Mkurugenzi wa Mad Mad Entertainment, Yasmin Razak (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu kampuni yake kuingia mikataba na wasanii wa filamu wa Tanzania watakaokwenda Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kutengeneza filamu. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Superior, Issack Kasanga na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba.
Msanii wa filamu, Steve Nyerere (kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano huo.Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Superior, Issack Kasanga na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba.
Na Ripota Wetu.
KAMPUNI ya Mad Mad Entertainment iliyopo jijini London nchini Uingereza, imeanzisha program maalum ya kupeleka wasanii wa filamu za bongo nje ya nchi kwa lengo la kukuza sanaa hiyo hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Yasmin Razak alisema ameamua kufanya kazi na wasanii hao ili kuleta mabadiliko na kuwakwamua kiuchumi wasanii wa filamu hapa nchini.
“Kwa muda mrefu niliokaa London sioni kama sanaa hii ina maendeleo, nikafikiria kitu gani nifanye ili kukuza tasnia hii, katika mkataba na kampuni msanii atakayetengeneza filamu na wasanii wa nje atalipwa kiasi cha sh 50 milioni pamoja na malipo mengine yatakayokuwepo kwenye mkataba, ikiwa ni pamoja na asilimia fulani kwa kila kazi itakayouzwa hapa nchini.
“Nimekuwa nikifanya kazi hiyo na wasanii wengi kutoka Nigeria wakiwemo kina Omotola, Two Face na wengineo na pia Ghana, Congo na hata Uingereza, hivyo nimeonelea kuwa itakuwa vema Tanzania nao kuingia katika mchakato huo,”alisema Razak.
Razak ambaye amewahi kufanya kazi ya filamu na Fally Ipupa, alitaja vigezo vya msanii atakayechaguliwa ikiwa ni pamoja na umaarufu, kuijua lugha ya kiingereza, uwezo wa kuigiza na kuuvaa uhusika wowote pamoja na mavazi.
Naye rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba aliwataka wasanii hao kujipanga katika kuhakikisha wanaingia kwenye ushindani huo na kuwataka wale watakaochaguliwa kujituma na kuonyesha nidhamu ya uhakika.
“Hapa kuna kuinua vipaji, soko la kimataifa na mengineyo, hivyo ni vema kufanya kazi kikamilifu kwa wale watakaochaguliwa na si kujisahau, wanatakiwa wasanii watatu na tupo katika hatua za awali za mchujo,” alisema
Mwakifamba.
Naye muigizaji Issa Musa maarufu kama Cloud, alisema kuwa lugha itakuwa ni tatizo kubwa kwa wasanii walio wengi, hivyo kuitaka kampuni hiyo iangalienamna ya kuweza kuwasaidia wasanii hao.