Na Richard Mwaikenda
SERIKALI imeutaka Ushirika wa Vibidar Namaingo kuanza kuzalisha mazao mengi kwa ajili ya malighafi ya viwanda vilivyopo na vinavyotarajiwa kuanzishwa nchini.
Ushauri huo ulitolewa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mary Mashingo wakati wa sherehe ya kukabidhi cheti kwa ushirika huo wa Vikundi vya Biashara Dar es Salaam (Vibidar), kwenye Uwanja wa Magereza, Ukonga.
Mashingo, aliipongeza Kampuni ya Namaingo Business Agency Ltd, kwa kuanzisha vikundi hivyo vya ujasiriamali na kuviatamia hadi kufikia kuunda ushirika wa Vibidar utakaoongeza viwango vya maarifa, taaluma pamoja na tija, jabo litakalowezesha wajasiramali wengi kuondokana na ujasriamali mdogo kwenda kwenye ujasiriamali mkubwa na hatimaye kuongeza pato la kaya na Taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa ushirika huu umekuja wakati muafaka, wakati Serikali ya Awamu ya Tano, imekuwa ikitoa kipaumbele katika kuhamasisha maendeleo ya sekta ya viwanda, ambapo sekta ya kilimo kupitia vikundi shirikishi inayo fursa kubwa ya kuweza kuzalisha malighafikwa ajili ya maendeleo ya viwanda.
"Ushirika wa vikundi mbalimbali kama Vibidar, vina uwezo wa kuzalisha malighafi ya kutosha kwa ajili ya kusindika mazao kutosheleza mahitaji ya viwanda, hivyo ushirika huu umeanzishwa katika muda muafaka wakati serikali inatilia mkazo katika kuchochea maendeleo ya sekta za kiuchumi zinazoweza kuchoche viwanda nchini," alisema Mashingo.
Mashingo, aliahidi serikali kuendelea kushirikiana na wadau kuimarisha ushirika ili kuzitatua changamoto mbalimbali kwa kutumia mikakati na mbinu za kila aina. Alizija baadhi ya changamoto zinaikabili sekta ya kilimo kuwa ni;uongezaji wa tija katika uzalishaji, mifumo ya soko yenye mpangilio mzuri, kujenga mitandao thabiti ya mawasiliano na kuwaunganisha wadau katika mlolongo wa thamani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mary Mashingo (katikati),akimkabidhi cheti Mwenyekiti wa Ushirika wa Vikundi vya Biashara Dar es Salaam (Vibidar Namaingo), Grace Lobulu katika sherehe iliyofanyika kwenye Uwanja wa Magereza, Ukonga juzi. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya ushirika huo, Ubwa Ibrahim.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mary Mashingo (katikati),akimkabidhi hati Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika wa Namaingo Vibidar, Ubwa Ibrahim.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mary Mashingo (katikati),akimkabidhi cheti Mwenyekiti wa Ushirika wa Vikundi vya Biashara (Vibidar Namaingo), Wilaya ya Kinondoni, Loiruck Mollel katika sherehe iliyofanyika kwenye Uwanja wa Magereza, Ukonga juzi. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya ushirika huo, Ubwa Ibrahim. (PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA)