Na Greyson Mwase, Mwanza.
Wadau mbalimbali wa vifaa ya umeme jua kutoka katika mikoa ya Mwanza na Kagera wamepongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kuanzisha mfumo mpya wa uhifadhi data na utoaji taarifa kwa ajili ya nishati jadidifu ujulikanao kama Tanzania Renewable Energy Management Information System (TREMIS) wenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji katika nishati jadidifu nchini.
Mfumo wa TREMIS unaratibiwa na Mradi wa Kuwajengea Uwezo Wataalam wa Nishati na Tasnia ya Uziduaji (CADESE) kwa kushirikiana na Idara ya Nishati, Wizara ya Nishati na Madini.
Wakitoa pongezi hizo katika kikao cha maandalizi ya mfumo huo kilichofanyika jijini Mwanza leo wamesema kuwa mfumo huo utawezesha shughuli za kampuni zao kufahamika ndani na nje ya nchi na kupata wabia wa kushirikiana nao katika bishara ya vifaa vya umeme jua.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmiliki wa kampuni ya kusambaza vifaa vya umeme jua ya Kaguta General Supplies yenye makazi yake Bukoba mkoani Kagera, Justin Kamlali amesema kuwa mfumo wa TREMIS utawawezesha kufahamika ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa biashara ya vifaa vya umeme jua imekuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutofahamika na kupelekea wateja kutokuwa na imani na huduma zao.
“Baada ya ya mfumo huu kukamilika na kuunganishwa na tovuti ya Wizara, wadau na wawekezaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi watakaotembelea tovuti ya wizara watapata fursa ya kuona taarifa za kampuni zetu na kuwa na imani ya kufanya kazi pamoja nasi tofauti na zamani”. Alisema .
Aliongeza kuwa kutokana na kampuni nyingi zinazojihusisha na biashara ya vifaa vya umeme jua kutokuwa na tovuti imekuwa ni vigumu kwa biashara zao kufahamika na watu wengi zaidi mbali na kutumia vyombo vya habari vilivyopo katika mikoa hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka kampuni ya Rex Energy, Francis Kibhisa alisema kuwa mfumo wa TREMIS ni mkombozi kwa wamiliki wa kampuni ndogo zinazojihusisha na vifaa vya umeme jua na nishati jadidifu ambapo watapata soko ndani na nje ya nchi kutokana na kufahamika kwao
Alisisitiza kuwa mfumo huo utawezesha wawekezaji kutoka nje ya nchi kufahamu maeneo ya uwekezaji zaidi katika eneo la nishati jadidifu na kuja kuwekeza nchini.
Mradi wa CADESE unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Maendeleo (UNDP) ulianzishwa mwaka 2014 na unatekelezwa na Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na wadau wengine kama Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taasisi ya Uongozi na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF). Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila akielezea faida za mfumo wa uhifadhi data na utoaji taarifa kwa ajili ya nishati jadidifu (TREMIS) mbele ya wadau wa nishati jadidifu (hawapo pichani)
Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila (mbele) akielezea faida za mfumo wa uhifadhi data na utoaji taarifa kwa ajili ya nishati jadidifu (TREMIS) mbele ya wadau wa nishati jadidifu.
Msimamizi wa Mradi wa Kuwajengea Uwezo Wataalam wa Nishati na Tasnia ya Uziduaji (CADESE), Paul Kiwele (kushoto) akifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa katika kikao hicho. Kulia ni Nasra Mohamed kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Sehemu ya wajumbe na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila (hayupo pichani)
Mtaalam kutoka Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Justin Chankan akiwasilisha rasimu ya mfumo wa TREMIS katika kikao hicho.
Wadau wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa katika kikao hicho