Quantcast
Channel: MICHUZI BLOG
Viewing all 110170 articles
Browse latest View live

BBC DIRA YA DUNIA JUMATANO 04.07.2018


TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE YAINGIA KATIKA ANGA ZA KIMATAIFA KWA KUWA KITUO CHA UFUATILIAJI WA KUFANYA UPASUAJI WA MOYO KWA WATOTO

$
0
0
Katika kuimarisha uhusiano na uboreshaji wa upasuaji wa magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo kwa watoto Tanzania kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imechaguliwa kuwa kituo cha ufuatiliaji na shirika la (International Quality Improvement Collaborative for Congenital  Heart Surgery (IQIC) la nchini Marekani.
Kabla ya kuchagulia kuwa kituo cha mafunzo mwaka jana mwezi wa 12  Shirika la IQIC ambalo linasimamiwa na Hospitali ya kimataifa ya watoto ya Boston nchini Marekani  liliangalia Hospitali ambayo inafanya kazi  zake vizuri katika upasuaji wa moyo kwa watoto na kuomba taarifa ya kazi walizozifanya kwa kipindi cha  miaka miwili iliyopita.
Kutambulika kwake kimataifa na kuwa moja ya vituo 66 kutoka nchi 25 Duniani Taasisi yetu itatumika kutoa elimu katika nchi za Afrika, wataalamu kutoka IQIC watakuja kutoa elimu kwa madaktari wetu pamoja na madaktari wengine wa moyo kwa watoto  wa Afrika.
Kwa upande wa watoto kliniki yetu  kila siku inatoa huduma kwa  wagonjwa 25 hadi 30 na kulaza mgonjwa mmoja hadi wawili . 
Mwaka jana upasuaji wa kufungua kifua ulifanyika   kwa watoto 182 na bila kufungua kifua kwa watoto 92.  Tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2018 jumla ya watoto 82 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na bila kufungua kifua  watoto 26.
Zaidi ya asilimia 75 ya watoto wanaofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na magonjwa yanayoshambulia milango ya mishipa mikubwa na midogo ya moyo. Asilimia 25 ni wale ambao walizaliwa salama lakini wameyapata matatizo hayo baada ya kuzaliwa. 
Taasisi inaendelea kutoa wito kwa wazazi na walezi wasisahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwani magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni. 
Mtoto akianza kuuguwa magonjwa ya moyo wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua baada ya kumfikisha mtoto Hospitali na kufanyiwa vipimo  ndipo inagundulikwa kuwa mtoto anasumbuliwa na magonjwa ya moyo. 

Kwa wamama wajawazito wafanye uchunguzi (Fetal Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni anamatatizo ya moyo au la. Kupitia kipimo hiki  mtoto akigundulika kuwa  na tatizo la moyo ataweza kupatiwa  matibabu kwa wakati  na hivyo kuwa na afya njema kama watoto wengine.

Wanahabari wamkumbuka Profesa Maji Marefu kwa ukarimu na ukaribu wake kwao

$
0
0

Na Benny Kisaka
Marehemu Profesa Maji Marefu alikuwa rafiki sana wa wanahabari, ambapo alikuwa mstari wa mbele katika kuwa karibu nao katika shida na raha.
Mfano mmojawapo ni mwezi Novemba mwaka 2003 ambapo baada ya kukawama kiuchumi marehemu alijitolea kudhamini safari ya kwenda Nairobi, kuripoti mchezo kati ya Taifa Stars na Kenya kwa kutoa usafiri, chakula na malazi. Hakusita kufanya hayo mara tu baada ya kuombwa.
Katika picha hii Profesa Maji Marefu (mwenye kibandiko mstari wa mbele) anaonekana akiwa na baadhi ya waandishi hao katika hoteli ya Safari Park jijini Nairobi  ambako Stars walifikia wakiwa chini ya kiongozi wa msafara katibu wa kamati ya Muda ya FAT( sasa TFF) wakati huo  Mwina Mohamed Seif Kaduguda.
Wanahabari hao ni Masoud Sanani, Aboubakar Liongo, Benny Kisaka, Ibrahim Bakari, Eric Anthony, Peter Mwenda, Oscar Mbuza, Somoe Ng'itu, Mashaka Mhando, Ezekiel Malongo, Jesse John, Michael Maluwe, Ndembeju na Emmanuel Muga (sasa wakili msomi).

UZINDUZI WA MAONESHO YA SABASABA 2018, WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AWATAKA WAJASIRIAMALI KUCHANGAMKIA FURSA ZA BIASHARA

Tangazo la kifo CHICAGO Marekani na Mbokomu, Moshi

$
0
0
Profesa James K. Shaba anasikitika kutangaza kifo cha mke wake, Elizabeth E. Shaba, kilichotokea Chicago IL, Marekani. 
Marehemu, aliyekuwa na miaka 80 aliaga dunia Jumapili, tarehe 1 Julai, 2018 nyumbani kwake akiwa amezungukwa na watoto na wote waliompenda. 
 Marehemu alizaliwa Disemba 21, mwaka 1937 kijijini Mbokomu Moshi, Tanzania. Alikuwa ni mtoto wa tano kati ya watoto nane wa familia ya mzee Elisa Kileo Mrema na Anale Mhache Mrema. Habari hizi ziwafikie ndugu, jamaa na rafiki wote mahali popote walipo. 
Mazishi ya marehemu yatafanyika siku ya Jumamosi tarehe 7 Julai, 2018.

