGIA KURA NOVEMBA 24 - RC NDIKILO

$
0
0
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI

SERIKALI Mkoani Pwani, imetoa rai kwa wananchi kupuuza baadhi ya watu wanaowahadaa kuwa kitambulisho cha Taifa -NIDA na cha kupiga kura wataweza kupigia kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji Novemba 24 mwaka huu, suala ambalo ni upotodhaji mkubwa.

Aidha imeweka bayana takriban watu 680,000 wanatarajiwa kujiandikisha kwenye daftari hilo, hivyo wamehamasishwa kujiandikisha ili kuwa na haki ya kupiga kura kuchagua viongozi wanaowataka.

Akihamasisha umuhimu wa kujiandikisha katika daftari hilo hadi octoba 14 mwaka huu ,wakati alipokwenda kutimiza haki yake ya msingi kujiandikisha kituo cha Mwanalugali 'A ' Kibaha ,mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alisema kitambulisho cha Taifa na cha kupigia kura havitahusika katika zoezi la kupiga kura.

"Nimetumia haki yangu ya msingi kujiandikisha ,nimejiandikisha wa 123  lengo la kituo hiki ni kuandikisha watu 1,332, na kimkoa tunatarajia kuwa na watu 680,000 ,alifafanua Ndikilo.

"Wapo baadhi ya watu wanahadaa wenzao kwamba hakuna ulazima wa kujiandikisha kwenye daftari la wakazi ,na badala yake watatumia vitambulisho kama si cha uraia basi cha kupiga kura,sio kweli mtapoteza haki yenu ya msingi"

Hata hivyo Ndikilo alieleza ,suala la kupiga kura ni la wananchi wote siyo la watu wachache ili kuondoa malalamiko kuwa viongozi waliochaguliwa hawafai wakati wao hawakushiriki hilo ni tatizo.

Alisema taratibu zote zimekamilika ikiwa ni pamoja na fedha ambapo wasimamizi tayari wameshateuliwa  kwa ajili ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka.

Katika hatua nyingine ,anaeleza ni wakati wa mabadiliko na kujitambua kuacha kuchagua viongozi wanaokingiwa kifua na fedha zao kutoa rushwa bali wachague viongozi walio bora ,watakaowaletea maendeleo.

Nae ofisa uchaguzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Saidi Kayangu alisema ,wamejipanga kuweka mazingira rafiki na kusimamia haki kwa makundi yote ili kuondoa vikwazo wakati wa uchaguzi.

Alitoa wito kwa wananchi wenye sifa kushiriki katika uchaguzi huo muda utakapowadia kwani ushiriki wao ndio mchango katika maamuzi na washiriki bila rushwa.

Kayangu alihimiza, wananchi kujiorodhesha kwenye rejesta za wakazi katika mitaa yote 73 ili kupata takwimu kwa uhalisia hasa idadi ya kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea,:"hatua hii anaelezea itasaidia maandalizi ya uchaguzi kama vile idadi ya karatasi za kupiga kura.

IJUIE HISTORIA YA MAISHA YA MSANII WA BONGOFLEVA,HAWA NTAREJEA

$
0
0
Maisha ni mzunguko, Changamoto ni daraja la mafanikio, Mipango sio matumizi, Mvumilivu hula mbivu na Penya nia pana njia. usilo lijua ni kama usiku wagiza!. Karibu kwenye Historia ya 'Hawa Ntarejea'.

Majina yake kamili anaitwa Hawa Said lakini jina la usanii anaitambulika kama 'Hawa Ntarejea' Mnamo mwaka 1990 ilipofika tarehe 5/2 ndipo Hawa alipo zaliwa na kuanza kuishi maisha ya hapa Duniani. Kipindi hicho hakuweza kutambua kama Dunia inaweza kugeuka na kuwa chungu, kutokana na umri wake ulikuwa bado. Kadri siku zilivyo zidi kwenda Hawa alizidi kukua na kuanza kujitambua. 

Bahati nzuri Mungu alimjaalia Hawa kipawa cha Sauti nzuri na uwezo wa kuitumia, hivyo ulipofika wakati Hawa akajitambua vizuri ndipo alipoanza kuusogelea Muziki. Jamii ilimpokea kwa kishondo mara baada ya kushirikishwa kwenye wimbo wa Ntarejea na Diamond Platnumz, ambapo kila mmoja alitambua Hawa ninani! Kwenye wimbo alitoa sauti nyororo iliyo jaa simanzi kutokana na Ujumbe wa Wimbo huo.

Hivyo basi umaarufu wa wimbo huo ndio uliyo pelekea mpaka leo anaitwa Hawa Ntarejea. Mbali na mahusiano ya kimuziki baina ya Hawa na Diamond Platnuz wawili hao walikuwa katiaka Mahusiano ya Kimapenzi. Na hata kabla ya kuimba pamoja walikuwa tayari ni marafiki.

Baada ya maisha ya muziki wa Ntarejea Hawa na Diamond Platnumz waliendelea kuishi kama mtu na Mpenzi wake, lakini tunakumbushwa tu kuwa hakuna marefu yasio na ncha, Hivyo Penzi la Hawa na Diamond halikuweza kudumu. Amini nakwambia upendo ukizidi kiasi huleta madhara, Hawa alikuwa na upendo uliyo pitiliza kwa Diamond Platnumz hali hiyo ilipelekea akawa na wivu uliopita kiasi mwisho Penzi likaangamia.

Pamoja na hayo yote msimamo wa Hawa katika ndoto zake ili kuwa ni kuja kuwa msanii mkubwa Duniani kote! Tukirejea kwenye utangulizi wangu hapo awali kuna msemo nimesema “Mipango sio matumizi” kumbe basi kuna vitu ambavyo vilibadilisha na kuharibu mtazamo wa ndoto za Hawa. Baada muda kidogo miaka ya 2015 -2016 Hawa alipata mwanaume wa kumuoa na ndoa ikafungwa kutokana na tofauti zao za kidini Hawa alilazimika kubadili jina akaitwa 'Angel' Ndoa ilifanikiwa vizuri tena ni ile ya kupendana kwenye shida na raha.

Kuna wengine wanaweza wakasema ni mikosi lakini pengine si kweli bali ni mipango tu ya Mungu, Ndoa ya Hawa ambaye kipindi hicho alikuwa ni Angel na Mumewe haikuweza kudumu pia!. Ilikuwaje ilikuwa hivi, Maisha ya ndoa ya Hawa hayakuchukua muda mrefu, lakini ndani ya muda huo mchache kulikuwa na mikwaruzano ya hapa na pale baina ya ndugu wa Mume kwa Hawa yalizidi kuwekwa sawa na maisha mengine yakawa yanaendelea kama kawaida.

