MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Taifa ( UWT), Sophia Simba (aliesimama), ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,ameshangazwa na kitendo cha Diwani wa Kata ya Nyandira kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA), Luanda Zengwe ,kushindwa kuwaondolea wananchi wake kero mbalimbali tangu achanguliwe ikiwemo kushirikiana na Halamshauri ya Wilaya a Mvomero kuwezesha kupatikana kwa kitanda maalumu cha kubeba wagonjwa.
Badala yake amekuwa mstari wa mbele kuwahamisha vijana na wanachama wa chama hicho na pia kuzomea na kuwaletea fujo viongozi wa Serikali ya chama Tawala ( CCM) wanaotembelea kwenye Kata hiyo kwa madhumuni ya kukutana na wananchi ili kupata kero zao mbalimbali na kuzitolea majawabu ya msingi.
Mwenyekiti wa Taifa wa UWT, alishangazwa na hatua hiyo ya kushindwa kutatua kero hizo na badala yake kuondoka eneo la meza kuu Chadema na kwenda kuwahamasisha wafuasi wake wafanye fujo wakati wa mkutano ulioanmdaliwa na UWT kwa wananchi wa Kata ya Nyandira.
Diwani Luanda alipandwa na munkari, baada ya Diwani wa zamani wa CCM wa Kata hiyo , Modesta Lubasije kuwasilisha kero kwa Mwenyekiti wa Taifa wa UWT juu ya ukosefu wa kitanda cha kubeba wagonjwa ‘ Strecha ‘ hasa akina mama wajawazito kwenye Zahanati ya Kijiji cha Nyandira hali inayosababisha kutumia machela za miti.
Kutokana na hoja hiyo, Mwenyekiti wa UWT Taifa na Waziri alimgeukia Diwani waliyekuwa ameketi pembezoni mwa meza kuu na kumtaka wakati ukifika awezekujibu kero za wananchi na wapigakura wake , alitolee majibu huku akimsisitizia kuwa suala hilo si la Waziri bali lipochini ya uwezo wa Diwani kwa kushirikiana na Diwani wa Viti maalumu wa Tarafa ya Mgenta pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Hata hivyo kufuatia kuelezwa suala hilo, Diwani huyo alinyanyuka ghafla kutoka meza kuu na kuanza kutoa maneno makali ya kejeri na kumshutumu Waziri Simba kwa kudai swali hilo lililenga kuchafua na hivyo kusababisha kuzuka kwa tafrani za dakika kadhaa na baadaye mkutano kuendelea kama kawaida.
Kutokana na kitendo chake cha kutoa lugha chafu mbele ya Waziri Simba, alimua kunyanyuka na kuindoka meza kuu na kwenda kwa wafuasi wake ambao walijipanga kufanya fujo na kuanza kupiga mayowe na kurushiana vijembe hali iliyowafanya baadhi ya Viongozi wa CCM na UWT chini Katibu wa CCM Wilaya ya Mvomero,Sadakati Kimati kwenda kumdhibiti Diwani huyo wakisaidiwa na Askari Polisi wa eneo hilo.
Waziri Simba akiendelea na mkutano huo, aliwataka wananchi kuona umuhimu wa kuchangua viongozi wenye busara na hekima , kwani kitendo cha utovu wa nidhamu uliooneshwa na Diwani wa Kata hiyo ni kuonesha ni namna gani siasa ya Vyama vya Upinzani zilivyo hapa nchini.
Akizumza kama Mwenyekiti wa Taifa wa UWT, Simba aliwahimiza wana CCM na wananchi wa Kata hiyo kutofanya makosa wakati wa uchaguzi mkuu ujao na badala yake warejeshe uongozi wa CCM katika Kata hiyo.
“ Wananchi wa Nyandira hii ndiyo siasa za wenzetu hawa , baada ya kujionea mwenyewe, ninaahidi panapo majaliwa mwaka 2015 nitatia timu hapa kuendesha kampeni ya nguvu ili Kata hii isiendelee kuwa chini ya watu walevi , ambao hawataki maendeleo ya wananchi “ alisema Simba.
Hata hivyo alisema, maendeleo lazima yaletwe na wananchi kwa kushirikiana na viongozi , hivyo burasa inahitajika pale viongozi wanapofika kwenye eneo kama hilo na wananchi wanayo haki ya kutoa kero zao na kuzipatia majawabu ya msingi.
Kufuatia ombi hilo , Waziri Simba aliahidi kutoa fedha za kununua kitanda maalumu cha kubeba wagonjwa katika Zahanati hiyo ya Kijiji na kuwataka wananchi wenye kupenda amani wampuuze Diwani huyo pamoja na wafuasi wake ambao wao hekima na busara zimewashinda.
Kwa upande wake Diwani Luanda, alidai kuwa , ziara ya Waziri Simba haikuwa ya kiserikali na badala yake ililalia kwenye Chama chake zaidi na yeye kama Diwani wa Chadema wa Kata hiyo alikuwa na wajibu na haki ya kuona wanachama na Chama chake hakichafuliwi.
Zengwe lilianzia hapa ambapo Diwani wa Kata ya Nyandira kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA), Luanda Zengwe (katikati) aliponyanyuka na kuanza kujibizana na Diwani wa zamani wa CCM wa Kata hiyo ,Modesta Lubasije aliyekuwa akiwasilisha kero mbali mbali kwa Mwenyekiti wa Taifa wa UWT,Mh. Sophia Simba (kushoto).
Katibu wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) Wilaya ya Mvomero, Sadakati Kimati akimdhibiti vilivyo Diwani wa Kata ya Nyandira, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA ), Luanda Zengwe, (mwenye skafu), mbele ya Askari Polisi, Sajini Taji aliyefahamika kwa jina la S .E Mndeme kutoka Kituo cha Polisi Mgeta , mara baada ya kutoa maneno ya lugha chafu kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii , Jinsia na Watoto, Sophia Simba ambaye pia ni Mwenyekiti wa UWT Taifa ( hayupo pichani) alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kata hiyo , Januari 19, mwaka huu, Diwani Luanda alikaribishwa akiwa ni mwakilishi wa wananchi kuketi meza kuu.
Diwani wa Kata ya Nyandira kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA), Luanda Zengwe akiingilia mkutano huo na kuanza kuongea na Wananchi wa Kata hiyo.