Anuani: Montclair-Lucania Funeral Home, 
6901 W. Belmont Ave 
Chicago IL, 60634
Muda ni saa 9 jioni, na kufuatiwa na sala saa 11 jioni. Wote mnakaribishwa.
Bwana alitoa, na Bwana ametwaa.
Jina la Bwana na lihimidiww
AMINA

Wakazi wa Mtoni Temeke, wapatiwa uhakika wa maji safi na salama

$
0
0
Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imefanikisha kuboresha uzalishaji wa maji katika mtambo wa Mtoni baada ya kununua na kufunga pampu mpya za kusukuma majighafi kutoka katika mto Kizinga.

Uzalishaji huo umeongezeka baada ya jumla ya pampu mbili zenye uwezo wa kusukuma maji kwa kiasi cha mita za ujazo 140 kwa saa kwa kila pampu moja ambazo zinafanya kazi kwa ufanisi.

Taarifa hiyo imetolewa jana jioni na ofisi ya uhusiano wa jamii DAWASA baada ya kumalizika kufungwa kwa mtambo huo uliogarimu jumla ya sh. Milioni 239.1

" kufungwa kwa pampu hizo kumeongeza uwezo wa kusukuma maji na hivyo kurejesha uwezo wa mtambo wa Mtoni kuzalisha maji kwa ajili ya wakazi na waty wenye viwanda katika eneo hilo la Temeke wanaopata maji kutoka katika mtambo huo". Imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Ameongeza kuwa, Mtambo wa Mtoni uliojengwa mwaka 1974, ndio mkongwe kuliko yote inayozalisha maji katika eneo la Huduma la DAWASA ukiwa unazalisha lita milioni tisa za maji kwa siku.
Aidha Msuya amevitaja vyanzo vingine vya maji vilivyopo DAWASA ni, Ruvu Juu, Ruvu Chini, na Visima Virefu vilivyopo katika maeneo mbali mbali jijini ambayo yanaweza kusaidia mahitaji ya maji jijini Dar, ambayo yanafikia Lita milioni 544 kwa siku.

Wafanyakazi wa NEMC wafikishwa Kizimbani

$
0
0
Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.

Wafanyakazi wa  NEMC na wenzao  wamefikishwa katika ma ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka nane ya uhujumu uchumi likiwemo la kughushi saini ya Waziri wa nchi ofisi ya makamo wa rais muungano na Mazingira,Januari  Makamba katika vyeti vya tathmini ya uharibifu wa Mazingira.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao jana Julai 4/2018 na wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga  mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde.

Washtakiwa  wametajwa kuwa ni Afisa wa Mazingira NEMC, Deusdith Bulamire (38) Mkazi wa Ubungo, Edna Lutanjuka, Sekretari wa Nemc,  Mwaruka Mwaruka (42) Mkazi wa Ukonga Mombasa na Mkaguzi kutoka ofisini ya CAG, Dauson Barwongeza Mkazi wa Dodoma.

Akisoma hati ya mashtaka wakili Katuga amedai kati ya Machi 28,2017 na Novemba 4,2018 Dar es Salaam washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la kughushi.

Washtakiwa Deusdith, Edna na Mwarukwa wanadaiwa, Oktoba 10,2017 Dar es Salaam kwa udanganyifu walighushi cheti cha tathmini ya uharibifu wa Mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 wakijaribu kuonesha kuwa cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewana NEMC wakati wakijua si kweli.

Washtakiwa hao, pia wanadaiwa kughushi cheti cha tathmini ya uharibifu wa Mazingira chenye usajili namba EC/ EIA/3365 wakijaribu kuonesha cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na NEMC wakati wakati wakijua si kweli.

Pia wanadaiwa kughushi saini ya Waziri Makamba kwenye cheti cha tathmini ya uharibifu wa Mazingira wakijaribu kuonesha sahihi hiyo ni ya Waziri huyo wakati si kweli.

Katika shtaka la tano washtakiwa Deusdith, Edna na Mwarukwa walighushi saini ya Waziri Makamba katika cheti cha tathmini ya uharibifu wa mazingira wakijaribu kuonesha sahihi hiyo ni ya  Waziri huyo wakati si kweli.

Katika shtaka la sita mshtakiwa Edna anadaiwa kuwa Novemba 2017 katika ofisi za NEMC Makao Makuu Dar es Salaam kwa kujua alitoa cheti cha kughushi cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3365 cha Oktoba 16,2017 kwa E 2598 D/CPL David wakijaribu kuonesha ni halali na kwamba kimetolewa na NEMC.

Katika shtaka la saba, imedaiwa kuwa kati ya Machi 28 na Novemba 4,2017  washtakiwa hao walijipatia sh. milioni 30 kutoka kwa F1195 CPL Yohana Mtweve kwa kudai kuwa wangeweza kufanya tathimini ya uharibifu wa mazingira na kumpatia cheti ambacho kinatolewa na NEMC huku wakijua kuwa si kweli.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa kuwa kuisababishia NEMC hasara ya Sh milioni 20.

Washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande  mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Washtakiwa wamepelekwa rumande hadi Julai 18,2018 kwa ajili ya kutajwa.

GPSA YAUNGA MKONO JUHUDI ZA KUTOA ELIMU BURE KWA KUSAIDIA VIFAA VYA KUFUNDISHIA KWA SHULE ZA MSINGI, SEKONDARI

$
0
0

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

WAKALA wa Huduma ya Ununuzi Serikalini(GPSA)umetoa msaada wa vifaa vya kufundishia kwa shule za msingi na sekondari wenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni tisa.

Umefafanua kuwa wanatambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli ya kutoa elimu bure,hivyo wameamua kuunga mkono juhudi hizo kwa vitendo kwa kutoa msaada huo.