Sikumoja Mume akamwambia Hawa kuwa anataka kusafiri kwenda kutafuta maisha, lakini Hawa hakuvutiwa saana na safari hiyo maana hakukukubaliana naye yaani alikataa, kwa kumwambia kuwa “ Mbona mimi nalizika na tunacho kipata kwani nimesema siwezi kula ugali na mlenda au matembele? Kwani huko kuna kitugani cha ziada? Maswali haya ya Hawa hayakuweza kusaidia chochote kwasababu Mume alikuwa tayari kapanga plan zake! Hivyo aliaga kuwa anaenda Botswana Baada ya safari hiyo, Mume alikata mawasiliano kabisa kwa Hawa pia ndungu wa Mume hivyo hivyo, Hawa akabaki kwenye mataa mpaka hii leo 2019 toka 2015 – 2016 hana mawasiliano yeyote na Mumewe.

Kutokana na mgongano wa matukio yote hayo katika maisha ya Hawa yalipelekea akajikuta akiishi katika ndimbwi kubwa la mawazo. Hali hiyo ikasababisha ajikite zaidi kweye vilevi hasa pombe aina ya Gongo kwa kudhani kuwa itamsaidia kuondoa mawazo kumbe ndio alizidi kujiangamiza kiafya. Lakini pia alikondeana sana kiasi cha kupoteza mvuto kwenye macho ya watu.

2018 ulikuwa ni mwaka wa Hawa kuteseka kiafya maana alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo, madhara ambayo yalisababishwa na Mawazo pamoja na Vilevi ambavyo alikuwa akitumia kwa kusudio la kupunguza mawazo. Amini na kwambia Ukitenda wema utatendewa wema, pamoja na kwamba Hawa alikuwa kwenye hali mbaya lakini Diamond Platnumz alitambua thamani ya Hawa kwa roho ya huruma alishirikiana na team yake ya WCB kumpeleka India kwa ajili ya Matibabu ya Moyo, Baada ya matibabu Afya ya Hawa ilirejea vyema, Mapaka sasa Hawa anaendelea na Muziki na mashabiki wake bado wana upendo wa dhati kwa kile anacho kifanya.

Ukirejea tena kwenye uangulizi wangu nimesema “Changamoto ni daraja la mafanikio” hivyo basi kumbe huwezi kufanikiwa pasipo kupitia changamoto mbalimbali. Kwa mambo ambayo ameyapitia msanii Hawa yanatosha kuukaribisha ulimwengu wa Mafanikio, lakini kupitia maisha yake naamni kuna mengi utakuwa umejifunza.

Note: Hawa ni msanii wa muziki wa Bongo fleva ambaye alifamika kwa wimbo wa 'Ntarejea' aliyo shirikishwa na Diamond Platnumz, lakini ananyimbo zake zingine kama Kucheka na Shagala bagala kwa yote aliyo pitia ikumbukwe tu kuwa Hawa Ntarejea anyota ya Upendo pia anakipaji kikubwa anahitaji suport ya kila mmoja ili kutimiza ndoto zake alizo ahidi tangu alivyo kuwa mdogo!.

By Mr. Super News

MAHAKAMA YA RUFAA KUSIKILIZA KESI 60 KWA ‘VIDEO CONFERENCE’

$
0
0
Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Mhe. Richard Mziray akisikiliza kesi kwa njia ya mtandao “Video Coference”.
Mleta maombi Victor Binamungu (katikati) akiendelea na kesi yake dhidi ya Farida Hamza (kulia) na Geofrey Kabala (kushoto).
Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Mhe. Shabani Lila akiendesha kesi kwa mfumo huo (kushoto) Wakili Dkt. Masumbuko Lamwai.
Edward Chuwa na Aaron Kabunga wakifuatilia kesi baina yao wakiwa mkoani Mwanza.(Picha na Mary Gwera – Mahakama)


Na Magreth Kinabo – Mahakama
Mahakama ya Rufani Tanzania inatarajia kusikiliza jumla ya kesi 60 kwa kutumia mfumo wa mawasiliano kwa njia ya picha maarufu jina la ‘Video Conference’ kuanzia Oktoba 9 hadi 16, mwaka huu.

Mfumo huo ambao husaidia Mahakama ya Tanzania kuokoa fedha zinazotumika kuendesha kesi mbalimbali na muda unaotumika, ikiwemo kuwapunguzia gharama wanazozitumia wananchi kufika mahakamani kwa ajili ya kutafuta haki zao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Elizabeth Mkwizu, Mahakama hiyo itasikiliza kesi madai na jinai, zilizoko katika Masjala ya Tabora, Mwanza, Bukoba na Mbeya, ambazo zitasikilizwa na Majaji tofauti 17 wa Mahakama ya Rufaa.

Hivyo Mahakama hiyo, imeanza kusikiliza kesi hizo mapema Oktoba 9, mwaka huu na imesikiliza jumla ya kesi 12, zilizoko katika masjala ya Mwanza na Tabora kwa kutumia mfumo huo.

Kwa upande wa Mwanza, Mahakama hiyo imesikiliza kesi sita, kati ya hizo mbili zimesikilizwa na Mhe. Jaji Stella Mugasha, katika Kituo cha Mafunzo na Habari kilichopo Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Jaji Mugasha alisikiliza kesi ya maombi namba 447/08/2019 ya Benjamin Manota na wenzake ambao ni Mwana Selemani na Mussa Benjamin dhidi ya Geita Gold Mine Limited, ‘The Principal Secretary Minisrty of Minerals’ na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kesi hiyo imeahirishwa kwa sababu wadawa wote wamefariki mpaka watakapochaguliwa wasimamizi wa mirathi.

Kesi ya pili kusikilizwa na Jaji huyo ni kesi ya maombi ya madai namba 31/08/2019 ya Tella Bupamba dhidi ya Elisha Shija, inayohusu kuomba kuongezewa muda wa kibali cha kuja Mahakama ya Rufaa na imesikilizwa pande zote mbili na yanasubiriwa maamuzi yakiwa tayari wahusika watajulishwa.

Mahakama hiyo pia imeskiliza kesi ya tatu ambayo imesikilizwa na Mhe, Jaji Richard Mziray. Kesi hiyo namba 46/08/2019 ya Samwel Munsiro dhidi ya Chacha Mwikwabe.

Katika kesi hiyo Samwel ameomba nyongeza ya muda kuwasilisha kibali Mahakama Kuu ili aweze kuwasilisha maombi ya mara ya pili baada maombi ya awali kukataliwa, ambapo Mwikwabe alidai kuwa maombi yake hayana mantiki.

