Ushirikiano wa pamoja baina ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na wadau wa maendeleo nchini umeiwezesha taasisi hiyo kuwasaidia na kuwainua wanawake kiuchumi ambao wameweza kujishughulisha na kazi za ujasiriamali na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Pia Taasisi hiyo imeweza kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi jambo ambalo limewafanya watoto hao wapate elimu sawa watoto wengine wenye wazazi na kuimarisha afya za mama wajawazito na watoto.
Hayo yamesemwa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati alipotembelea Taasisi inayoshughulika na masuala ya watoto (France Parrainages) kiliyopo mjini Paris ambacho kinafanya kazi na Kituo cha Ufaransa cha kuwaangalia watoto kwa kushirikiana na Taasisi ya Partage Tanzania inayohudumia watoto yatima katika mkoa wa Kagera.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA alisema kuwa Taasisi hiyo imeweza kujenga shule ya Sekondari ya WAMA – NAKAYAMA iliyopo Rufiji Mkoani Pwani ambayo ina wanafunzi 247 ambao ni watoto yatima na matarajio ya baadaye ni kuwa na wanafunzi 780.