Akizungumza leo katika Shule ya Msingi Kilimahewa iliyopo wilayani Temeke jijini Dar es Salaam Kaimu Mtendaji Mkuu wa GPSA Lilian Mwinuka amefafanua utoaji wa msaada huo pia ni sehemu ya kuadhimisha miaka 10 tangu wakala huo ulipoanzishwa. Amefafanua kutokana na kutimiza miaka 10 tangu kuanza kwa wakala huo wameona ipo haja ya kurudisha shukrani kwa jamii na wakaona haja ya kusaidia vifaa vya kufundishia.

"Kwa leo tumekabidhi msaada huo wa vifaa vya kufundishia kwa shule nne za Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam. Tumekabidhi kwa shule hizi kwa niaba ya shule zote za Dar es Salaam."Nijukumu letu kurudisha fadhila na shukrani zetu kwa jamii na tumeona tutoe vifaa vya kufundishia shuleni. Ni jukumu letu kuunga mkono uamuzi wa Serikali wa kutoa elimu bure,"amesema Mwinuka.

Ametaja baadhi ya msaada ambao wameutoa ni chaki, daftari, ufutio wa ubaoni, kalamu, na vifaa vya kuhifadhia taka. Mwinuka ameongeza baada ya kutoa msaada huo Dar es Salaam watakwenda kutoa msaada kama huo wa vifaa kwa shule zilizopo mkoani Dodoma siku za karibuni. Akizungumzia kuhusu GPSA Mwinuka amesema vifaa ambazo wanauza bei yake iko chini ukilinganisha na maeneo mengine kwasababu wao hawapo kwa ajili ya kupata faida kubwa.

Hivyo amewashauri Watanzania kwenda uununuzi kwao kwani mbali ya unafuu wa gharama pia ziko imara."Bidhaa zetu ni bora na zinapatikana kwa bei nafuu, sababu kubwa sisi tunaagiza moja kwa moja kwa wazalishaji, hivyo bei yetu ni yakawaida,"amesema. Hivyo amewahamiza Watanzania kununua bidhaa zao na kufafanua kauli mbiu yao inasemaje "Okoa fedha za umma kwa kufanya ununuzi kupitia GPSA.

Kwa upande wao baadhi ya walimu kutoka shule ambazo wamepatiwa msaada huo wakiongozwa na Kaimu Ofisa Elimu wa Wilaya Bakari Mnondwa wameahukuru kwa msaada huo. Pia ameomba wadau wengine nao kusaidia sekta ya elimu na kufafanua msaada ambao wameupata umeongezeka chache ya wao kufanyakazi ya kufundishia kwa amri zaidi.

Kuhusu changamoto ambayo wanakabilana kwa Wilaya yake Temeke ni uhaba wa vyumbo vya madarasa 2,162 huku idadi ya wanafunzi wa shule ni 161,313.


.Kaimu Mtendaji Mkuu wa GPSA LIlian Mwinuka akikabihi vifaa kwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Karume iliyopo wilayani Temeke jijini Dar es Salaam Hillgaro Lwambusha.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kilimahewa, walimu wa shule nne ambazo zimekabidhiwa msaada huo pamoja na uongozi wa GPSA ukiongozwa na Kaimu Mtendaji wao Mkuu wakiwa katika picha ya pamoja.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) Lilian Mwinuka(kulia) akizungumza katika Shule ya Msingi Kilimahewa baada ya kukabidhi msaada wa vifaa vya kufundishia kwa shule za msingi wenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni tisa.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa GPSA LIlian Mwinuka (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wengine baada ya kukabidhi msaada wa vifaa vya kufundishia kwa shule za msingi na sekondari ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kutoa elimu bure.

Watumishi Muhimbili Wapigwa msasa Kuhusu Maadili, Rushwa

$
0
0
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeendesha mafunzo ya siku mbili ambayo yamelenga kuwakumbusha watumishi wa hospitali hiyo kuzingatia sheria ya kupambana na rushwa mahali pa kazi sambamba na maadili katika utumishi wa umma.
Watumishi walikumbushwa kutojihusisha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa pamoja na madhara yanayotokana na vitendo hivyo.  
Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Bw. Steven Agwanda aliwataka watumishi wa hospitali hiyo kuzingatia maadili kwa sababu makosa mengi ya rushwa yanasababishwa na ukiukwaji wa maadili.
“Kuna uhusiano mkubwa kati ya rushwa na maadili, mtumishi au viongozi hawachukui rushwa kwa sababu hawana hela, hapa tatizo ni ukosefu wa maadili, zikiwamo tamaa ambazo zinasababishwa na watumishi au viongozi,” alisema Agwanda.
Mafunzo hayo ya siku mbili yalifunguliwa na Mkuu wa Idara ya Ajira na Mafunzo, Bw. Abdallah Kiwanga na yaliwalenga wakuu wa vitengo na wasimamizi wa wodi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
 Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Bw. Steven Agwanda akitoa mada katika semina ya siku mbili kuhusu rushwa mahali pa kazi kwa watumishi wa umma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
 Sehemu ya watumishi wa umma wa Muhimbili wakimsikiliza mtoa mada kwenye semina hiyo.
Sehemu ya watumishi wa umma wa Muhimbili wakimsikiliza mtoa mada kwenye semina hiyo.

Halmashauri yatenga Millioni 370 kuchimba Visima katika Vijiji 16 Tarime.

$
0
0
Na Frankius Cleophace Tarime.

Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini Mkoani Mara,  imeanza rasmi kazi ya kuchimba Visima Virefu Vya Maji katika Vijiji 16 kati ya Vijiji 88 vyenye thamani ya Shilingi Millini 370, kwa lengo la kupunguza adha ya upatikanaji wa Maji na akina Mama kutembea umbali mrefu ili kutafuta Maji.

Moses Misiwa Yomami ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini amesema kuwa katika Mwaka wa fedha 2016-2017 Halmashauri ilitenga kiasi cha Fedha Mill 150 lakini kwa ajili ya kuchimba Visima Vijiji vya Matongo na Kemambo lakini zoezi hilo halikufanikiwa kwa sababu ya ukosefu wa pesa zilizotengwaambapo Mwaka wa Fedha ambao unamalizika 2017-2018 wametenga Kiasi cha Shilingi Millioni 370 na Vijiji 16 kati ya 88 Vinaenda kunufaika na Mradi wa Kuchimba Visima Vya Maji.

“Tuna Mikaba Miwili hapa Kuna Mkataba wa Visima Nane Virefu vya pampu Vyenye Thamani ya Shilingi 204 katika Vijiji Nane na Mkataba wa Pili Visima Shilingi Mill 170 ambapo jumla ya fedha tunazitoa kwa ajili ya Uchimbaji wa Visima kupitia Mapato ya ndani itakuwa Jumla ya Shilingi 370” alisema Misiwa.

Yomami ametaja kuwa Vijiji 16 katika Halmashauri hiyo vitanufaika na Mradi kuwa ni Gibaso, Kitawasi, Mutana, Surubu, Nyantira, Boga A Kwisarara na Mangucha pia katika mkataba wa Pili Vijiji Vitakavyonufaika ni Weigita, Nyamirambaro, Mutana, Kimusi, Kewanja, Mjini Kati na Nyangongo jumla Vijiji 16 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini.

Licha ya Serikali kuletea Maendeleo Wananchi wananchi hao wamekuwa wakidai fidia pale Miradi inapopita ambapo Mwenyekiti amessma kuwa wananachi wamekubali Miradi hiyo hivyo hakuna haja ya kuomba Fidia pale miradi inapofanyika.

Yomami ameongeza kuwa Nyuma kampuni iiyopewa kazi ilikuwa ikifanya Utafiti na kuchukua Mchanga na Kampuni nyingine inakuja kuchimba ikikosa Maji wanashindwa kuwabana kwa madai wao hawakufanya utafiti kazi yao ilikuwa ni Kuchimba Maji lakini kwa Mikaba iliyotolewa kwa sasa imeboreshwa anayechimba Visima hivyo ndiye atakayefanya Utafiti wa eneo lenye maji hiyo yakikosa lazima awajibike yeye mwenyewe na siyo mtu mwingine.

Mwenyekiti amesisitiza Wananchi kulinda Miundombinu ya Maji itakayojengwa Maeneo tofauti kwani Miradi ya Maji imekuwa ikiharibika kwa sababu ya kuaribu Miundombinu hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Moses Misiwa Yomami akiwa ofisi kwake baada ya Kuongea na Vyombo vya habari kuhusu Mradi huo wa kuchimba Visima hivyo.

WAZIRI KIGWANGALLA AAGIZA TFS KUCHANGIA MILIONI 20 KWA AJILI YA UJENZI WA ZAHANATI SUMBAWANGA

$
0
0



Na Hamza Temba, Rukwa

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS kuchangia shilingi milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Ametoa agizo hilo kufuatia taarifa iliyowasilishwa kwake na Mtendaji wa Kata ya Majengo, Matage Bikaniko Mjarifu alipotembelea kijiji hicho kinachopakana na Msitu wa Mbizi ambapo amesema wananchi wa kijiji hicho husafiri umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 11 kwa ajili ya kufuata huduma za afya mjini Sumbawanga.

Amesema mpaka sasa wananchi wa kijiji hicho wameshachangia shilingi laki 9 na Mbunge wa Sumbawanga mjini shlingi milioni 5. Hata hivyo amesema jumla ya shilingi milioni 134 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.Kufuatia taarifa hiyo, Waziri Kigwangalla alisema Wizara yake kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS itachangia shilingi Milioni ishirini hivyo wananchi wapambane kwa kushirikiana na halmashauri yao ili jengo hilo lisimame na hatimaye fedha hizo ziwasilishwe kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake. 

Alisema Falsafa ya Uhifadhi Endelevu ni Uhifadhi Shirikishi Jamii, hivyo wizara yake itaendelea kusimamia sera ya kuhakikisha wananchi hususan wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi wananufaika moja kwa moja na hifadhi hizo kupitia miradi ya maendeleo.Dk. Kigwangalla ameziagiza taasisi zote za uhifadhi nchini kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii ili wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hizo waone umuhimu wa hifadhi hizo moja kwa moja na hivyo kutoa ushirikiano kwenye uhifadhi.

Katika hatua nyingine, Waziri Kigwangalla amemsimamisha kazi Meneja wa Pori la Akiba Uwanda, katika wailaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Mark Chuwa kwa tuhuma za kushindwa kuondoa mifugo zaidi ya 12,000 iliyopo ndani ya hifadhi hiyo.