Mhe. Jaji Mziray alisema amewasikiliza na kuangalia nyaraka, hivyo atatoa uamuzi na utakapokuwa tayari watapewa.Jaji Mziray pia alisikiliza kesi ya madai ya maombi namba 602/08/2017 ya Victor Binamungu dhidi ya Geofrey Kabala na Farida Hamza.

Kesi hiyo ilihairishwa ili kutoa nafasi kwa Farida kuwasilisha nyaraka ya maelezo ya kesi na Majibu ya kiapo cha mleta maombi na kuhakikisha Victor na Geofrey wamezipata ndani ya siku 14 kuanzia Oktoba 9 mwaka huu. 

Kesi ya tano kusikilizwa ni madai ya maombi namba 63/17/2018 inayomhusu ‘The board of trustees of the National Social Security Fund,’ iliyowakilishwa na Wakili Dkt. Masumbuko Lamwai dhidi ya Nakara Hotel Limited, aliyewakilishwa na Dkt. Tugemeleza Nshalla, imesikilizwa na Mhe. Jaji Shabani Lila.

Jaji Lila aliahairisha kesi hii kwa sababu Dkt. Nshalla anaumwa, hivyo itasikilizwa siku nyingine.Kesi nyingine ya sita ya madai namba 32/08/2019 ya Edward Chuwa dhidi ya Aaron Kabunga, ambapo Chuwa aliomba kuongezewa muda.

Akisikiliza kesi hiyo Jaji Lila alisema hayana msingi katika Mahakama hiyo na alimwamuru mleta maombi kumlipa gharama aliziotumia mjibu maombi. 
Kwa upande wa masjala ya Tabora kesi sita zimesikilizwa, ambazo ni ya madai moja na jinai tano.Kesi hizi zimesikilizwa na majaji mbalimbali katika ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

Kesi zilizosikilizwa ni ya jinai namba 03/20/2015 ya Juma Kahukule dhidi ya Jamhuri,jinai namba 2/ ‘B’/2015 ya Hamis Mashishanga dhidi ya Jamhuri, jinai namba 3/20/2016 ya Chiganga Mapesa dhidi ya Jamhuri namadai namba 524/11/2018 ya Athumani Mauruti dhidi ya Yusta Maganga.

Nyingine ni jinai namba 02/2016 ya Hussein Masoud dhidi ya Yusuph Said na jinai namba 4/2016 ya Yusuph Said dhidi ya Jamhuri.

Kesi nyingine zitasikilizwa kwa kutumia mfumo huo, Oktoba 10, 15 na 16 mwaka huu. Mfumo huo ulianza kutumika rasmi Desemba 5, mwaka 2018, ambapo Mahakama ya Tanzania ilianza kutumia vitendea kazi vyake yenyewe.

TAASISI ZA UMMA ZAPIGWA MARUFUKU KUTUMIA KAMPUNI BINAFSI KATIKA MASUALA YA TEHAMA

$
0
0
Na James K. Mwanamyoto, Namtumbo
Serikali imepiga marufuku taasisi za umma nchini kutumia fedha za Serikali kuilipa taasisi binafsi ili kupatiwa huduma ambazo pia zinazotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) ametoa agizo hilo kwa watumishi wa umma na waajiri Serikalini, wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. 

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, Serikali imebadili Wakala ya Serikali Mtandao kuwa Mamlaka kwa sababu hivi sasa ina wataalamu wa kutosha wa TEHAMA hivyo hakuna ulazima wa kuilipa kampuni binafsi ili kupata huduma ya TEHAMA.

“Kama Serikali ina chombo chenye uwezo na weledi wa kutosha wa kutoa huduma za TEHAMA ikiwemo mifumo ya kielektroniki ya utoaji huduma, ni nini kinachoshinikiza Taasisi za Umma kuendelea kuomba kupatiwa huduma hiyo na kampuni za watu binafsi?,” Mhe. Mkuchika amehoji.

Mhe. Mkuchika yuko katika ziara ya kikazi mkoani Ruvuma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani humo.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao wilayani humo. 
 Baadhi ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), George H. Mkuchika (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha waziri huyo na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao wilayani humo. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), George H. Mkuchika (Mb) akifafanua masuala ya kiutumishi kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilichofanyika wilayani humo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji. 

MAKAMU MWENYEKITI WACCM ZANZIBAR.DK.SHEIN AZUNGUMZA NA WAZEE WA CCM WA WILAYA YA MKOANI PEMBA

$
0
0
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Wazee wa CCM wa Wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Mohammed Juma Pindua Mkoani, akiwa katika ziara yake Pemba
MZEE Issa Nassor Issa akichangia wakati wa mkutano wao na Makamu Mwenyekiti wa CC Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, uliofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Mohammed Juma Pindua Mkoani Pemba.
MZEE Mohammed Abass Mselem, akizungumza na kutowa shukrani kwa niaba ya Wazee wa CCM wa Wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba wakati wa mkutano wao na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein, yaliofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Mohammed Juma Pindua Mkoani Pemba.
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekitiu wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Mzee Mohammed Abass Mselem, baada ya kutowa neno la shukrani kwa niaba ya Wazee wa CCM Wilaya ya Mkoani Pemba, katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Mohammed Juma Pindua Mkoani Pemba.(Picha na Ikulu)

WATUHUMIWA WIZI WA MADINI WAFIKISHWA MAHAKAMANI

$
0
0
Watuhumiwa wa wizi wa Mawe yenye dhahabu mali ya Mgodi wa North
Mara wakiwasili Mahakamani.
Watuhumiwa wa wizi wa dhahabu wakiwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi wa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime.

*******************************

Na Tito Mselem Tarime,

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewafikisha
Mahakamani Watuhumiwa Wanane (8) kwa makosa mbalimbali
likiwemo la kuingia katika Mgodi wa North Mara na kuiba mifuko 15 ya
Mawe yenye Dhahabu yanayokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya
shilingi Milioni 234 za kitanzania.

Watuhumiwa hao waliingia Mgodini kwa nyakati tofauti kati ya tarehe 15
Septemba na 25 Septemba 2019 walikamatwa wakiwa na mawe mifuko
15 kinyume na Sheria.

Miongoni mwa watuhumiwa hao ni Zabron John (43), Jemes Makune
(35), Jonathan Chuwa (27), Amos Raphael (28), Mseti Chacha (29),
Chacha Marwa (29), Petro Mariba (32), na Samson Mathayo (17).

