Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwenye mechi ya marudiano ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) itakayochezwa Jumamosi jijini Kampala.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo, Kim amesema tangu kikosi chake kimeingia kambini Julai 14 mwaka huu, wachezaji wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mazoezi na wako tayari kwa ajili ya mechi hiyo.
“Uganda ni timu bora kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Mechi itakuwa ngumu, tunaamini tunakwenda kufanya vizuri. Tayari tunayo mikakati kwa ajili ya mechi hiyo, tunakwenda kuikamilisha Kampala,” amesema Kim.
Hata hivyo, Kim amesema licha ya mwitikio mzuri wa wachezaji kwenye mazoezi lakini wanakabiliwa na changamoto ya wengi wa wachezaji kuwa wamefunga wakati wachezaji wanapokuwa kambini wanatakiwa kula, kunywa na kupumzika.
“Hiki ni kipindi kigumu kwa mpira wa miguu, na suala la kufunga ni la kiimani ambapo hatuwezi kuwazuia wachezaji kufunga. Karibu nusu ya wachezaji wanafunga, hii ni changamoto ambayo tunaiheshimu,” amesema Kim na kuongeza kuwa ni wazi kikosi chake cha kwanza kitakuwa na mabadiliko baada ya beki Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio nchini Uholanzi.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaondoka Mwanza kesho (Julai 24 mwaka huu) saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir na kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 8.15 mchana.
Wachezaji waliomo kwenye msafara huo ni makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.
Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)