Kabla ya uamuzi huo, akisoma taarifa ya mkoa kwa Waziri huyo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Khalfan Haule alisema uvamizi katika pori hilo umekuwa wa kiasi kikubwa ambapo wafugaji huingia na makundi makubwa ya mifugo na kugeuza eneo hilo sehemu ya malisho.Alisema licha ya na kufanyika kwa opresheni za mara kwa mara za kuondoa mifugo hiyo, baada ya muda mfupi wafugaji hao hurejea na makundi makubwa ya mifugo kwa ajili ya malisho.Hata hivyo Dk. Kigwangalla alishangazwa na uongozi wa mkoa na wilaya kwa kushindwa kuchukua hatua za kuondoa mifugo hiyo hifadhini wakati sheria za uhifadhi haziruhusu mifugo hifadhini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa mkoa wa Rukwa wakikagua eneo shamba la miti kwenye Msitu wa Mbizi wilayani Sumbawanga jana. Aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda.
Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia eneo linalojengwa zahanati ya kijiji cha Mponda ambayo ameahidi wizara yake kuchangia ujenzi wake wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wilayani Sumbawanga jana. Ambapo aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda. Wapili kulia kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Khalfan Haule. 
Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwapungia mkono wananchi wa kijiji cha Mponda katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wilayani humo jana. Aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda. Kulia kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Khalfan Haule.

HABARI ZAIDI BOFYA HAPA

RC TEMEKE AWAMWAGIA SIFA WOISO ORIGINAL PRODUCTS KWA KUNYAKUA TUZO YA BIDHAA ZA NGUO NA NGOZI

$
0
0
Na Leandra Gabriel , Globu ya Jamii.

MKUU wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva amewataka wananchi hasa watokao katika Manispaa ya  Temeke kujitokeza kwa wingi kushuhudia maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba ili kujipatia elimu ya ujasiriamali.

Lyaniva ametembelea mabanda mbalimbali katika maonesho hayo na kujionea kazi za wazalendo wakiwa na bidhaa tofauti zilizotengenezwa hapa nchini wakitilia mkazo kauli ya Rais wa John Pombe Magufuli ya uchumi wa viwanda.

Akizungumza na Globu ya Jamii akiwa ndani  ya banda la bidhaa za nguo na ngozi la Woiso Orginal Company Ltd Lyaniva ameeleza kuwa maonesho hayo yameboreshwa na washiriki wamekuwa wengi kutoka katika nchini mbalimbali duniani.

"Maonesho ya mwaka huu zaidi ya mataifa 50 kutoka nje ya nchi wameweza kushiriki na wameleta bidhaa bidhaa nzuri zikiwa zenye ubora wa hali ya juu,"amesema Lyaniva.

Lyaniva amewapongeza wazalishaji wa bidhaa za nguo na ngozi kutoka kampuni ya Woiso Original Products kwa kuzalisha bidhaa nzuri na zenye ubora wa hali ya juu na kwa bei nzuri ambayo unanunua kitu na utadumu nacho kwa mda mrefu na amewataka wananchi kujitokeza sasa kuona na kujifunza namna bidhaa za kitanzania hasa za ngozi zilivyoshika hatamu kwa ubora wa hali ya juu.

Aidha amewashukuru watanzania walioelewa na kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika masuala ya kiuchumi na wamekuja vizuri sana na kuboresha maonesho hayo ambayo kwa namna moja au nyingine yana tija kwa taifa letu.

Naye Meneja masoko wa Woiso Original Products Company Ltd bi. Teya Herman ameeleza kuwa wao kama kampuni wanajituma sana katika kuhakikisha wanatoa bidhaa bora za ngozi na nguo kama vile viatu, mikanda, pamoja na nguo na mapazia.

Kuhusu tuzo waliyokabidhiwa leo wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kassim ya watayarishaji bora wa bidhaa za nguo na ngozi bi. Teya ameeleza kuwa ni mara yao ya 4 kushiriki maonesho hayo na ni mara ya 4 kushinda tuzo hiyo ambapo awali ilijikita katika bidhaa za ngozi na ila kwa sasa imejumuisha bidhaa za ngozi na nguo.

Akielezea changamoto wanazokutana nazo hasa kwenye upatikanaji wa ngozi bi. Taya amesema kuwa upatikanaji wa bidhaa hiyo hauko vizuri  kutokana na uwepo wa alama zilizowekwa na wafugaji na zile zinazotokana na kuchinjwa hali inayopelekea ugumu wakati wa kuandaa bidhaa hizo.

Na ameungana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke akiwaomba watanzania kuunga mkono juhudi za serikali katika kuelekea uchumi wa viwanda kwa kupenda vya nyumbani.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva akimuelezea mwananchi aliyefika kwenye banda la Woiso Original Products Company Ltd wanaojihusisha na uuzaji wa bidhaa za nguo na ngozi wakiwa washindi kwenye kipengele hicho kwa mara ya nne mfululizo katika maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba 
Meneja Masoko wa Kampuni ya Woiso Original Products Ltd Teya Herman akieleza jambo kwa mkuu wa  Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva katika maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva akieleza jambo kwa Meneja Masoko wa kampuni ya Woiso Original Products Ltd Teya Herman  alipotembelea banda hilo na kujionea bidhaa zinazotengenezwa na watanzania zikiwa zenye ubora katika maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba
Meneja Masoko wa kampuni ya Woiso Original Products Ltd Teya Herman akizungunza na Globu ya Jamii akielezea tuzo ya ushindi waliyoipata katika kipengele cha Bidhaa za nguo na ngozi kutoka Tanzania ikiwa ni mara ya nne mfululizo wakishinda katika maonesho ya 42 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva akizungumza na Globu ya Jamii akiwa ndani ya banda la washindi wa bidhaa za nguo na ngozi akielezea umuhimu wa watanzania kupenda vitu vya nyumbani ikiwemo kuwaunga mkono Wazalishaji wa ndani wa Viwanda vidogo na vikubwa.