Akiwasomea mashtaka, Wakili wa Serikali Peter Ilole alitaja makosa yao
ni pamoja na kosa la kuhujumu uchumi, kutakatisha fedha, kuingia
mgodini bila kibali, kuiba mawe ya dhahabu pamoja na kukutwa na
madini bila kuwa na leseni ya uchimbaji au biashara ya madini.

Aidha, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara Mohamed
Robert Silii, hakuwaruhusu watuhumiwa hao kujibu lolote kwa sababu
Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashtaka yanayowakabili na
hivyo wakarudishwa rumande na kesi yao kuhairishwa hadi Oktoba 23,
2019 itakapotajwa tena.

Kosa la Kwanza ni kwa walishitakiwa wote Nane (8) kupanga njama
kinyume na sheria Wilayani Tarime Mkoa wa Mara na kuiba mawe ya
dhahabu katika mgodi wa Mgodi wa North Mara, kosa la Pili
watuhumiwa walikutwa wakiwa na mawe yenye madini bila ya kuwa na
leseni yoyote, Kosa la Tatu ni wizi wa mawe yenye dhahabu ambayo ni
mali ya Mgodi wa North Mara, Kosa la Nne ni utakatishaji wa fedha na
Kosa la Tano ni kuingia kwenye Mgodini bila ya kibali na kuiba mawe
yenye dhahabu yenye thamani ya shilingi 234,590,832/=.

Akizungumzia tukio hilo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo
amevipongeza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuwakamata
watuhumiwa hao na kutoa rai kwa watu wengine wenye tabia kama hizo
kuachana na wizi wa madini kwani Serkali iko macho kwa mtu yeyote
anayejihusisha na wizi wa madini.

Pia, Naibu Waziri Nyongo amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama
vihakikishe vinamkamata kiongozi wao Kitabo Ryoba Molel, ambaye
ndiye aliyedhamini wizi huo na baada ya kukamatwa alitoroka katika
kituo cha polisi Wilaya Tarime.

Ameongeza kitendo hicho cha kuwafikisha Mahakamani ni moja ya
jitihada zinazofanywa na Serikali katika kudhibiti wizi wa madini
unaojitokeza katika Migodi Mikubwa ambapo wafanyakazi wa Migodi
hiyo wanashirikiana na watu wa nje kuiba mali za wawekezaji.

Vilevile, Nyongo amewasisitiza wafanyabiashara wa madini kuyatumia
masoko ya madini kufanya biashara zao na kwa atakayebainika kufanya
biashara ya madini nje ya soko atakamatwa na kufikishwa Mahakamani
huku akiwaonya wale wote wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali kuacha
mara moja.

WATUHUMIWA WIZI WA MADINI WAFIKISHWA MAHAKAMANI

$
0
0
Na Tito Mselem Tarime,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewafikisha Mahakamani Watuhumiwa Wanane (8) kwa makosa mbalimbali likiwemo la kuingia katika Mgodi wa North Mara na kuiba mifuko 15 ya Mawe yenye Dhahabu yanayokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 234 za kitanzania.

Watuhumiwa hao waliingia Mgodini kwa nyakati tofauti kati ya tarehe 15 Septemba na 25 Septemba 2019 walikamatwa wakiwa na mawe mifuko 15 kinyume na Sheria. 

Miongoni mwa watuhumiwa hao ni Zabron John (43), Jemes Makune (35), Jonathan Chuwa (27), Amos Raphael (28), Mseti Chacha (29), Chacha Marwa (29), Petro Mariba (32), na Samson Mathayo (17).

Akiwasomea mashtaka, Wakili wa Serikali Peter Ilole alitaja makosa yao ni pamoja na kosa la kuhujumu uchumi, kutakatisha fedha, kuingia mgodini bila kibali, kuiba mawe ya dhahabu pamoja na kukutwa na madini bila kuwa na leseni ya uchimbaji au biashara ya madini.

Aidha, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara Mohamed Robert Silii, hakuwaruhusu watuhumiwa hao kujibu lolote kwa sababu Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashtaka yanayowakabili na hivyo wakarudishwa rumande na kesi yao kuhairishwa hadi Oktoba 23, 2019 itakapotajwa tena. 

Kosa la Kwanza ni kwa walishitakiwa wote Nane (8) kupanga njama kinyume na sheria Wilayani Tarime Mkoa wa Mara na kuiba mawe ya dhahabu katika mgodi wa Mgodi wa North Mara, kosa la Pili watuhumiwa walikutwa wakiwa na mawe yenye madini bila ya kuwa na leseni yoyote, Kosa la Tatu ni wizi wa mawe yenye dhahabu ambayo ni mali ya Mgodi wa North Mara, Kosa la Nne ni utakatishaji wa fedha na Kosa la Tano ni kuingia kwenye Mgodini bila ya kibali na kuiba mawe yenye dhahabu yenye thamani ya shilingi 234,590,832/=

Akizungumzia tukio hilo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amevipongeza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuwakamata watuhumiwa hao na kutoa rai kwa watu wengine wenye tabia kama hizo kuachana na wizi wa madini kwani Serkali iko macho kwa mtu yeyote anayejihusisha na wizi wa madini.

Pia, Naibu Waziri Nyongo amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama vihakikishe vinamkamata kiongozi wao Kitabo Ryoba Molel, ambaye ndiye aliyedhamini wizi huo na baada ya kukamatwa alitoroka katika kituo cha polisi Wilaya Tarime.

Ameongeza kitendo hicho cha kuwafikisha Mahakamani ni moja ya jitihada zinazofanywa na Serikali katika kudhibiti wizi wa madini unaojitokeza katika Migodi Mikubwa ambapo wafanyakazi wa Migodi hiyo wanashirikiana na watu wa nje kuiba mali za wawekezaji.

