HATMA ya kuliondoa ama la, shitaka la nane la kutakatisha fedha haramu dhidi ya Kamishna Mkuu wa Zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake (pichani) wanaokabiliwa na mashitaka ya utakatishaji wa dola za Marekani milioni 6 mali ya Serikali kujulikana Aprili 27, mwaka huu.
Leo mahakama hiyo kutoa uamuzi huo lakini kwa sababu Hakimu Mkazi Mwandamizi, Emmilius Mchauru anayesikiliza kesi hiyo alipangiwa majukumu mengine ya kitaifa yaliyosababisha kushindwa kukamilisha kuandika uamuzi huo.
“Nawaomba radhi nimeshindwa kumaliza kuandika uamuzi kwa sababu nilipangiwa majukumu mengine ... mpaka kufikia Jumanne ijayo ntakuwa nimemaliza ntausoma uamuzi huo Jumatano ijayo” alisema Hakimu Mchauru.
Aprili 8, mwaka huu, Mawakili wa upande wa utetezi ukiongozwa na Dk. Ringo Tenga akisaidaiana na Alex Mgongolwa, Majura Magafu ulitoa hoja za kupinga uhalali wa kisheria wa shitaka la nane kwamba kifungu kilichotumika kinamapungu uliomba shtaka hilo lifutwe.
Akitoa hoja kuhusu mapungufu ya kisheria katika shitaka hilo, Wakili Mgongolwa alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 12 A cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), kinachoelezea shitaka hilo katika hati ya mshitaka yanayowakabili washtakiwa hakielezei kuhusu utakatishaji wa fedha haramu.
“Tunaomba tafsiri ya mahakama kuhusu kifungu cha 12 A kwa kuwa kinaeleza tofauti na hakihusiani na kuhamisha fedha lakini kifungu hicho kupia B kinaeleza kuhusu utakatishaji... ili kosa la utakatishaji fedha haramu likamilike lazima kuwe na A na B, sheria lazima ipewe tafsiri inayotakiwa” alidai Wakili Mgongolwa.
Alidai kuwa pamoja na mambo mengine, mahakama itumie mamlaka yake kutoa tafsiri inayotakiwa na kwamba ni rai yao upande wa utetezi shitaka la nane liondolewe katika hati ya mashitaka yanayowakabili washtakiwa kwa kuwa haliko kihalali katika hati hiyo.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Osward Tibabyekomya akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Shadrack Kimaro, Christopher Msigwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Stanlay Luoga.
Tibabyekomya alidai kuwa makosa yaliyopo kwenye kifungu cha 12 A cha CPA yanajitegemea na kwamba utakatishaji wa fedha haramu kifungu hicho kinaainisha makosa hayo.
“Kila hatua ya utakatishaji fedha haramu imeainishwa kwenye kifungu hicho inayokana na kosa lenyewe kwa kuwa sheria imeharamisha lengo ni kuzuia hata jaribio la utakatishaji wa fedha haramu... hoja za utetezi hazijitoshelezi kuhusu kuliondoa shitaka hilo, sisi upande wa Jamhuri hatuna pingamizi na ombi la kupata tafsiri sahihi ya kifungu hicho” alidai Tibabyekomya.
Mbali na Kitilya washtakiwa wengine ni, wafanyakazi wa Benki ya Stanbic Tanzania aliyekuwa Mrembo wa Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na mwanasheria wa benki hiyo Sioi Solomon.
Kufikishwa mahakamani kwa washtakiwa hao ni baada ya tuhuma za ufisadi zilizowahi kuibuka na serikali kupoteza zaidi ya Sh.trilioni 1.3.
Aprili Mosi, mwaka huu, Tibabyekomya aliwasomea washtakiwa hao mashitaka yao, alidai katika shitaka la kwanza kati ya Agosti 2012 na Machi 2013 ndani ya jiji la Dar es Salaam washtakiwa wanadaiwa kula njama ya kutenda makosa hayo.
Shitaka la pili hadi la tano yanamkabili Sinare, ilidaiwa kuwa Agosti 2, 2012 akiwa katika benki ya Stanbic Makao Makuu, kwa nia ya kudanganya alighushi hati ya mapendekezo ya uwezeshwaji wa kifedha ya tarehe hiyo kwa lengo la kuonesha kwamba,benki hiyo kwa kushirikiana na na benki ya Standard Bank ya Uingereza watatoa mkopo wa dola milioni 550 kwa serikali ya Tanzania kwa ada ya asilimia 2.4 ya mkopo huo huku akijua si kweli.
Sinare anadaiwa kwamba Agosti 13, 2012 katika ofisi za Wizara ya Fedha aliwasilisha hati hiyo.
Ilidaiwa kuwa Septemba 20,2012 akiwa katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic Tanzania iliyopo Wilaya ya Kinondoini, jijini Dar es Salaam Sinare, alighushi barua ya pendekezo la mkopo huo ya terehe hiyo akionesha kwamba Benki ya Standard Plc kwa kushirikiana na benki ya Stanbic wangetoa mkopo huo kwa serikali kama benki hizo zitapopewa kazi ya kutafuta mkopo huo kwa riba ya asilimia 2.4 huku akijua si kweli. Mshitakiwa huyo pia anadaiwa kuwasilisha nyaraka hiyo ya kughushi katika Wizara ya Fedha.
Shitaka la sita ilidaiwa kuwa Novemba 5, mwaka 2012 washtakiwa wote watatu wakiwa katika benki ya Stanbic Tanzania Makao Makuu kwa nia ya kudanganya walighushi mkataba wa ushirikiano wa tarehe hiyo kwamba Benki ya Stanbic Tanzania Limited imeanzisha ushirikiano na kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors (Egma) Limited kwa ajili ya kutafuta mkopo huo kwa serikali.
Ilidaiwa kwamba Egma pia ingewezesha na kuandaa mikutano na nyaraka mbalimbali ambazo zingetakiwa na mamlaka za Tanzania huku wakijua siyo kweli.
Upande huo wa Jamhuri ulidaiwa katika shitaka la saba, Machi 2013, ndani ya jiji la DaresSalaam,washtakiwa wote kwa udanganyifu,,walijipatia Dola za Kimarekani Milioni 6 Kwa serikali baada ya kudanganya kwamba fedha hizo ni ada ya malipo kwa kampuni ya Egma na benki ya Stanbic kwa kuwezesha serikali kupata mkopo wa Dola za Kimarekani Milioni 600.
Tibabyekomya alidai katika shitaka la nane, washtakiwa wanadaiwa kutakatisha fedha hizo kwa kuzihamishia katika akaunti mbalimbali ikiwamo 0240026633702, 0240026633701, na 9120001251935 zinazomilikiwa na Egma katika benki ya Stanbic na akaunti namba 3300605539 na 3300603692 ambazo pia zinamikikiwa na Kampuni ya Egma katika benki ya KBC wakati wakijua fedha hizo zimetokana na kosa la jinai la kughushi.
Washtakiwa walikana mashitaka yao kwa nyakati tofauti, upande wa Jamhuri upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.