Na Novatus Makunga,Simanjiro Agosti 01,2019
Vijana 24 wa jamii ya kabila la Kimasai katika wilaya za Simanjiro na Kiteto wameanza mafunzo ya ufundi uashi baada ya kukamilika kwa chuo pekee za ufundi katika wilaya hizo kilichojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 531.
Chuo hicho kilichopo katika kata Emboret wilayani Simanjiro ambacho kimejengwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la ECLAT Development Foundation kwa ufadhili wa shirika la Upendo Society la nchini Ujerumani,kimekabidhiwa kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Nchini(VETA).
Akizungumza wakati wa kuwapokea wanafunzi , mwenyekiti wa shirika la ECLAT,Peter Toima alisema kuwa hiyo ni awamu ya kwanza inayohusisha madarasa,bweni moja,jiko,vyoo,kisima kirefu cha maji,umeme wa nishati ya jua na vifaa vya kufundishia uashi.
“Tuliamua kujikita katika ujenzi wa Chuo hiki kwa lengo la kuunga mkono mpango wa serikali wa kujenga vyuo vya ufundi stadi kwa kila wilaya huku tukizingatia kipaumbele cha wananchi wenyewe wa Simanjiro,”alisema.
Naye mwenyekiti wa shirika la Upendo la Ujerumani ambao ndiyo wafadhili wa mradi huo,Dk.Fred Heimbach aliwataka wanafunzi hao wa awali kusoma kwa bidii kwani wamepata fursa ambayo inawahakikishia ajira na baadaye kuweza kuendesha maisha ya.
Kwa upande wake Mratibu wa VETA kanda ya kati,Abdulkadiri Yussuf alisema kuwa chuo hicho kimeanza mafunzo ya fani ya uashi kutokana na mahitaji ya wananchi wa wilaya ya Simanjiro na wilaya ya jirani ya Kiteto ya mafundi wa ujenzi wa majengo.
“Kwa ujumla katika wilaya ya Simanjiro hivi sasa kuna kasi kubwa ya ujenzi wa nyumba lakini kuna changamoto kubwa ya mafundi wanatoka mjini Arusha kuja kujenga nyumba hapa”alisema.
Yussuf alisema kuwa katika awamu ya pili ya chuo hicho,kitaanzisha fani nyingine zikiwemo ufundi seremala,ufundi umeme na bomba,ushonaji wa nguo pamoja na ufundi wa zana na mitambo ya kilimo.
Alisema chuo hicho ambacho mpaka kitakapokamilika kitakuwa na wanafunzi 250 pia kitaanzisha mafunzo ya ufugaji wa kisasa na wa kibiashara wa ng’ombe,mbuzi,kondoaa na kuku pamoja na wanyamakazi kama vile punda.
Aidha alisema kuwa katika mwaka huu wa fedha wameshatenga shilingi milioni 81 kwa ajili ya kujenga bweni lingine litakalokuwa na uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 24 katika eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 100.
Diwani wa kata ya Emboret,Christopher Kuya alisema chuo hicho kitakuwakomboa vijana wengi wanaozurura mitaani kutokana na kushindwa kuendelea na elimu ya juu baada ya kuhitimu darasa la saba na kidato cha nne.
Alisema kuwa kuhitimu kwao katika fani mbalimbali za ufundi kutawawezesha kujiajiri na pia kuajiriwa kama mafundi wa ngazi ya kati hivyo kuingia katika mwelekeo wa serikali ya sasa ya Tanzania ya viwanda
Kuya alisema kuwa hivi sasa katikan maeneo ya Umasaini kuna kasi kubwa ya ujenzi wa nyumba za kisasa na ununuzi wa pikipiki maarufu kama bodaboda na hivyo mafundi wengi wanahitajika
Mkufunzi wa chuo cha ufundi cha VETA Simanjiro,David Mrutu(kulia) akitoa maelezo ya vifaa vya kufundishia uashi kwa mwenyekiti wa shirika la ECLAT,Peter Toima(katikati) na Mwenyekiti wa Shirika la Upendo Society la Ujerumani Dkt.Fred Heimbach(kushoto).
Mwenyekiti wa shirika la ECLAT,Peter Toima na mwenyekiti wa Shirika la Upendo Society la Ujerumani,Dkt.Ferd Heimbach wakitoa nasaha kwa baadhi ya wanafunzi walioanza masomo katika chuo cha ufundi cha VETA Simanjiro.
Mwenyekiti wa ECLAT,Peter Toima(kushoto) na Mwenyekiti wa Shirika la Upendo Society la Ujeruman Dkt.Fred Heimbach(kulia) wakitoa maelekezo kwa msimamizi wa miradi inayotekelezwa na mashirika hayoMasham Bakiri(katikati)
Mkufunzi wa chuo cha ufundi VETA Simanjiro,David Mrutu akikagua vifaa vya kufundishia ufundi uashi katika chuo hicho
Mwenyekiti wa ECLAT,Peter Toima(kushoto) na Mwenyekiti wa Shirika la Upendo Society la Ujeruman Dkt.Fred Heimbach(kulia) wakikagua vifaa vya kufundishia ufundu uashi katika chuo cha VETA Simanjiro
Mratibu wa Mamlaka ya Elimu na Ufundi Studi(VETA) katika kanda ya kati Abdulkarimu Yussuf akizungumza na waandidhi wa habari(hawapo pichani) nje ya moja ya jengo la chuo cha ufundi VETA Simanjiro.(Picha na Novatus Makunga)