Vilevile, Nyongo amewasisitiza wafanyabiashara wa madini kuyatumia masoko ya madini kufanya biashara zao na kwa atakayebainika kufanya biashara ya madini nje ya soko atakamatwa na kufikishwa Mahakamani huku akiwaonya wale wote wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali kuacha mara moja.
 Watuhumiwa wa wizi wa Mawe yenye dhahabu mali ya Mgodi wa North Mara wakiwasili Mahakamani.
 Watuhumiwa wa wizi wa dhahabu wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime

MAJALIWA AKIWA KIJIJINI NANDAGALA ALIKOZALIWA, WILAYANI RUANGWA

$
0
0
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimnyanyua mtoto Safina Selemani (3) wakati aliposhiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kwenye kijiji alichozaliwa cha Nandagala wilayani Ruangwa, Oktoba 9, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Muhidin Hassan Said wakati alipoingia kwenye duka la mfanybiashara huyo katika kijiji alichozaliwa cha Nandagala wilayani Ruangwa, Oktoba 9, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na vijana wa kikundi cha uhamsishaji cha wilaya ya Ruangwa kwenye ukumbi wa Ofisi ya CCM ya wilaya ya wilaya hiyo, Oktoba 9, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

TSA yaja na Mafunzo ya kuogelea shule za Msingi, Sekondar

$
0
0
Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA) kimezindua mafunzo ya mchezo wa kuogelea kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Mafunzo hayo yenye lengo la kuutangaza mchezo huo na kuuendeleza, yatafanyika kwa shule sita za mkoa wa Dar es Salaam kwa kuanzia. Mafunzo hayo ni sehemu ya udhamini wa Shirikisho la kuogelea, Fina).

Mkurugenzi wa Ufundi wa TSA, Amina Mfaume alisema kuwa jumla ya wanafunzi 100 wamepata fursa ya kujifunza mafunzo hayo ambayo yanaendeshwa kwa njia ya kujitolea na makocha mbalimbali.

Mfaume alisema kuwa  wanafaunzi hao watapata fursa ya kuonyesha walichojifunza  Jumamosi (Oktoba 12) wkati wa maadhimisho ya Siku ya Kuogelea Duniani (Fina Aquatic day) kwenye bwawa la kuogelea la Shaaban Robert.

Alisema kuwa programu hiyo ina lengo la kuutangaza mchezo huo sambamba na kutafuta vipaji kwa ajili ya klabu na timu mbalimbali za Taifa na itaendeshwa nchi nzima kwa kipindi maalum.

“Tumeanza na shule sita, Diamond, Olympio na Upanga kwa shule za Msingi wakati na kwa upande wa sekondari ni Azania, Jangwani na Zanaki, baada ya shule hizo, makocha watatembelea shule mbalimbali ili kutafuta wanafunzi ambao watapata mafunzo zaidi, lengo ni kupata waogeleaji wengi zaidi wa vilabu na timu ya Taifa,” alisema Mfaume.

Alisema kuwa waogeleaji hao watapatiwa vifaa vya mchezo huo na kuviomba vilabu mbalimbali kufika siku ya kufunga ili kuchagua waogeleaji ambao watajiunga na timu zao.

MWENGE WA UHURU WAMALIZA MBIO RUANGWA

$
0
0
*Wapitisha miradi yote mitatu iliyozinduliwa

MWENGE wa Uhuru uliokuwa unakimbizwa wilayani Ruangwa, mkoani Lindi umemaliza mbio zake na kukabidhiwa wilayani Nachingwea.

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Bw. Mzee Ali Mkongea amesema miradi mitatu ya maendeleo iliyopangwa kuzinduliwa wilayani humo, imeridhiwa na wataalamu wake.

Miradi hiyo ni mabweni mawili kwenye shule ye sekondari ya wasishana ya Hawa Mchopa, mradi wa maji wa Kitandi katika kata ya Likunja na mradi wa barabara ya lami kwenye kata ya Nachingwea, iliyoko Ruangwa mjini.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kupokea mwenge huo leo asubuhi (Alhamisi, Oktoba 10, 2019) kwenye viwanja vya shule ya msingi Chiola, wilayani Nachingwea, Bw. Mkongea amewataka wananchi wa wilaya hiyo wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na pia wajitokeze kupiga kura siku ya uchaguzi huo, Novemba 24, mwaka huu.

Mapema, akizungumza na wakazi waliojitokeza kuupokea mwenge huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mwenge wa uhuru unakimbizwa maeneo mbalimbali nchini ili kuwahamasisha wananchi washiriki kwenye shughuli za maendeleo.

“Mwenge wa Uhuru unakimbizwa kwenye maeneo yetu mbalimbali ili kuwahamasisha wananchi wajitokeze kushiriki kwenye miradi ya kujiletea maendeleo. Pia unaendana na kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hivyo, tunakumbushwa kuyaenzi mawazo yake,” alisema.

Mbali ya kuwahimiza washiriki kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu alisema kuna makundi manne ambayo yanapaswa kushiriki uboreshaji wa taarifa zao kwenye Daftari la Mpiga Kura pindi zoezi hilo likianza.

“Wanaotakiwa kushiriki zoezi hili, ni wale waliopoteza vitambulisho vyao au wanavyo lakini vimefutika; waliohama maeneo yao na wako kwenye maeneo mapya ambako watapigia kura mwakani; waliokuwa na umri chini ya miaka 18 mwaka 2015 na sasa wamezidi umri huo; na wale ambao mwakani wanatarajia kufikisha umri wa miaka 18,” alisema.

Mapema, akizungumza baada ya kupokea mwenge huo saa 2:45 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Bi. Rukia Muwango alisema leo utakimbizwa kwenye wilaya hiyo ambapo miradi yenye thamani ya sh. milioni 781.5 itazinduliwa.

Kesho (Ijumaa, Oktoba 11) mwenge huo utaenda Liwale, Jumamosi (Oktoba 12) utaenda Kilwa na Jumapili (Oktoba 13) utakuwa Manispaa ya Lindi ambako utahitimisha mbio hizo na kuzimwa Oktoba 14, mwaka huu.

RC KIGOMA AIPONGEZA MAHAKAMA KWA KUSOGEZA HUDUMA YA MAHAKAMA KUU

$
0
0

Na Festo Sanga, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kigoma
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kigoma ikiongozwa na  Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga imetembelea Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na Nyumba za Makazi za Majaji na kupongeza upatikanaji wa huduma ya Mahakama Kuu katika mkoa huo.

Ugeni huo ulitembelea miradi hiyo ya ujenzi mapema  Oktoba 08, 2019 na ulipokelewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Ilvin Mugeta. 
Katika ziara hiyo, Brigedia Jenerali Mstaafu Maganga amepongeza jitihada za Mahakama ya Tanzania katika kusogeza huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwani awali  walikuwa wakisafiri umbali wa takribani  kilomita 858(kwenda na kurudi) kufuata huduma za Mahakama Kuu Mkoani Tabora. 

