Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema matokeo ya kidato cha nne bado hayajakamilika na kuwa habari zilizozagaa wiki hii kuwa yapo tayari si za kweli.
Hata hivyo Baraza hilo limebainisha kuwa licha ya kutokamilika, matokeo hayo yanakaribia kutoka kwa mujibu wa ratiba za baraza hilo ambapo hutakiwa kutoa matokeo hayo mwezi Februari.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa NECTA, John Nchimbi amesema uvumi wa kwamba matokeo hayo yako tayari ulitokana na kuzushwa kupitia mtandao wa kijamii (Facebook).
Alifafanua kwamba habari kuwa matokeo hayo yameanza kutoka kisirisiri kabla hayajatangazwa rasmi na kwamba hatua hiyo inalenga kuyachakachua, siyo taarifa sahihi.
Aliwataka wananchi kuwa makini na uvumi huo kwa vile endapo matokeo hayo yatakuwa tayari yatatangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo na pia kuwekwa kwenye tovuti ya Baraza pamoja na wananchi kuweza kuyapata kupitia simu zao za mkononi.