Ndugu zangu,
Leo ni mwisho wa mwezi wa mwaka mpya. Na mwaka ulivyo ni kama noti ya shilingi elfu kumi ya Bongo. Ukiichenji tu, utashangaa inavyopukutika!
Ukae sasa ukijua, kuwa kesho ndio Februari Mosi. Hivyo, mwaka mpya wa 2013, kama ilivyo kwa noti elfu kumi, ndio tutakuwa tumeuchenji. Subiri sasa uone siku, wiki na miezi inavyopukitika. Fumba na kufumbua utasikia tumeshaingia Juni tunaelekea Bajeti ya Serikali ya Julai, na ukitoka hapo utafikiri mwaka unateremsha milima ya Kitonga.
Inatukumbusha nini?
Umuhimu wa kupanga mambo yetu. Inahusu muda na matumizi ya muda. Na mwanadamu usipokuwa makini na muda, itakuwa sawa na kisa kile cha mzazi aliyeulizwa na wanawe; " Mbona nguo za Krismasi hatujanunuliwa?"
Mzazi akawajibu wanawe; " Jamani, Krismasi ya mwaka huu imekuja ghafla sana!"
Kana kwamba hakujua, kuwa kwenye kalenda ya mwaka tarehe ya Krismasi imeshawekwa, Desemba 25!
Ndio, Afrika mvua hainyeshi ghafla, huwa kuna dalili zake. Na katika maisha, mambo mengi hayaji ghafla, bali hutukuta tukiwa hatujajiandaa. Jiandae na mwaka unaoanza kupukutika kuanzia kesho, kama noti ya shilingi elfu kumi. Kila la kheri.