Pia amepongeza utendaji kazi  wa Mkandarasi wa  ‘Masasi Construction Co Ltd’ anayejenga jengo la Mahakama Kuu pamoja na nyumba za Makazi za Majaji.
“Wajumbe wenzangu tuone uwezekano wa kuwatumia wakandarasi hawa katika miradi ya ujenzi kutokana na kazi waliyoifanya katika jengo hili,” alisema Mkuu wa Mkoa 

Ziara hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa Mpango ulioandaliwa na Uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma kuhakikisha wadau wa Mahakama Mkoa wa Kigoma wanapata fursa ya kutembelea jengo hilo jipya na kujionea miundo mbinu iliyopo ikiwa ni pamoja na kupata elimu.
Baadhi ya wadau wakiwemo wajumbe wa Haki Jinai Mkoa, wajumbe wa vituo vya msaada wa kisheria( paralegal) Mkoa wa Kigoma, watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma, wazabuni mbalimbali waliweza kutembelea jengo hilo ambalo linatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni. 
  Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga (katikati) akifafanua jambo wakati yeye pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipofanya ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa Mahakama Kuu Kigoma na nyumba za makazi ya Wahe. Majaji.
 Muonekano wa jengo jipya la Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma.
 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Ilvin Mugeta akiongoza msafara wa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi mara walipofika Katika jengo la Mahakama Kuu Kigoma. Nyuma ya Mhe. Jaji  ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga.
 Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga akiteta jambo na Mhe. Jaji Mfawidhi  pamoja na Wakandarasi katika UKumbi wa Wazi wa Jengo la Mahakama Kuu.

Picha ya pamoja ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kigoma, Viongozi wa Mahakama na Wakandarasi wa 'Masasi Construction Ltd.'

MBUNGE LEMA AAHIDI KUTOA MAGARI 20 KUHAMASISHA UANDIKISHAJI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA

$
0
0
Na Jusline Marco-Arusha.

Mbunge wa Arusha mjini,Godbless Lema ameahidi kutoa magari 20 yatakayogharimu milioni sita kwa ajili uhamasishaji wa uandikishaji wa daftari la wapiga kura.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amesema kuwa licha ya uhamasishaji kuwa mdogo pia mawakala wao hawapewi daftari ili kufahamu  tathimini ya waliojiandikisha kwa siku  ingawa wanayo haki ya kujua idadi hiyo ili kuondoa ubadhirifu wa majina yatakayoongezwa  kupitia mawakala wote.

"Tatizo la kuwanyima mawakala wetu  kujua idadi waliojiandikisha na uhamasishaji wa gari la matangazo kupita kwa kasi hivyo naomba wananchi wajitokeze kujiandikisha kwa wingi hili waweze kuchagua kiongozi atakayeleta maendeleo," alisema Mbunge huyo.

Aidha amesema pamoja na mawakala kutopewa ruhusa ya kukagua daftari hilo amewataka  wananchi kujitokeze kujiandikisha kwa wingi ili ifikapo Novemba mwaka huu wakafanye maamuzi sahihi ya kuchagua wenyeviti wa serikali za mtaa.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha demokrasia na maendeleo(Chadema) wa wilaya ya Arusha mjini,Innocent Kasanyage amesema kitendo cha mawakala wao kuzuiwa kujua idadi ya waliojiandikisha ni kinyume na sheria hivyo kama chama watapeleka malalamiko kwenye baraza la nidhamu msimamizi wa uchaguzi wa wilaya hiyo.

Akizungumza kwa njia ya simu Msimamizi wa uchaguzi jiji la Arusha,Mpena Bina amesema ni haki ya wakala wa uchaguzi kufahamu idadi ya watu waliojiandikisha kwa siku isipokuwa changamoto ni pale wakala anapochelewa kufika kituoni hukuta mwandikishaji akiendelea.

"Kwa kuwa changamoto hii nimeisikia kwako kwa Mara ya kwanza nitaifanyia kazi kama kuna baadhi ya watu wanawazuia mawakala kujua idadi ya waliojiandikisha," alisema Msimamizi huyo.
Mbunge waArusha Mjini Mhe.Godbless Lema akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mapema leo kuhusiana na baadhi ya mawakala wako walio katika vituo vya uchaguzi kuzuiwa kukagua daftari la uandikishwaji.

MKUCHIKA APONGEZA WATUMISHI WA UMMA KUPANDA MAPATO YA SERIKALI

$
0
0
Na Mwandishi Wetu, Tunduru

WAZIRI wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt Mstaafu Georg Mkuchika,amewapongeza Watumishi wa Umma hapa Nchini kwa kuwezesha mapato ya Serikali kuongezeka kutoka Shilingi Bilioni 800  mwaka 2015  hadi kufikia Trilioni 1.7 Mwezi Septemba 2019.

Kapt Mkuchika ametoa pongezi hizo jana wakati akizungumza na  watumishi  wa wilaya ya Tunduru, wakati wa ziara yake ya siku tano mkoani Ruvuma inayolenga kusikiliza kero na kuongea na watumishi wa Umma katika wilaya zote tano za mkoa huo.

Kwa mujibu wake,mafanikio hayo ya Serikali ya yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na Watumishi Halmashauri za Wilaya,Miji,Manispaa na Majiji kutokana na kusimamia vema  mapato yanayopatikana kutoka kwenye vyanzo vya mapato.

Hata hivyo Mkuchika alisema, pamoja na makusanyo  mazuri ya kodi watumishi kutojaribu  kuzitumbuiza fedha mifukoni mwao, badala yake zielekezwe katika kuwapatia wananchi huduma Bora na za msingi kama Elimu,Maji,Afya na miundombinu mbalimbali.

Alisema,  asilimia kubwa fedha zinazokusanywa zinapelekwa kwenye Serikali za Mitaa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwataka watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru kuhakikisha wana simamia vema fedha na zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Aidha alionya kuwa,Serikali inavyo vyombo vya Dola ikiwemo Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa(TAKUKURU) ambavyo kazi yake ni kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha zinazopelekwa kwenye Halmashauri na Idara nyingine za Serikali.

Akizungumzia suala la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa Umma Kapt Mkuchika alisema,zoezi hilo ni endelevu hata hivyo limekuwa na changamoto kadhaa,lakini Serikali baada ya kubaini hali hiyo ilitoa maelekezo kuwa Watumishi wote ambao walikuwa na ajira za kudumua au  mikataba ambao walikuwa kazini kabla ya tarehe 20 Mei 2004 ulipoanza kutumika waraka wa Utumishi warejeshwe kazini na walipwe  mishahara yao hadi watakapostaafu.

Alisema, katika  zoezi hilo watumishi Elfu Moja Mia Tatu Sabini(1,370) waliolegezewa masharti  ya sifa za muundo kupitia Barua ya Katibu Mkuu Utumishi wa Umma Juni 2011, hata hivyo alifafanua kuwa haukuwahusu watumishi wale wenye vyeti vya kughushi, na walioajiriwa baada ya Mwaka 2014.