Picha na Emmanuel Massaka Globu ya jamii)

WCF YAWAHIMIZA WAAJIRI NCHINI KUCHANGIA MFUKO HUO KWA WAKATI

$
0
0
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi(WCF) Masha Mshomba amewasisitiza waajiri wote nchini kulipa michango yao katika mfuko huo kwa wakati.

Pia ameelezea namna ambavyo mfuko huo ufurahishwa na hatua ambazo zinachukuliwa na viongozi wa ngazi za juu katika Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhimiza wajajiri kuchangia.

Akizungumza leo katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam Mshomba amesema kuwa hamasa ambayo viongozi wa Serikali wanayo katika kuhimiza waajiri kuchangia mfuko huo imefanya waajiri wengi kuchangia kwa wakati.

“Ukweli tunapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa Serikali kwa ngazi mbalimbali.Hivyo imekuwa rahisi kwa waajiri kuelewa na kutoa kuchangia mfuko.“Waajiri ambao hawachangii mfuko ni wachache na sheria inaturuhusu kuwachukulia hatua lakini tunachofanya ni kuendelea kuwahimiza na kuwalimisha na wale ambao tutaona hawataki kulipa basi tutachukua sheria,”amesema Mshomba.

Kuhusu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi amesema ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 Sheria ya fidia kwa wafanyakazi.Amesema lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara ambao wataumia , kuugua ama kufariki kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao.

Akitaja mafao ya mfuko huo amesema kuna mafao ya Huduma ya matibabu, malipo ya ulemavu wa muda, malipo ya ulemavu wa kudumu, malipo kwa anayemhudumia mgonjwa, huduma za ukarabati na ushauri nasaha , msaada wa mazishi na malipo kwa wategemezi.

Kuhusu walengwa wa mafao Mshomba amesema walengwa ni wafanyakazi ambao wataumia au kuugua kutokana na kazi walizoajiriwa nazo.Pia wategemezi wa mfanyakazi atakayefariki kutokana na ajali au ugonjwa uliotokana na kazi.

Pamoja na hayo amesema mfuko huo umekuwa msaada mkubwa katika kuwahudumia wafanyakazi na kwamba kwa upande wao wanatumia siku 30 tu katika kulipa mafao na kubwa zaidi ambacho wanajivunia ni namna ambavyo wanatumia mtandao katika kutekeleza majukumu yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw.Masha Mshomba akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Tathmini na Tiba Dk. Abdulssalaam Omary wakati alipotembelea katika banda la taasisi hiyo lililopo kwenye viwanja vya maonesho vya Sabasaba barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam leo, Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Fedha, Mipango na Uwekezaji Bw. Bezil Ewala na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Bi. Laura George .
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw.Masha Mshomba akizungumza na waandishi wa habari wa kituo cha luninga cha Chanel Ten wakati alipokuwa akieleza mikakati mbalimbali ya shirika hilo kwa ajili ya wastaafu.
Baadhi ya wafanyakazi mbalimbali wakiwa katika banda la shirika hilo tayari kwa kuhudumia wateja mbalimbali wanaotembelea katika maonesho ya Sabasaba.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw.Masha Mshomba katikati Mkurugenzi wa Tathmini na Tiba Dk. Abdulssalaam Omary kushoto na Mkurugenzi wa Fedha, Mipango na Uwekezaji Bw. Bezil Ewala wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi walioko katika banda hilo ili kuwahudumia wananchi wanaotembelea banda hilo.
Baadhi ya wafanyakazi wakiwa katika picha ya pamoja nje ya banda hilo.

WANANCHI WAFURIKA KWENYE BANDA LA MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA) SABASABA

$
0
0
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA Bi. Rose Joseph akimsikiliza mmoja wa wananchi waliofika kwenye banda la mamlaka hiyo kwa ajili ya kujiandikisha na kupata kitambulisho chake cha taifa alipotembelea kwenye banda hilo katika maonesho ya biashara ya Sabasaba viwanja vya TANTRADE barabara ya Kilwa jijini Dar es salaam leo. 
Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye misururu mirefu wakipata huduma ya vitambulisho vya taifa katika banda la Mamlaka ya Vitambulisho NIDA kwenye maonyesho ya Sabasaba leo.
Baadhi ya wafanyakazi wa NIDA wakiwapatia huduma ya vitambulisho wananchi waliotembelea katika banda hilo ili kupata vitambulisho vya taifa.
Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho NIDA wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kazi ya kutwa nzima wakihudumia wananchi kwenye maonesho hayo leo.

NIC KIDEDEA SABASABA, YANYAKUA TUZO MBILI KWA MPIGO

$
0
0


Big Boss: Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Sam Kamanga akiwa amebeba vikombe vya mshindi wa kwanza katika sekta ya bima (kushoto), na cha ushindi wa pili (kulia) katika washindi wa jumla miongoni mwa washiriki wa maonyesho hayo ya 42 ya sasasaba yanayoendelea katika viwanja vya mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Sam Kamanga kikombe cha mshindi wa kwanza katika sekta ya bima , NIC pia imekuwa mshindi wa pili katika washindi wa jumla miongoni mwa washiriki wa maonyesho hayo ya 42 ya sasasaba yanayoendelea katika viwanja vya mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam
Vigogo NIC:Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Bima za Mali,Ajali na Shehena Romanus Hokororo,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NIC Thomas Msongole,Mkurugenzi Mtendaji wa NIC Sam Kamanga na Kaimu Mkurugenzi wa Masoko Elisante Maleko
Picha ya pamoja, wafanyakazi wa NIC waliosimama mbele na viongozi wao mstari wa nyuma

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje atembelea maonesho ya 42 ya biashara ya kimataifa (sabasaba)

$
0
0
Mhe. Dkt. Susan Kolimba Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akisaini kitabu cha wageni kwenye banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Bi. Mindi Kasiga pamoja na watumishi wa Wizara. 

