Rais wa TFF, Leodegar Tenga (kulia) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo juu ya sakata la uchaguzi mkuu wa TFF,kwenye ukumbi wa mikutano uwanja wa taifa.
SAKATA la uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limefika patamu baada ya rais wa TFF, Leodegar Tenga kudai kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa walioenguliwa kuomba upya marejeo (review) ya rufaa zao.
Tenga ambae juzi alikuwa na kikao kizito na kamati zake za uchaguzi kabla ya leo asubuhi kuwa na kikao kingine Wizarani,alisema binafsi hana uwezo wa kutengua maauzi ya kamati zake kwa kuwa ni huru lakini yupo tayari kutoa muongozo kwa atakayetaka ili aweze kufanikiwa kupata haki yake.
Akizungumza na Wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Tenga alisema kuwa kwa mujibu wa katiba yua TFF kamati ya rufaa ndiyo ya mwisho katika maamuzi lakini mlalamikaji anaweza kuomba marejeo ili kutafuta haki yake.
"Jambo la kwanza mtu kama hajaridhika na uamuzi anaweza kuomba review(Marejeo) katika kamati ya rufaa, majibu yatakayopata kama hajaridhishwa tena anaweza pia kupeleka malalamiko yake Shirikisho la Soka la Dunia (fifa) na tatu ni kwenda CAS (mahakama ya usuluhishi).
"Jambo hili linazungumza kinazi zaidi watu hawaangalii katiba inasemaje, lugha za kejeli zimekuwa zikitumika kiasi kwamba maamuzi yaliyofanywa tunaonekana kana kwamba sisi wote ni wapumbavu, watu wanaotaka kutusaidia kukuza mpira wetu (wadhamani) hawawezi kuja kama kuna migogoro.
"Nipo tayari kufanya kila njia kuhakikisha tunatoa msaada kwa kila anayetaka kamati ya rufaa itakaa kesho kupitia review (marejeo) ya watu wawili ambao wameomba.
Tenga aliwataja walioomba marejeo ya rufaa hizo kuwa ni Jamali Malinzi ambaye alienguliwa kwa kigezo cha kukosa uzoefu wa miaka mitano kwenye masuala ya soka ikiwa ni pamoja na kupinga mabadiliko ya katiba ya TFF na Hamad Yahaya ambaye alienguliwa kuwania nafasi ya mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu.
"Sisi tupo tayari kutoa msaada kwa ambaye hajaridhishwa na uamuzi wa kamati ya rufaa kwa kuwaelekeza taratibu zinazotakiwa kufuata katika kutafuta haki zao wanatakiwa kujenga nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu,".alisema Rais huyo.
Kauli ya Tenga imekuja ikiwa ni siku chache baada ya kamati ya rufaa chini ya mwenyekiti wake Idd Mtiginjola kumuengua kwenye kinyang'anyiro cha urais katibu mkuu wa zamani wa Yanga Jamali Malinzi ambaye pia amepinga kuenguliwa kwake na tayari ameshawasilisha ombi lake la kutaka marejeo ya rufaa yake sambamba na mwenyekiti wa Mtibwa Sugar Hamad Yahaya ambaye naye alienguliwa kwenye kinyang'anyiro hicho ambacho alikuwa akiwania nafasi ya mwenyekiti wa bodi ya Ligi Kuu.
Wakati huo huo,Tenga alipangua hoja ya Katibu Mkuu wa zamani wa Fat sasa TFF Michael Wambura ambaye alidai katiba imesiginwa kwa TFF kuikiuka katika mchakato mzima wa kuifanyia mabadiliko.
Mapema wiki hii Wambura alitoa siku tatu kwa TFF kuhakikisha inaangalia upya suala la kuenguliwa kwa Jamali Malinzi na hadi Jumatatu kama rais Tenga angekuwa hajatoa kauli yoyote angeenda kufungua kesi mahakamani ili haki itendeke.
Alisema pia TFF ilikiuka katiba yao kwa kufanya marekebisho kwa njia ya waraka na pia kumdanganya msajili wa vyama vya michezo kuwa mkutano mkuu ulikaa Desemba 15 kitu ambacho si cha kweli huku kanuni za uchaguzi zikianza kutumika Januari 7 wakati katiba imepigwa muhuri wa msajili Januari 12 na kuiita katiba hiyo ni batili na mchakato mzima wa uchaguzi.
Akizungumzia suala hilo Tenga alisema "Kikao sio lazima tukae sasa hivi dunia imebadilika hata kwa njia ya mtandao watu mnafanya kikao tulitoa waraka kwa kupiga kura wanachama 70 walisema ndio na 33 wakasema hapana.
"Kamati yetu ya utendaji ndio ilipokea majibu ya waraka Desemba 15 na haraka ikaanza kutumika, hatukudanganya na barua tuliyopeleka Wizarani na taarifa za kikao zilisema hivyo.
Kuhusu kupigwa stop kwa uchaguzi wa TFF baada ya aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais Richard Rukambura kwenda mahakamani kwa kupinga kuenguliwa kwake Tenga alisema "Mpaka sasa mimi sijaona samsa ya mahakamani kwa hiyo siwezi kuzungumza lolote kwa sasa."