Mkuchika amewataka watumishi wa Umma,kutekeleza majukumu yao  kwa kuzingatia Weledi, na kuacha  kufanya kazi kwa mazoea, na kuacha ubabaishaji tabia ambayo inakwamisha sana malengo ya Serikali ya awamu ya tano.

Pia Mkuchika amezitaja idara ya kilimo,Maji na Utawala zinaongozwa kulalamikiwa  kuhusu vitendo vya Rushwa  na kuwataka watumishi wa Idara hizo kubadilika na kujiepusha na vitendo vya Rushwa ambavyo vinachangia kuwepo kwa miradi hewa na watumishi wa chini kukosa haki zao.

Hata hivyo baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, wamelalamikia kutopandishwa vyeo mara wanaporudi kutoka vyuoni na wengine kutolipwa stahiki zao kama fedha za uhamisho na kupandishwa madaraja.

DODOMA YA KIJANI INAWEZEKANA - SAMIA SULUHU HASSAN

$
0
0
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akikagua miti iliyopandwa wakati wa kampeni ya kukijanisha Dodoma katika eneo la Mzakwe jijini Dodoma ikiwa sehemu ya ufuatiliaji wa ukuaji wa miti hiyo.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Godwin Kunambi wakati wa ziara ya ukaguzi wa miti iliyopandwa wakati wa kampeni ya kukijanisha Dodoma.  Wengine katika picha ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Bw. Patrobas Katambi na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandishi Joseph Malongo


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kutoka kwa Mwakilishi wa Wakala wa Misitu Tanzania Kanda ya Kati Bi. Teddy Yoramu  juu ukuaji wa miti iliyopandwa katika eneo la Mzakwe jijini Dodoma wakati wa kampeni ya Kuifanya Dodoma ya Kijani.


Lulu Mussa na Monica Sapanjo


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema azma ya kuifanya Dodoma kuwa ya Kijani iko pale pale.

Hayo yamesemwa leo mara baada ya kutembelea shamba la miti lililopo katika eneo la Mzakwe katika Kambi ya Jeshi la Makutupora Jijini Dodoma, ikiwa ni ufuatiliaji wa Kampeni aliyozindua mwaka 2017 ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.


Makamu wa Rais ameupongeza uongozi wa Kambi ya Jeshi ya Makutupora, Wakala wa Misitu Tanzania na Watendaji wa Ofisi yake kwa kuhakikisha miti iliyopandwa mwezi Desemba 2017 inastawi.


“Vitabu vya dini vinasema Moja kati ya sadaka endelevu ni kupanda miti, miti hii imekuwa na kustawi kwasababu ya jitihada zenu za kuimwagilia na kuitunza, msikate tamaa, endeleeni na kazi hii njema ambayo matokeo yake yanaonekana ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa mifumo ya hali ya hewa ambayo huimarisha shughuli za kilimo na maendeleo ya viwanda.” Alisisitiza Makamu wa Rais.


Nae Mkuu wa Kambi ya Jeshi ya Makutupora Luteni Kanali Festo Mbanga amesema kuwa miti 2300 ilipandwa  tarehe 21/12/2017 na kati ya hiyo miti 2076 imekuwa na kustawi ikiwa ni sawa na asilimia 90.3 ya miti yote iliyopandwa.“Katika miti iliyooteshwa awali baadhi haikuota, hivyo tumefanya jitihada za kuirudishia, tumepanda takriban miti 300 ya ziada” alisema Luteni Kanali Mbanga.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha tafiti zinakamilika mapema kutoka katika sampuli ya udongo iliyochukuliwa ili kubaini aina ya miti inayostawi katika eneo hilo na Jiji la Dodoma kwa Ujumla.


Kampeni ya Kukijanisha Dodoma ilizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 21/12/2017 katika eneo la Mzakwe Jijini Dodoma ambapo miti 2300 ilipandwa siku hiyo.


Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari asikiliza na kutatua kero za wateja wa Tigo katika wiki ya huduma kwa wateja.

$
0
0


Mkuu wa kitengo cha huduma kwa wateja (Tigo)Bi. Mwangaza Matotola -, akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mawasiliano Tigo Bw. Simon Karikari pamoja na viongozi wa idara mbalimbali katika kituo cha kisasa cha huduma kwa wateja. Tukio hilo liliambatana na ukataji wa keki.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mawasiliano TIGO Bw. Simon Karikari akimuongoza mteja katika duka la Tigo Mlimani City kukata keki ya kusherehekea wiki ya Huduma Kwa Wateja pamoja na kushiriki katika kutoa huduma kwa wateja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari, akijibu na kutatua maswali ya wateja wa Tigo katika kituo cha cha kisasa cha huduma kwa wateja , zoezi hilo limefanyika katika wiki ya huduma kwa wateja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari, akijibu na kutatua maswali ya wateja wa Tigo katika kituo cha cha kisasa cha huduma kwa wateja , zoezi hilo limefanyika katika wiki ya huduma kwa wateja.
Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya mawasiliano TIGO Bw. Simon Karikari ametembelea duka la Tigo Mlimani City na kupata nafasi ya kushiriki katika wiki ya huduma kwa wateja na wateja wa Tigo waliokuwa wakiendelea kupata huduma.

MARUFUKU KUTOA MATANGAZO YA DAWA BILA KIBALI -TMDA

Msimamizi wa Mirathi ya mke wa Balali, Kizimbani kwa utapeli👆🏻

$
0
0
Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.

MFANYABASHARA, Elizabeth Balali (54) ambaye anadaiwa kuwa msimamizi wa Mirathi za mke wa marehemu Daud Balali, mkazi wa Boko Magengeni jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kujipatia Sh milioni 25 kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha wa fedha.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa serikali Mwandamizi, Simon Wankyo amedai Mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa kati ya Oktoba 19 na Desemba 21, 2017 Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia kiasi cha Sh 25 milioni kutoka kwa Dk Roderick Kisenge kwa njia ya ulaghai akijifanya anamuuzia eneo la squre mita 900 ambalo halijapimwa lililopo eneo la Boko Dovya Kinondoni wakati akijua kuwa eneo hilo si lake.

Katika shtaka la pili imedaiwa, siku na mahali hapo hapo mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha Sh. Milioni 25 kutoka kwa Dk Kisenge kupitia akaunti yake iliyopo kwenye benki ya CRDB wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo,Elizabeth hakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikilizwa makosa ya Uhujumu Uchumi na pia shtaka la utakatishaji wa fedha halina dhamana.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa alipelekwa rumande.