Dkt. Kolimba alifurahishwa na ushiriki wa Wizara kwenye maonyesho ya sabasaba, ambapo aliwasisitiza watumishi wa Wizara kuendelea kutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wizara. 
Mhe.Dkt. Kolimba akipata maelezo kutoka kwa Bi. Mindi Kasiga 
Mhe. Dkt. Susan Kolimba akizungumza na watumishi alipotembelea banda la Wizara kwenye maonesho ya sabasaba 
Mkurugenzi wa Masomo wa Chuo cha Diplomasia Prof. Watengere Kitojo akizungumza na watumishi alipotembelea Banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye maonesho ya sabasaba . 
Wanafunzi kutoka Chuo cha Diplomasia wakipata maelezo kutoka kwa watumishi wa Wizara walipotembelea bandala kwenye maonesho ya saba.Wanafunzi hao walipata fursa ya kuelezwa kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kikanda na kimataifa sambamba na fursa na faida zinazopatikana. 
Bw. Teodos Komba Afisa Mawasilino, akielezea jambo kwa wananchi waliojitokeza kwenye banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 
Bw. Hassan Mnondwa akielezea jambo kwa wananchi waliotembelea banda la Wizara. 
Mhe.Dkt. Susan Kolimba akiwa katika Picha ya pamoja na Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alipotembelea banda la Wizara 

KANGI LUGOLA NA MHANDISI ISAAC KAMWELWE WATEMBELEA ENEO LA AJALI NA MAJERUHI WA AJALI ILIYOTOKEA MLIMA IWAMBI JIJINI MBEYA

$
0
0
 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia), akimjulia hali mmoja wa majeruhi  aliyelazwa  katika Hospitali ya Rufaa Ifisi, ajali hiyo  iliyotokea hivi karibuni, katika eneo la Mlima Iwambi,jijini Mbeya.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac  Kamwelwe (kushoto),na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati), wakimjulia hali mmoja wa majeruhi aliyelazwa katika Hospitali Teule ya  Mbalizi, ajali hiyo iliyotokea hivi karibuni, katika eneo la Mlima Iwambi,jijini Mbeya.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza na wananchi katika eneo la Mlima Iwambi,jijini Mbeya, ambako hivi karibuni kumetokea ajali iliyosababisha vifo na majeruhi.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

 Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Dkt. Louis Chomboko, akitoa taarifa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Kangi Lugola(kulia) na  Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac  Kamwelwe (katikati) ,juu ya hali  za majeruhi wa ajali waliolazwa katika Hospitali ya  Teule Mbalizi, ajali hiyo  iliyotokea hivi karibuni katika eneo la Mlima Iwambi,jijini Mbeya.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akisalimiana na watumishi wa afya baada ya kuwasili Hospitali ya Teule Mbalizi, kuwajulia hali majeruhi wa ajali iliyotokea katika eneo la Mlima Iwambi,jijini Mbeya.

WAZIRI UMMY AFANYA KIKAO NA GLOBAL FUND

$
0
0
Mfuko wa Pamoja wa Dunia wa kushughulikia magonjwa ya TB,Maralia na Ukimwi (GLOBAL FUND) umeridhishwa kwa kiasi kikubwa na Jinsi Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya katika kupambana na magonjwa hayo.
Pamoja na hayo Wawakilishi wa Mfuko huo hapa Nchini wamesema kuwa kutokana na mwenendo mzuri wa Tanzania katika kutumia viozuri Mfuko huo sasa wanaweza kuanzisha kitu kingine kizuri kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya na kupeleka mapendekezo na kukubaliwa.
Malengo ya kikao hiko kikao kati ya Mfuko wa Pamoja wa Dunia wa kushughulikia magonjwa ya TB,Maralia na Ukimwi (GLOBAL FUND) na Wizara ya Afya ni kujadili ,kupanga na kuboresha Sekta ya Afya nchini.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa kikao na wawakilishi wa Mfuko wa Pamoja wa Dunia wa kushughulikia magonjwa ya TB,Maralia na Ukimwi(GLOBAL FUND)  hawapo pichani kilichofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es salaam.
 Mkurugenzi wa Mfuko wa Pamoja wa Dunia wa kushughulikia magonjwa ya TB,Maralia na Ukimwi (GLOBAL FUND)  hapa nchini Dkt. Sai Kumar kulia akimueleza jambo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao cha kujadili mambo mbalimbali ya afya kilichofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kulia  akizungumza na Naibu Waziri wake Dkt. Faustine Ndugulile kushoto wakati wa kikao na wawakilishi wa Mfuko wa Pamoja wa Dunia wa kushughulikia magonjwa ya TB,Maralia na Ukimwi (GLOBAL FUND)  hawapo pichani kilichofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katikati akizungumza wakati wa kikao na wawakilishi wa Mfuko wa Pamoja wa Dunia wa kushughulikia magonjwa ya TB,Maralia na Ukimwi (GLOBAL FUND) kilichofanyika katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es salaam. Kulia ni Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile.
PICHA NA WIZARA YA AFYA.

Watafiti wa afya waombwa kubaini sababu ya wanaume kukwepa kupima VVU

$
0
0
Naibu Waziri wa Afya , Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile ametoa wito kwa watafiti wa afya nchini kufanya utafiti ili kubaini sababu na suluhisho kuhusiana na uwepo wa idadi ndogo ya wanaume wanaojitokeza kupima virusi vya Ukimwi (HIV) hapa nchini.

