HIVI karibuni Serikali kupitia Kamishina wa elimu Dk. Edicome Shirima ilitoa taarifa kwa umma ikizitaka shule binafsi kuwarejesha mara moja katika madarasa yao wanafunzi waliokaririshwa madarasa au kuhamishiwa shule zingine
Kwa kigezo cha kushindwa kufikia wastani uliowekwa na shule husika hadi kufikia tarehe 20 mwezi huu.
Taarifa hiyo inaeleza kitendo cha kuwakaririsha madarasa, kuwafukuza shule ama kuwahamisha wanafunzi ambao wamefaulu mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nne, Kidato cha Pili au ule wa Kidato cha Nne ni kwenda kinyume na Waraka wa Elimu Namba 7 wa mwaka 2004.
Kwa maoni yangu nasema hii inaweza kudhoofisha shule binafsi na huenda ukawa ni mkakati wa Serikali kutaka kujaribu kuleta uwiano baina ya shule binafsi na zile za umma jambo ambalo litachukua miaka mingi sana kutokea.
Walianza na ada elekezi na sasa hivi wamehamia kulazimisha wanafunzi wasikariri madarasa.Ingawa sikatai kuwa uendeshaji wa shule binafsi lazima uzingatie sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali,
Lakini binafsi naona kuna haja ya Serikali kuacha kuingilia baadhi ya mambo yanayofanywa na shule hizo binafsi.Ni lazima ifahamike kusoma shule binafsi siyo haki ya kila Mtanzania isipokuwa tu shule hizo zipo kwa ajili ya wale ambao watakubaliana na vigezo na masharti ya kujiunga na shule hizo ikiwemo uwezo wa kulipa ada na ufaulu.
Naomba ninukuu kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Suleiman Jaffo aliyowahi kuitoa hivi karibuni kwamba " hatutaziua shule binafsi kwa kuzifungia badala yake zitakufa zenyewe kwa kukosa wateja pale tutakapoboresha na kuimarisha mazingira ya shule zetu za umma”.