RAIS WA ZANZIBAR DK. SHEIN AFUNGUA MAONESHO YA MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI VIWANJA VYA CHAMANANGWE PEMBA

$
0
0
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi, wakitembelea banda laMaonesho la Kikundi cha Ulimwengu wa Miti Mirefu, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Siku ya ChakulaDuniani yaliofanyika katika viwanja vya Chamanangwe Wilaya ya Wete Pemba.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akifungua Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani yaliofanyika katika viwanja vya Chamanangwe Wilaya ya Wete Pemba , kulia Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar.Mhe. Mmanga Mjengo Mjawiri.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani yaliofanyika katika viwanja vya Chamanangwe Wilaya ya Wete Pemba leo.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza laMapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein, akitembelea banda la Maonesho la Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar.(ZSTC) wakati wa hafla ya maonesho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika katika viwanja vya Chamanangwe Wilaya ya Wete Pemba.(Picha na Ikulu)RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akimsikiliza Afisa wa Chuo Cha Mafunzo Zaameja.Khamis Seif, wakati akitembelea maonesho hayo katika Kitali cha Shamba la Mihindi na Mtama katika viwanja vya Chamanangwe Wilaya ya Wete Pemba.(Picha na Ikulu)

Watumishi wa umma, Watanzani jitokezeni kujiandikisha-Kailima

$
0
0

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Chimuli, Kata ya Makole,mkoani Dodoma, John Fundi akimshukuru Naibu Katibu MkuuWizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima(aliyekaa katikati), kwa kujitokeza na kujiandikisha katikadaftari la wapiga kura. Kulia ni muandikishaji, Peter Ititi.


Na Mwandishi Wetu, MOHA

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Ramadhan Kailima, ametoa wito kwa watumishi wa umma na
Watanzania kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili
kutumia fursa hiyo kuchague viongozi wenye sifa karika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kailima aliyasema hayo Mjini Dodoma jana asubuhi baada ya
kujiandikisha katika daftari hilo kwenye kituo kilichopo Mtaa
wa Chimuli, Kata ya Makole.

Alisema uzoefu unaonyesha kuwa, kuna mwamko mdogo kwa
kundi la watumishi wa umma kujiandikisha, kushiriki uchaguzi
huo ili waweze kuchagua viongozi wenye sifa.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa una umuhimu mkubwa kwa
maendeleo ya nchi na wananchi kwa ujumla, uandikishaji huu
umeanza Oktoba 8-14, mwaka huu.

“Kampeni zitafanyika kwa wiki moja kuanzia Novemba 17-23,
mwaka huu, uchaguzi utafanyika Novemba 24, mwaka huu…ni muhimu jamii kutambua kuwa, mshindi katika uchaguzi huu atapatikana kwa idadi ya wapiga kura sio asilimia,” alisema.

Kailima alisema ni muhimu Watanzania wakashiriki uchaguzi
huo uli watumie fursa hiyo kuchagua kiongozi anayestahili,
wasiposhiriki atachaguliwa Mwenyekiti wa Serikali ama
mjumbe ambaye jamii kubwa haitapenda achaguliwe.

“Nawaomba wananchi wahudhurie kampeni, waulize maswali
kwa wagombea, watumie fursa hiyo kuchagua viongozi ambao
ni waadilifu na waaminifu.

“Rushwa ni adui wa maendeleo, wananchi mjiepushe kupokea
rushwa, Wizara yangu kupitia taasisi zake za ulinzi na usalama
ziko imara, tutaimarisha ulinzi wakati wa kampeni, upigaji kura
na utangazaji matokeo,” alifafanua.

Aliwapongeza waandikishaji, wasimamizi wa zoezi hilo kwa
kufika mapema kwenye vituo vya uandikishaji wapiga kura.
Alisema vituo hivyo viko sehemu barabarani, mitaani ambapo
uandikishaji huo hauna vikwazo kwani hauhitaji kitambulisho
cha uraia, cheti cha kuzaliwa.

“Ukifika kituoni utaulizwa majina yako kamili, umri wako, eneo
unaloishi…kama eneo lako la kujiandikisha sio hilo utaelekezwa
eneo la kwenda kujiandikisha,” aliongeza.

Kwa upande wao, mwandikishaji wapiga kura katika kituo
hicho, Peter Ititi na mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo, John

Fundi walimshukuru Kailima kwa wito alioutoa ili jamii ione
umuhimu wa kushiriki uchaguzi huo.

NAIBU SPIKA AFUNGUA KONGOMANO LA WASICHANA JIJINI DAR ES SALAAM

$
0
0
Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa kongamano lilowakutanisha wasichana kutoka mikoa ya Mara, Dodoma na Dar es Salaam ili kujadili chagamoto zinazomkabili Mtoto wa Kike katika kuelekea maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) . Wengine katika picha kutoka kushoto ni Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) Prof. Bernadeta Killian, Balozi wa Sweden nchini Mhe. Andres Sjoberg na Kaimu Mkurugenzi wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) Bi.Lennyster Byalugaba.
Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (katikati) akizungumza wakati wa kongamano lilowakutanisha wasichana kutoka mikoa ya Mara, Dodoma na Dar es Salaam ili kujadili chagamoto zinazomkabili Mtoto wa Kike katika kuelekea maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) . Wengine katika picha ni Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) Prof. Bernadeta Killian (kushoto) na Balozi wa Sweden nchini Mhe. Andres Sjoberg (kulia).
Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (wa pili kulia kwa waliokaa) katika picha ya pamoja na washiriki wa kongamano lilowakutanisha wasichana kutoka mikoa ya Mara, Dodoma na Dar es Salaam ili kujadili chagamoto zinazomkabili Mtoto wa Kike katika kuelekea maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE).
Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) Prof. Bernadeta Killian (kulia) alipokwenda Chuoni hapo kwenye Kongamano lilowakutanisha wasichana kutoka mikoa ya Mara, Dodoma na Dar es Salaam ili kujadili chagamoto zinazomkabili Mtoto wa Kike katika kuelekea maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike.
Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (kulia) akiaagana na Balozi wa Sweden nchini Mhe. Andres Sjoberg (wa kwanza kushoto), Kaimu Mkurugenzi wa Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) Bi.Lennyster Byalugaba (katikati) na Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) Prof. Bernadeta Killian mara baada ya kuzungumza na washiriki wa Kongamano lilowakutanisha wasichana kutoka mikoa ya Mara, Dodoma na Dar es Salaam ili kujadili chagamoto zinazomkabili Mtoto wa Kike katika kuelekea maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike.

PICHA NA BUNGE
Viewing all 110173 articles
Browse latest View live




Latest Images