NA MIZA KONA / HABARI MAELEZO ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kulivunja Shirika la Utalii Zanzibar kutokana na changamoto zinazolikabili Shirika hilo hivi sasa.
Akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2013/2014 huko katika Baraza la Wawakilishi Chukwani,Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk amesema sababu kubwa ya kuvunjwa shirika hilo ni kushindwa kuhimili ushindani uliopo wa biashara ya sekta hiyo.
Amesema kuwa taratibu za kulivunja rasmi Shirika la Utalii la Zanzibar zinatarajiwa kukamilika katika muda mfupi ujao kuanzia sasa.
Akizungumzia Shirika la Utangazaji Zanzibar(ZBC) amesema linatarajia kuweka vifaa vipya vya Studio pamoja na kununua gari moja ya kurushia matangazo ya moja kwa moja kutoka nje ya studio hasa katika sherehe na maadhimisho ya Kitaifa.
Waziri Said Ali Mbarouk amesema lengo la Wizara ni kusimamia mazingira bora ya kazi ili kuliwezesha Shirika la ZBC kutoa huduma bora na zenye ufanisi.
Akitoa maoni ya Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari Mwenyekiti wa kamati hiyo Mlinde Mbarouk Juma wameshauri watendaji wa Shirika la Utangazaji Zanzibar kubadilika kiutendaji. kufanyakazi kwa umakini zaidi na kuacha kufanyakazi kwa mazoea .
“Kwa kuwa uendeshaji wa Mfumo wa Digital unahitaji umakini wa hali ya juu kwa kutokuwa makini tutakuja kulaumiana na kuona ni bora tungelibaki katika mfumo wa analogia”, alisema Mwenyekiti Mlinde.
Aidha ameeleza kuwa Utalii ni chachu ya maendeleo katika nchi jirani, lakini bado Zanzibar haujapewa kipaumbele na kuwekewa mikakati na kuwanufaisha wananchi wengi.
“Kamati inatoa rai kwamba dhana ya Utalii kwa wote itekelezwe kwa vitendo na wala sio maneno pamoja na kuwekwa sera na sheria ambazo zitapunguza gharama kwa wazawa.” Alisisitiza Mlinde.
Wameishauri Wizara kujidhatiti katika kuutangaza Utalii wa Zanzibar kwani kufanya hivyo utaweza kuongeza soko katika mataifa mbali mbali na kuitangaza katika nchi za jirani.
Katika kutekeleza majukumu yake Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo imeomba iidhinishiwe jumla ya shilingi 9,985,000,000 kwa kazi za kawaida na shilingi 510,000,000 kwa kazi za maendeleo.