Dk Ndugulile alitoa wito huo jijini Dar es Salaam jana wakati akifunga Mkutano wa sita wa kisayansi ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS).

Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2016/2017 ulioangalia maambukizi mapya na kiwango cha kufubaza VVU, wanawake wanaongoza katika maambukizi mapya lakini ni wepesi kupima na kutumia dawa kikamilifu ikilinganishwa na wanaume.

“Lengo hasa tunahitaji kuona idadi kubwa ya wanaume ikijitokeza kupima VVU ili tuweze kupunguza kasi ya maambukizi mapya ifikapo 2030. Ili tuweze kufanikisha hili ni lazima tuwe na majibu ya kitafiti yatakayotupa muongozo kuhusu sababu za wanaume kukwepa kupima VVU na nini hasa kifanyike kuondoa changamoto hizo,’’ alisema.

Alisema kwasasa serikali ipo kwenye mchakato wa kuandaa sera ya afya hivyo tafiti mbalimbali kuhusu masuala ya afya ni muhimu ili kuiwezesha sera hiyo kuhakisi ualisia wa masuala muhimu katika sekta hiyo.

Naibu Waziri wa Afya , Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile (kulia) akizungumza wakati akifunga Mkutano wa sita wa kisayansi ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS)jijini Dar es Salaam jana.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Prof Andrew Pembe (wa pili kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Afya , Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile (katikati) kuhusu dawa zinazaondaliwa na wataalamu wa Kitengo cha Dawa asili kutoka Chuo cha MUHAS muda mfupi kabla hajafunga Mkutano wa sita wa kisayansi ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS)jijini Dar es Salaam jana. Wengine ni pamoja na Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa (wa tatu kulia)
Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Prof Andrew Pembe akizungumza wakati wa kuhitimisha Mkutano huo
Naibu Waziri wa Afya , Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi wa huo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) mara tu baada ya kufunga Mkutano wa sita wa kisayansi ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS)jijini Dar es Salaam jana.
Naibu Waziri wa Afya , Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi wa huo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa sita wa kisayansi ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS)jijini Dar es Salaam jana.

Airtel yazindua Hakatwi MTU HAPA –Tuma Pesa Bure kupitia Airtel Money

$
0
0
Kampuni ya simu za mkononi inayoongoza kwa utoaji wa huduma bora za Smartphone Airtel Tanzania kupitia huduma yake ya Airtel Money leo imetangaza na kuzindua huduma mpya kwa wateja wote wanaotumia huduma ya kutuma na kupokea pesa kupitia Airtel Money kwa sasa wataweza kutuma na kupokea pesa bure bila ya makato yoyote.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam kwa niamba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo Mkurugenzi wa Masoko wa Airtel Isack Nchunda alisema, “Tunayo furaha kubwa kuona ungezeko la watumiaji wa Airtel Money kila siku, tunaamini ya kuwa malengo ya serikali ya kuhakikisha inafanikisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa kila mwananchi linaelekea kupata mafanikio makubwa. Leo Airtel tunazindua huduma hii inayojulikana kama HAKATWI MTU HAPA – Tuma Pesa Bure ili kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali na kuwawezesha wateja wetu zaidi ya milioni 10 nchini kuweza kutuma na kupokea Pesa BURE”.

“Mwaka jana Airtel tulizindua huduma ya ya kutuma na kupokea pesa bure kwa wateja wa Airtel Money wanaotuma pesa kuanzia 200,000 na kuendelea. Tumezingatia tena uhitaji wa wateja wetu wengi hivyo kupitia HAKATWI MTU-Tuma Pesa Bure tunaamini wale wanaotuma pesa chini ya hapo wataweza kufurahia huduma hii ya Bure.

 Ni imani yetu kwamba huduma ya tuma na pokea pesa bure kupitia Airtel Money itakuwa ni chachu kwa wale ambao sio wateja wa Airtel Money kuanza kutumia huduma hii salama, rahisi na ya uhakika,  Tunategemea kuona wateja wakichangamkia  Fursa hii ya kutuma na kupokea pesa bila makato yoyote ili  kuokoa pesa  hadi Sh 5,000 kuanzia sasa”. alieleza Nchunda
Mkurugenzi wa Masoko Airtel Tanzania Isack Nchunda akiongea wakati wa kuzindua huduma inayojulikana kama HAKATWI MTU HAPA – Tuma Pesa Bure ambapo wateja wote wanaotumia huduma ya kutuma na kupokea pesa kupitia Airtel Money kwa sasa wataweza kutuma na kupokea pesa bure bila ya makato yoyote kwa kupinga *150*60# kisha changua tuma pesa bure.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Airtel Tanzania Beatrice Singano akiongea wakati wa kuzindua huduma inayojulikana kama HAKATWI MTU HAPA – Tuma Pesa Bure ambapo wateja wote wanaotumia huduma ya kutuma na kupokea pesa kupitia Airtel Money kwa sasa wataweza kutuma na kupokea pesa bure bila ya makato yoyote kwa kupinga *150*60# kisha changua tuma pesa bure.
Mkurugenzi wa Masoko Airtel Tanzania Isack Nchunda – kulia na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampuni wakionyesha bango baada kuzindua huduma inayojulikana kama HAKATWI MTU HAPA – Tuma Pesa Bure ambapo wateja wote wanaotumia huduma ya kutuma na kupokea pesa kupitia Airtel Money kwa sasa wataweza kutuma na kupokea pesa bure bila ya makato yoyote kwa kupinga *150*60# kisha changua tuma pesa bure.

Viewing all 110170 articles
Browse latest View live




Latest Images