Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kocha wa zamani wa Taifa Stars, Bert Trautmann (89) kilichotokea jana (Julai 19 mwaka huu) nchini Hispania.
Kabla ya kuwa kocha, Trautmann aliyezaliwa 1923 mjini Bremen, Ujerumani alikuwa kipa wa timu ya Manchester City ya Uingereza ambapo anakumbukwa kwa kucheza mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Birmingham City akiwa amevunjika shingo.
Manchester City ilishinda fainali hiyo iliyochezwa mwaka 1956 mabao 3-1. Trautmann ambaye aligongana na mshambuliaji wa Birmingham, Peter Murphy zikiwa zimesalia dakika 17 mechi hiyo kumalizika aligundua kuwa amevunjika shingo siku tatu baadaye.
Mbali ya kuwa kocha wa Taifa Stars mwanzoni mwa miaka ya 60, Trautmann pia alikuwa mkufunzi wa makocha ambapo hapa nchini aliendesha kozi mbalimbali zilizotoa makocha waliokuja kutamba baadaye.
TFF itamkumbuka Trautmann kwa mchango wake aliotoa katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini ikiwemo wazo lake la kuanzishwa kwa Ligi Kuu (Daraja la Kwanza) ambalo alilitekeleza katikati ya miaka ya 60.
Msiba huo ni pigo kwa familia ya Trautmann, TFF na familia ya mpira wa miguu kwa ujumla nchini kutokana na mchango alioutoa kwa Tanzania hasa wakati akiwa kocha na mkufunzi wa makocha.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Trautmann, Chama cha Mpira wa Miguu cha Ujerumani (DFB), Chama cha Mpira wa Miguu cha Uingereza (FA) na kuwataka kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Bert Trautmann mahali pema peponi. Amina
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)